2017-12-26 15:33:00

Askofu mkuu Nosiglia: Noeli ni sherehe ya upendo na mshikamano!


Fumbo la Umwilisho ni chemchemi ya furaha, amani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwana wa Mungu aliyezaliwa mjini Bethlehemu ili kuvunjilia mbali nguvu za dhambi na mauti na hatimaye, kumrudishia tena mwanadamu utu na heshima yake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Noeli ni sherehe inayofumbatwa katika umoja, upendo na mshikamano na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na furaha ya ujio wa Mwana wa Baba wa milele.

Hii ni sherehe ya watakatifu na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu; ni furaha ya wazima wanaowajibika kuwatunza na kuwahudumia wagonjwa; ni sherehe ya matajiri wanaopaswa kuonesha huruma, upendo na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha! Ni Sherehe ya waamini wanaopaswa kushuhudia imani yao kwa njia matendo ya huruma na utu wema, ili wale wasio amini waweze kuvtika kwa kuona ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaotolewa na Wakristo katika maisha na utume wao!

Hivi ndivyo alivyosema Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo Kuu la Torino, nchini Italia, wakati wa mahubiri yake kwenye Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2017. Noeli ni Sherehe inayofumbatwa katika wongofu wa ndani, moyo mnyofu na utu wema katika maisha, kwani Neno wa Mungu, Kristo Yesu amejinyenyekeza na kuzaliwa katika hali ya umaskini, changamoto kwa waamini kumtambua katika imani na kumpokea ili aweze kupata nafasi katika sakafu ya mioyo ya waamini. Mwanadamu mamboleo anayo mambo mengi ambayo yanakwamisha fursa ya kumtambua Kristo Yesu katika maisha!

Hii inatokana na changamoto mbali mbali zinazojionesha katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, kazi na jamii katika ujumla wake. Watu wengi wamekengeuka, kiasi cha kuzama na kutopea katika uchu wa mali na madaraka. Hawa ni watu wanaoogopa kupoteza nafasi na utambulisho wao katika jamii kama ilivyokuwa kwa Mfalme Herode, kiongozi katili aliyetaka kumfutilia mbali Mtoto Yesu kwa kudhani kwamba, alitaka kumpora Ufalme wake hapa duniani! Noeli kiwe ni kipindi cha kutoa nafasi ya kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha; utu na heshima ya binadamu; utimilifu wa furaha na amani ya kweli.

Ni wakati wa kujikita katika ukweli na uwazi; uaminifu na udumifu katika mambo msingi; kwa kusamehe na kusahau; kwa kujenga na kudumisha urafiki na udugu; kwa kujadiliana katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Noeli ni kipindi cha mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali zao za maisha, lengo ni kuonesha na kushuhudia uwepo wa Mungu kati ya watu wake! Huyu ndiye Immanueli. Kila mtu anayo thamani, utu na heshima yake, mbele za Mwenyezi Mungu. Ukarimu kwa maskini ni njia ya kumkaribisha Kristo Yesu katika maisha, ili aweze kuwatembelea, kuzungumza na kuonja maisha yao, ili kuwaonesha upendo wake usiokuwa na mipaka! Ni wakati wa kumtengenezea Mwenyezi Mungu nafasi katika maisha, kwa njia ya upendo na mshikamano kwa jirani.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo Kuu la Torino, nchini Italia anawakumbusha vijana kwamba, wao wamesheheni: upendo, furaha na urafiki, lakini wasikae na kubweteka kwa mafanikio waliyokwisha kuyafikia; bali wawe na ujasiri wa kujitoa katika ubinafsi wao; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mambo makubwa zaidi katika maisha kwa kukazia: ukweli, uwazi na uaminifu. Vijana wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo, mshikamano, udugu na umoja, kwa kutambua kwamba, wao ni nguzo na jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa,

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.