2017-12-30 09:53:00

Kampeni ya Utoto Mtakatifu dhidi ya kazi za suluba nchini India!


Shirika la Utoto Mtakatifu nchini Ujerumani linaloundwa na watoto zaidi 2, 600, Ijumaa, tarehe 29 Desemba 2017 limezindua kampeni ya Siku kuu ya Epifania kwa Mwaka 2018 ambayo inapania kuchangisha fedha kwa ajili ya mapambano ya kutokomeza kazi za suluba miongoni mwa watoto wadogo sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee nchini India. Watoto hawa wakiwa wamevaa kama Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali wanapita nyumba kwa nyumba huku wakizibariki kwa Jina la Kristo Yesu “C+M+B” yaani “Christus Mansionem Benedicat” “Kristo Abariki Nyumba hii” na kukusanya fedha kwa ajili ya kuchangia mapambano dhidi ya kazi za suluba nchini India.

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa anasema, huduma ya watoto hawa ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Watoto hawa kama walivyokuwa Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali wanaongozwa na nyota kumwendea Kristo Yesu, ambaye kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ameuinua ubinadamu uliokua umechakaa kwa kufanana na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakuna na dhambi. Umoja, mshikamano na upendo ndiyo mambo makuu yanayowasukuma watoto hawa kuchapa mwendo kuzungukia nyumba za Wajerumani kwa ajili ya kutafuta fedha za kugharimia miradi mbali mbali ya maendeleo endelevu sehemu mbali mbali za dunia.

Shirika la Kazi Duniani, ILO linabainisha kwamba,  duniani kuna watoto milioni 168 wenye umri kati ya miaka 5 -17 wanaofanyanyishwa kazi za suluba, ambayo ni asilimia 11% ya watoto wote ulimwenguni. Kati yao pia kuna watoto milioni 85 wanaonyonywa kwa kufanyishwa kazi ngumu kinyume kabisa cha umri wao. Askofu Klaus Kramer, Rais wa Shirika la Utoto Mtakatifu nchini Ujerumani lililoanzishwa kunako mwaka  1959 anasema, fedha inayokusanywa na watoto inasaidia kugharimia huduma ya elimu, ili kuwajengea uwezo wa kukua; kiakili, kimaadili, kiroho, kiutu na kitamaduni.

Dhamana hii inatekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kutoka kwenye Makanisa mahalia. Kwa bahati mbaya kuna watoto wanaofanyishwa kazi ngumu kwa kuwa wamegeuzwa kuwa ni vitega uchumi vya familia zao. Watoto hawa wamekwisha kukusanya zaidi ya Euro bilioni moja, ambazo zimegharimia miradi 71, 700 kwa ajili ya watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kundi la Watoto wa Utoto Mtakatifu kutoka Austria, Uswiss, Italia, Ungheria na Slovachia, wanatashiri ki katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Papa Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 1 Januari 2018, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Siku ya Kuombea Amani Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.