2017-12-30 14:03:00

Familia thabiti inasimikwa katika sala, ushuhuda wa imani na furaha!


Noeli ni sherehe pia ya kifamilia. Huwakusanya kusherekea pamoja wanafamilia na kudumisha undugu na mahusiano mema kati yao. Ndiyo maana kabla ya kumaliza kipindi hiki cha Noeli Kanisa linatupatia nafasi ya kuadhimisha sherehe ya Familia Takatifu ya Nazareti,  Familia ya Yesu Maria na Yosefu. Kanisa linatupatia Familia Takatifu kama kielelezo kwa familia zetu zote likizialika kujifunza kutoka Familia Takatifu tunu za kifamilia na kujifunza namna ya kuzifanya familia zetu pia ziwe Takatifu.

Katika muundo wa familia kila mwanafamilia anayo nafasi yake na anao wajibu wake wa kutimiza kwa ajili ya ustawi wa familia. Maandiko Matakatifu siku ya leo yanakazia juu ya nafasi na wajibu mbalimbali za wanafamilia.  Watoto wanawaalika kutambua kuwa wanao wajibu wa kuwapa heshima wazazi wao. Tena linaongeza kuwa mtoto anayeheshimu wazazi hujichotea baraka tele toka kwa Mwenyezi Mungu. Somo la Injili linajelekeza kwa wazazi. Linawaalika kutambua kuwa ni sehemu ya wajibu wao wa msingi kuwaelekeza watoto kwa Mungu kama Maria na Yosefu walivyomtolea Yesu hekaluni.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki hufundisha kuwa familia ndio kiini cha maisha ya jamii. Ni mlango ambapo mtu huingia katika jamii na hapo hapo akijifunza tunu za kimaadili, hofu ya Mungu na namna ya kutumia vema uhuru wake (KKK, 2207).  Familia ni kanisa la nyumbani linalotekeleza kazi ya Kristo ya kikuhani katika kuishi roho ya sala; ya kinabii katika kufundisha na kuishi kweli za kimungu na ya kifalme katika kueneza fadhila zinazojenga ufalme wa Mungu. Hivi inakuwa kweli  ni shule ya kwanza na ya msingi katika malezi na makuzi ya mtu kama mwana jamii na hasa kama mwana wa Mungu. Tunapoziangalia familia zetu katika mwanga huu wa mafundisho ya Kanisa na pia wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu tunamshukuru Mungu kwa ajili ya familia ambazo zinatoa ushuhuda misingi hii.  Familia hizi ni pamoja na zile jumuiya zinazoishi kifamilia kama jumuiya za mapadre, jumuiya za watawa, n.k. Tunaziombea ziendelee kudumu na kuwa ushahidi wa uwepo wa tunu za familia takatifu katika ulimwengu wa leo.

Zipo pia familia ambazo kwa sababu moja au nyingine bado hazijaweza kuishi tunu hizi kati yao. Badala ya kuwa ushuhuda wa uwepo wa tunu za familia takatifu, zimekuwa na sura ya kukosa imani, utengano, chuki, kutokujaliana, kukata tamaa na mambo mengine kama hayo. Hapa pia ni pamoja na jumuiya zinazoishi kifamilia kama jumuiya za mapadre, jumuiya za watawa, n.k. Hizi pia leo tuziombee ili kwa neema ya Mungu ziweze kuamka na kusonga mbele kuelekea utakatifu kama ule wa familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia ndiyo msingi wa jamii na Kanisa. Familia bora huunda jamii bora na kanisa lililo na waamini bora. Familia iliyo msingi wa jamii na wa kanisa, nayo hujengwa juu ya misingi yake. Lakini kama anavyohoji mzaburi “misingi ikishaharibika mwenye haki atafanya nini? (Zab. 11:3), ikiwa familia haitaundwa wala kuishikilia misingi yake itakuwa katika hatari ya kuporomoka. Baba Mtakatifu Francisko wakati akiadhimisha Sherehe ya Familia Takatifu ndani ya Mwaka wa Imani alikazia misingi mitatu kati ya mingi inayounda familia dhabiti.

Sala ya Familia: Sala ya familia ambapo wanafamilia hukusanyika nyumbani na kusali pamoja ni msingi unaoimarisha familia. Papa anakiri kwamba kuna familia ambazo namna zinavyoishi hazioni kama zina nafasi nzuri ya kusali au pengine zinaona hazina muda kabisa. Lakini hapo hapo anahoji, ni mazingira magumu kiasi gani yatazuia hata wanafamilia kusali Baba yetu moja kwa pamoja hata wakiwa mezani? Je hicho kitakuwa kitu cha ajabu? Hata katika mazingira magumu tunahitaji kujinyenyekeza na kusali kukiri kwamba tunahitaji msaada wa Mungu. Tena sala ya Rosari takatifu inayosaliwa kifamilia ni chanzo kikubwa sana cha nguvu katika familia. Familia inayosali pamoja hukaa pamoja! Zaidi ya sala ya kifamilia, Papa anasisitiza ni muhimu kwa wanafamilia kuombeana. Mke kumwombea Mume, Mume kumwombea Mke, wazazi kuwaombea watoto, watoto kuwaombea wazazi na kuombeana wao kwa wao. Hata katika jumuiya za mapadre na za watawa, wanajumuiya wanaoombeana hujikwamua kutoka changamoto nyingi za maisha ya kijumuiya.

Familia kurithisha na kushuhudia Imani: Papa anasisitiza kuwa ni muhimu kwa familia kutoa ushuhuda wa imani na kuirithisha kwa vizazi vinavyokuja. Anasema imani si kama hazina au fedha ambazo mtu huzitunza benki apate faida. Imani inahitaji kusambazwa na kurithishwa kama namna ya kutoa ushuhuda. Familia ni mahala muafaka pa kuridhisha imani kwa watoto. Hapa unalala wajibu unaokaziwa na somo la leo la injili: wajibu wa wazazi kuwapeleka watoto wao kwa Mungu. Ndio kuwalea kwa misingi ya imani na hatua kwa hatua kuwakomaza katika tamatuni za imani ya kikristo.

Familia kufurahi pamoja: Papa anauliza, mambo huwaje pale familia inapokuwa na furaha? Bila shaka familia inapokuwa na furaha huwa na umoja; watu husikilizana, husaidiana na huaminiana. Furaha ya namna hii katika familia hailetwi na fedha wala mali, bali huletwa na uwepo wa Mungu katika familia. Ni uwepo ambao huzipa familia upendo hata katika magumu, huzipa uvumilivu na saburi. Lakini yote haya huwezekana pale ubinafsi unapowekwa kando na kila mwanafamilia kutafuta furaha ya familia nzima. Katika sherehe ya leo ya Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, Mwenyezi Mungu na aziimarishe familia zetu katika sala, imani na furaha ya uwepo wake na kwa neema yake ziweze kufanana na familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Bikira Maria Malkia wa Familia, atuombee.

Padre William Bahitwa.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.