2017-12-21 13:54:00

Ujumbe wa Noeli kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza!


Simameni kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu; amani ya kweli inapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu; uhuru katika Kristo unaojikita katika upendo dhabiti unaofumbatwa katika amani, mshikamano na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Dini zinapaswa kuwa ni vyombo vya amani na maridhiano kati ya watu; mambo yanayodumishwa katika majadiliano ya kidini ili kujenga hali ya kuaminiana, tayari kujikita katika mshikamano na ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kushirikiana rasilimali za dunia!

Haya ni kati mambo msingi yaliyomo kwenye Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2017 kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli! Anasema, Mwaka 2018, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu lilipochapishwa! Lakini hata leo hii, bado kuna uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kutishia utu na heshima ya binadamu. Vita, kinzani, uchu wa mali na madaraka pamoja na unyonyaji ni mambo ambayo yanahatarisha haki msingi za binadamu.

Katika maendeleo makubwa ya sayansi, teknolojia pamoja na uchumi, yamechangia kukuza kiu ya haki jamii na amani miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, unaendelea kuhatarisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu. Mama Kanisa hawezi kukaa kitako na kufumbia macho changamoto hizi mamboleo dhidi ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa litaendelea kusimama kidete kupambana dhidi ya mambo yote yanayonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu; kwa kujikita katika kudumisha uhuru na amani kwa kutambua kwamba, amani ya kweli inabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, ndani ya Kanisa, waamini wanaonja uhuru unaopata chimbuko lake kwa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha uhuru na upendo wa kweli kwa jirani. Ukweli huu ndio msingi wa ustawi na maendeleo ya binadamu kwa siku za usoni! Kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema, waamini wanaweza kupambana na changamoto mamboleo zinazotishia ustawi, maendeleo na maisha ya binadamu! Dini mbali mbali duniani zinao wajibu wa kukuza na kudumisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, utamaduni wa mshikamano; majadiliano na amani.

Huu ni mchango mkubwa sana unaoweza kutolewa na dini mbali mbali duniani kutokana na nguvu yake ya maisha ya kiroho. Hii ni nguvu inayoweza kudumisha misingi ya amani, mshikamano kwa kutoa maana halisi ya hatima ya maisha ya binadamu, yaani uzima wa milele; kwa kudumisha umoja katika utofauti! Hii ni changamoto ya kukataa katu katu misimamo mikali ya kidini na kiimani, inayokwenda kinyume na misingi ya kidini. Hii inatokana na ukweli kwamba, dini kimsingi ni chombo cha amani, changamoto na mwaliko kwa waamini wa dini mbali mbali kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, ili kudumisha utamaduni wa amani na maridhiano kati ya watu! Dini ziwe ni vyombo na mashuhuda wa mshikamano na daraja la: amani, maridhiano pamoja na maelewano ili kusaidia kukuza utamaduni wa mshikamano na hali ya kuaminiana!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kufafanua kwamba, majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani yanawawezesha kuimarisha imani, mahusiano na mafungamano yao na jirani zao. Huu ni mchakato unaopania kuganga na kuponya maamuzi mbele, ili kudumisha maelewano, daima kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto, kinzani na matatizo yanayojitokeza kwa njia ya amani na hivyo kuondokana na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko, ili kujenga hali ya kuamianiana na kuthaminiana. Dini mbali mbali duniani zinapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kulinda na kudumisha uhuru, utu na heshhima ya binadamu; mambo muhimu katika kukuza amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kukabiliana na changamoto mamboleo kwa njia ya mshikamano katika medani mbali mbali za maisha!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anahitimisha Ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2017 kwa kusema ni jambo la kufikirika kudhani kwamba, utandawazi na mshikamano vinaweza kujengwa kwa njia ya: maendeleo ya kiuchumi, mitandao ya mawasiliano pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ikumbukwe kwamba, binadamu wanategemeana na kukamilishana; wanapaswa kuunganisha nguvu zao ili kujenga mshikamano, majadiliano, ushirikiano pamoja na hali ya kuthaminiana; kwani, hii ni safari ya maisha kwa watu wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.