2017-12-31 13:30:00

Familia zifufuke na kutembea katika utu, ukristo na tunu za Kiinjili


Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni mwaliko kwa waamini kutafakari mang’amuzi ya Familia Takatifu yaliyofumbatwa katika upendo wa dhati, imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu waliweza kushuhudia imani hii kwa kumtoa sadaka Yesu kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyoandikwa kwenye Torati ya Musa. Wazazi wa Yesu wakaenda Hekaluni Yerusalemu kumtoa sadaka kwa kutambua kwamba, Mtoto wao ni mali ya Mungu na kwamba, wao wamepewa dhamana ya kulinda maisha yake na wala si wamiliki wa mtoto wao!

Hii inaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu ni Bwana wa historia ya maisha ya kila mtu na familia katika ujumla wake, kila kitu kinapata chimbuko lake kutoka kwa Mungu! Kila familia inapaswa kutambua nafasi ya kwanza ya Mungu katika maisha, kwa kuyalinda na kuwalea watoto ili kumwelekea Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya maisha. Huu ndio ushuhuda wa siri ya maisha ya ujana wa Familia ya Nazareti kama unavyosimuliwa  na Mzee Simeoni pamoja na Nabii Ana, binti Fanueli. Mzee Simeoni anamshukuru Mungu kwa kusema, “Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa… ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi”. Lk. 2: 34-35.

Hii ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 31 Desemba 2017 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, katika maadhimisho ya Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Unabii uliotolewa na wahenga unaonesha kwamba, ujio wa Kristo Yesu unapania kuvua sura potofu ya Mungu inayooneshwa na binadamu, ili kupingana na malimwengu ambayo mwanadamu anapenda sana kuyakumbatia. Lengo ni kuwawezesha watu “kufufuka” na kuanza kutembea katika utu na ukristo unaosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili. Familia zote zinaguswa na mchakato wa kuzaliwa na kufufuka, ili kuganga na kuponya madonda yanayotokana na udhaifu na makosa ya kibinadamu, ili kurejea tena kwenye chemchemi ya mang’amuzi ya Kikristo yanayowafungulia njia na fursa mpya katika maisha! Injili ya siku inafafanua jinsi ambavyo Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walivyorejea nyumbani kwao Nazareti baada ya kukamilisha Sheria ya Mungu na Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo huku akimpendeza Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, furaha kubwa ya familia ni ukuaji wa watoto wake, wanaopaswa kuendelezwa na kuimarishwa, ili hatimaye, waweze kupata hekima na kuambata neema ya Mungu katika maisha, kama ilivyotokea kwa Kristo Yesu anaye onesha mshikamano na binadamu, kwani hekina na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walifurahia sana kuona yote haya yana mwilishwa katika maisha ya Mtoto wao; utume ambao unapaswa kutekelezwa na familia. Ni wajibu wa familia kuunda mazingira rafiki yatakayosaidia ukuaji na ukamilifu wa watoto wao, ili waweze kuishi maisha mema kadiri ya mpango wa Mungu na ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi. Haya ndiyo matashi mema ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuzitakia familia zote, huku akiziombea na kuziweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa Familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.