2018-01-03 06:54:00

Kardinali Kurt Koch: dini na amani vinategemeana na kukamilishana!


Ni matumaini ya Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2018, viongozi wa Makanisa wataendelea kuimarisha mchakato wa uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwaka 2017 umeshuhudia matukio ya kiekumene yaliyowakutanisha viongozi mbali mbali wa Makanisa kama kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano ili kubomoa kuta za utengano ambazo zimekuwepo miongoni mwa Makanisa haya kwa miaka mingi!

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, Wakristo wanapaswa kushikamana ili kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili hatimaye, siku moja Wakristo wote waweze kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Uekumene wa damu unafumbatwa katika dhana ya: mauaji, nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaouwawa si kutokana na madhehebu yao, bali imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Uekumene na Ubatizo wa damu, tayari umekwisha waunganisha Wakristo huko mbinguni, mbele ya Mwana Kondoo wa Mungu.

Kardinali Kurt Koch katika mahojiano maalum na Shirika la Habari la Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, SIR anakiri kwamba, Mwaka 2017 umekuwa ni mwaka uliosheheni matukio changamani ya kiekumene. Mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Wakristo pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani inayopelekea uvunjifu wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Wakristo wote wanaunganishwa kwa namna ya ajabu na Uekumene wa damu. Kipindi hiki cha Noeli, ujumbe unaosikika ni amani duniani na kwamba, dini na amani vinapaswa kuwa ni chanda na pete. Uekumene wa damu ni dhana iliyoibuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa kitume, Ut Unum Sint” yaani “Ili wote wawe wamoja”. Uekumene wa damu uwasaidie Wakristo kushikamana katika sala na kusaidiana kadiri ya uwezo.

Kardinali Koch anasema licha ya mauaji, dhuluma na nyanyaso za kidini, bado Wakristo wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kusamehe na kusahau, kama alivyofanya  Mtakatifu Stefano Shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Msamaha, haki, amani na upatanisho ni tunu msingi ambazo Wakristo wanaweza kuzishuhudia katika ulimwengu mamboleo kama kielelezo cha mchakato wa kumwilisha Fumbo la maisha ya Kristo. Uekumene unapaswa pia kukuzwa na kudumisha umoja, udugu na mshikamano miongoni mwa Wakristo wakati wa raha na shida. Patriaki Tawadros wa Kanisa la Kikoptik la Misri ana tasaufi kubwa sana ya uekumene wa sala, ndiyo maana ametenga tarehe 10 Mei kila mwaka, maadhimisho ya Siku ya Urafiki kati ya Waorthodox na Wakatoliki. Urafiki huu unapaswa kufumbatwa katika maisha ya waamini wa kawaida kiasi hata cha kuwafikia viongozi wa Kanisa.

Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani limekuwa ni tukio lililoadhimishwa kiekumene, kwa kuwashirikisha viongozi wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo, huko Lund, nchini Sweden. Tukio hili ni matunda ya majadiliano ya kiekumene tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Itakumbukwa kwamba, mwaka 2017, Mama Kanisa amefanya kumbu kukmbu ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili Vatican walipochapisha Tamko juu ya Uekumene ”Unitatis Redintegratio”. Matunda ya majadiliano haya ni Tamko la pamoja juu ya Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki lililochapishwa kunako mwaka 1999 pamoja na Tamko ”Kutoka kwenye kinzani kuelekea kwenye umoja”, msingi wa maadhimisho wa Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani.

Mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaendelea kusonga mbele kutoka katika kinzani, vita na mipasuko ya kidini kwa kuanza kuambata toba, wongofu na upatanisho, ili kuanza kuandika ukurasa mpya wa kiekumene unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo na Kanisa lake, ili watu wengine pia waweze kuamini! Makanisa hayana budi kumshukuru Mungu kwa hatua kubwa ambayo imefikiwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika kipindi cha miaka 50 iliyopita na kwamba, huu ni msingi thabiti wa matumaini ya umoja wa Wakristo!

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya waamini wa Kanisa la Kiorthodox la Russia na Moscow! Wao wanaunganishwa na Uekumene wa watakatifu. Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Cyrill wa Russia na Moscow nzima, walikutana mjini Havana, Cuba, mwezi Februari 2017. Mchakato unaendelea ili kuwawezesha viongozi wa Makanisa haya kuweza kukutana tena anasema Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa Linalohamasisha Umoja wa Wakristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.