2017-12-25 12:19:00

Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya kifo!


Noeli ni Sherehe inayowachangamotisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Kanisa linafundisha kwamba, zawadi ya maisha haina budi kulindwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi pale mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu na wala si vinginevyo! Huu ni ujumbe wa Kardinali Andrew Yeom Soo-yung, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini katika Kipindi cha Noeli kwa mwaka 2017.  

Ujumbe huu unaongozwa na kauli mbiu “Mwenyezi Mungu ameonesha upendo wake kwa binadamu”. Kardinali Andrew Yeom Soo-yung anapenda kuonesha msimamo wa Kanisa ktika kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamduni wa kifo unaoanza kuota mizizi nchini Korea ya Kusini baada ya baadhi ya watu kutaka sheria ya utoaji mimba ifutwe na badala yake, wananchi wawe huru kutoa mimba kadri wanavyotaka. Hapa, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, hawana budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Laudato si” anasema si rahisi sana kusimama kidete kutetea utunzaji bora wa mazingira, ikiwa kama watu wanashindwa kutetea zawadi ya uhai wa mtoto mchanga ambaye yuko tumbaoni mwa mama yake, hata kama uwepo wake unaleta mashaka! Jamii ikipoteza mwelekeo wa kuthamini uhai mpya, itashindwa pia kusimamia mambo msingi katika maisha ya jamii husika. Kardinali Andrew Yeom Soo-yung anapenda kuonesha mshikamano wake wa huruma na mapendo kwa wagonjwa, wazee na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, bila kuwasahau ndugu zake kutoka Korea ya Kaskazini wanaokabiliana na changamoto kubwa za kitaifa na kimataifa!

Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kumwangalia Mtoto Yesu aliyezaliwa katika hali ya unyenyekevu mkubwa, unyonge na umaskini, licha ya kuwa ni Mwana wa Baba wa milele! Hii iwe ni changamoto ya kuangalia jinsi ambavyo jamii inawahudumia na kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali zao za maisha. Kristo Yesu, aonekane kati ya watu hawa, ili kuwa na mwelekeo sahihi wa kuwahudumia “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”.

Kardinali Andrew Yeom Soo-yung katika ujumbe wake wa Noeli anatumia fursa hii kulaani kwa nguvu zote vita, vitendo vya kigaidi na uvunjifu wa haki msingi za binadamu; utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, ubaguzi sanjari na utumwa mamboleo. Hii ni kwa sababu utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi hayapewi kipaumbele cha kutosha na badala yake uchu wa mali, faida na madaraka yanapewa msukumo wa pekee kabisa! Jamii iwe na ujasiri wa kuthamini maisha sanjari na kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wengine. Noeli iwe ni kipindi cha kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Iwe ni fursa ya kuwahudumia na kuwafariji wazee, wagonjwa, watoto yatima na wale wote wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Ni mwaliko wa kuwaonea huruma na kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Jamii ijitahidi kuboresha mazingira ya kazi, ili kweli kazi iwe ni utimilifu wa maisha ya binadamu na wala si kinyume chake. Umefika wakati wa kuachana na vipigo vya wanawake majumbani kwa kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano ndani ya familia, kama Kanisa dogo la nyumbani! Noeli ni kipindi cha kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi! Kardinali Andrew Yeom Soo-yung, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini anahitimisha ujumbe wake wa Noel kwa Mwaka 2017 kwa kuwataka viongozi wa kisiasa kujisadaka kwa ajili ya kutetea utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Uhai ni haki msingi inayofumbata haki nyingine zote, usipolindwa, familia ya binadamu iko hatarini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.