2017-12-29 15:43:00

Jimbo Kuu la Torino na mbinu mkakati wa utume kwa vijana!


Baba Mtakatifu Francisko  hivi karibuni ametangaza kwamba kuanzia tarehe 19 Marchi 2018 Sherehe ya Mtakatifu Yosefu mchumba wake Bikira Maria hadi tarehe 24 Machi 2018, kutaadhimishwa utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Baba Mtakatifu anasema, hii ni safari ya maisha ya Kanisa katika kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana, kuwajali, kuwaimarisha katika imani pamoja na kusikiliza changamoto zinazotolewa na vijana wa kizazi kipya. Hitimisho la maadhimisho haya litawasilishwa kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu itakayoadhimishwa rasmi mwezi Oktoba, 2018.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Furaha ya Injili anasema kwamba, Uinjilishaji wa kweli katika ulimwengu mamboleo unajikita kwa namna ya pekee kabisa katika ushuhuda wa imani tendaji unaomtangaza Kristo Yesu kuwa kweli ni Bwana na Mwalimu. Hii ndiyo Furaha ya Injili inayopaswa kumwilishwa katika maisha ya vijana wa kizazi kipya wanaokabiliana na changamoto nyingi za maisha katika ulimwengu huu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Watu wa Mungu kwa nyakati zote wanapaswa kutangaziwa kwamba, Kristo aliteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua changamoto za maisha ya ndoa na familia aliliwezesha Kanisa kuadhimisha Sinodi mbili za Maaskofu na matunda ya maadhimisho haya ni Wosia wa Kitume “Furaha ya Upendo ndani ya Familia” Amoris Laetitia!

Kama sehemu ya mwendelezo wa tafakari hii ya kina katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Sinodi ya Maaskofu kwa Mwezi Oktoba, Mwaka 2018 ijikite ili kuangalia njia bora zaidi ya kufundisha na kurithisha imani kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na kuwasaidia kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha yao ya ujana, kwani waswahili wanasema, ujana mali, lakini fainali uzeeni! Kanisa linapenda kuwasaidia vijana kufurahia maisha ya ujana sanjari na kukabiliana na changamoto za maisha ya ujana kwa ari na moyo mkuu bila kuyumba wala kuteteleka katika misingi ya imani, matumaini na mapendo ya Kikristo!

Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, nchini Italia, kwa kutambua na kuthamini maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ameandika Barua ya Kichungaji kwa mwaka 2017-2018 kwa ajili ya vijana na walezi wao, inayoongozwa na kauli mbiu “Mwalimu, una kaa wapi?” Ni barua inayojikita kwa namna ya pekee katika maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ambayo imeitishwa na Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni mwendelezo wa majiundo endelevu wa familia ya Mungu, Jimbo kuu la Torino, ambalo kwa miaka ya hivi karibuni imejikita zaidi katika kukuza na kudumisha mahusiano kati ya vijana wa kizazi kipya na “wahenga”. Hii ni tafakari inayofumbatwa kwa namna ya pekee katika maisha na utume kwa Kanisa la Kiulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Jimbo kuu la Torino kuanzia tarehe 21 hadi 22 Juni 2015 alitenga muda mwingi wa kuweza kukutana na kuzungumza na vijana, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Mtakatifu Yohane Bosco, chachu ya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana. Kumbe, huu ni mwendelezo wa tafakari ya changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Torino.

Barua hii ni mwongozo, taratibu na dira kwa maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa Jimbo kuu la Torino. Lengo ni kukazia majiundo ya awali na endelevu katika maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kitaaluma, ili kuwajenga na kuwafunda vijana wanaoweza kupambana na changamoto kutoka katika medani mbali mbali za maisha, na wakabaki salama na thabiti katika imani kwa Kristo na Kanisa lake. Maisha na shughuli mbali mbali zinazofanywa kwa ajili ya vijana zinapaswa kuwa ni sehemu ya majiundo yao ndani ya Kanisa, ambamo wamezaliwa kwa “Maji na Roho Mtakatifu”; mahali ambamo, wanaendelea kulishwa kwa Neno la Sakramenti za Kanisa.

Utume kwa vijana, ni fursa makini inayopaswa kutumiwa vyema kwa ajili ya ukuaji na ukomavu wa vijana wa kizazi kipya kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili; kitamaduni, kijamii, kielimu; kimaadili na kiutu! Vijana watambue umuhimu wa kazi kama sehemu ya utimilifu wa maisha na utu wa binadamu; umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Vijana wawe na ujasiri wa kujenga utamaduni wa upendo, udugu na mshikamano na wahamiaji pamoja na wakimbizi wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.

Vijana wawe na moyo wa ukarimu, kwa kuthubutu kugawana hata ile rasilimali kidogo iliyopo kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Wazazi na walezi anasema Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, wanapaswa kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kupambana fika na changamoto za maisha katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wawajengee utamaduni wa maridhiano na majadiliano ili kuondokana na tabia ya ubinafsi, hali ya vijana kujitafuta wenyewe na matokeo yake ni kuwa na misimamo mikali katika maisha. Kanisa linapenda kuwarithisha vijana wa kizazi kipya, tunu msingi za maisha ya Kikristo, Kiutu na Kijamii; mambo yanayobubujika kutoka kama amana ya imani inyoshuhudiwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Kanisa linapenda kutembea na kushikamana na vijana wa kizazi kipya katika furaha, mahangaiko na matumaini yao halali kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Vijana wanapaswa kuwa na mweleo mpya wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana wa kizazi kipya! Ni matumaini ya Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino kwamba, barua hii itawasaidia vijana kusimama kidete pasi na kukata wala kukatishwa tamaa na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo! Vijana watambue kwamba, wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake! Vijana wa kizazi kipya wajenge na kudumisha moyo wa upendo na mshikamano na “vijana wa zamani” kwa kuweka pamoja tunu za kale na tunu mpya pamoja, kwa ajili ya ujenzi wa familia ya Mungu inayowajibika zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.