2017-12-24 15:37:00

Papa:Maria ni mnyenyekevu:hatafuti kujionesha pamoja na hadhi aliyopewa!


Katika Dominika inayotangulia sikukukuu ya Noeli, tusikilize Injili ya upashanaji habari (Lk 1,26-38). Katika maelezo ya Injili tunaweza kuona utofauti katika ahadi za Malaika na jibu la Maria. Tofauti hii inajitokeza katika mwelekeo na malengo ya wahusika wawili. Malaika alimwambia Maria; “Usiogope Maria, kwasababu umepata  neema  kwa Mungu. Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto  mwanaume na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana aliye juu, na Bwana Mungu atampatia kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. (tz Lk 1, 30-33) Ni ufunuo mrefu ambao unafungua upeo ambao haujawahi kusikika!

Ni mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko aliyo anza nayo tarehe 24 Desemba 2017, wakati wa sala ya malaika wa Bwana katika viwanja vya Mtakatifu Petro mjini Vatican.  Baba Mtakatifu amendelea na ufafanuzi wa Injili ya Siku, ikiwa tayari ni vijilia ya sikukuu ya Kuzaliwa kwa Bwana kwamba. Baba Mtakatifu anaendelea na ufafanuzi huo kuwa, mtoto atakaye zaliwa na msichana  huyo wa Nazareth ataitwa Mwana wa aliye juu: si rahisi kuwa na utambuzi wa hadhi ya juu zaidi namna hiyo. Na baada ya swali la Maria ambalo anaomba maelezo zaidi, ufunuo wa Malaika unakuwa wazi zaidi  na kushangaza .

Badala yake, jibu la Maria ni sentensi fupi, ambayo haikuzungumza juu ya utukufu au fursa aliyopata, bali uwezekano na huduma kwamba “tazama mimi mjakazi wa Bwana; na niwe kwangu kama ulivyo sema”. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anathibitisha kwamba inaonesha hata lengo pia ni tofauti. Maria hakujiinua mbele ya mtazamo wa kuwa jinsi hiyo, yaani kuwa  mama wa Masiha, badala yake  anaendelea kuwa wa kawaida  na kujieleza  kwa kuzingatia mpango wa Bwana.

Utofauti huo una maana yake anathibitisha!  Baba Mtakatifu anaongeza, unatufanya tutambue kwamba, Maria kweli ni mnyenyekevu na hatafuti kujiweka katika maonesho. Anatambua udogo wake mbele ya Mungu na anafurahi kwa jinsi alivyo. Wakati huohuo anao utambuzi kwamba, ni  kutokana na jibu lake la ndiyo kufanya ukamilifu wa mpango wa Mungu ambao ameitwa kuitikia yeye binafsi.

Katika hali hii, Maria anajionyesha kwa mtazamo unaokwenda sambamba na ule wa Mwana wa Mungu anayekuja katika  ulimwenguni: Yeye anataka kuwa Mtumishi wa Bwana, kujikita katika huduma ya binadamu ili aweze kukamilisha mpango wa Baba,kwa maana hiyo, Maria anasema: “Tazama mimi mjakazi wa Bwana; vile vile hata na Mwana wa Mungu, wakati wa kuingia katika dunia anasema: “Tazama nimekuja (…) kuyafanya ee Mungu mapenzi yako” ( Eb 10,7.9). Hiyo ni kuonesha wazi kwamba, mtazamo wa Maria unaonesha kikamilifu tamko hili la Mwana wa Mungu, ambaye pia anakuwa mwana wa Maria.

Na kwa njia hiyo Maria anatoa ufunuo wa kushiriki kikamilifu mpango wa Mungu na, kuonesha hata kama mtume wa Mwanae, hasa katika wimbo wa sifa anaimba kwamba “amewashusha wenye nguvu kutoka katika viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu (Lk 1,52); hilo ndilo jibu lake la unyenyenyekevu na ukarimu ambao aliupata kutoka katika utukufu wa aliye juu. Baba Mtakatifu amemalizia akisema kuwa, tukiwa tunashangazwa na Mama yetu kwa jibu lake  la “tazama mimi hapa” na utume wa Mungu, tumuombe atusaidie kila mmoja wetu kupokea mpango wa Mungu katika maisha yetu, kwa unyenyekevu wa kweli na ukarimu wa ujasiri , furaha ya juu na hata utukufu.

Mara baada ya tafakari ya Injili ya siku, kwa mahujaji wote walio udhuria sala ya Malaika wa Bwana katika viwanja vya Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko, amesema, tukiwa katika kusubiri kwa maombi na sala siku ya  Kuzaliwa kwa Mfalme wa Amani, tumuombe zawadi ya amani kwa ajili ya dunia nzima hasa kwa watu wanaoteseka zaidi kutokana na migogoro inayoendelea. 

Anatoa wito kwa mara nyingine tena ili kwamba fursa ya Sikukuu Takatifu ya Noeli, watu wanaotekwa nyara, kama vile, mapadre, watawa na waamini walei wengi waweze kuachiwa huru na kurudi katika makazi yao. Aidha amependelea kuonesha ukaribu wa sala na maombi  kwa watu wa Kisiwa wa Mindanao nchini Ufilippini waliokumbwa na kimbunga na kusababisha waathitrika wengi na uharibifu mkubwa. Mungu wa huruma apokee roho za marehemu, na kuwapa nguvu wote wanaoteseka katika janga hilo.

Amewasalimia watu wote, waamini kutoka Roma, mahujaji waliotoka nchi mbalimbali, familia makundi ya parokia na vyama mbalimbali. Anaongeza kusema kuwa, katika masaa haya yaliyobaku  ya kujiandaa na Noeli, watu wote wapate muda wa kukaa kimya kwa sala mbele ya pango, ili kuabudu katika moyo wa fumbo la Noeli ya kweli ambayo ni Yesu anayekaribia kwetu kwa upendo, unyenyekevu na huruma. Na kwa muda huo wanaposali, basi iwe pia fursa ya kutmsahabu Baba Mtakatifu katika maombi hayo. Amewatakia  Jumapili njema, mlo mwema wa mchana  na Sikukuu njema ya Kuzaliwa kwa Bwana.

Sr Angela Rwezaula
Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.