2017-12-21 15:43:00

Kardinali Bernard Law asindikizwa kwenye usingizi wa amani!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko na majonzi makuu taarifa za kifo cha Kardinali Bernard Law, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Boston, Marekani, na Mhudumu mkuu wa Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu, lililojo mjini Roma, aliyefariki dunia Jumatano tarehe 20 Desemba 2017 mjini Roma akiwa na umri wa miaka 86 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Baba Mtakatifu katika salam za rambi rambi alizomtumia Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, anasema, anapenda kuungana na Makardinali wote, kutoa sala kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, ili aweze kumpokea Mtumishi wake Kardinali Bernard Law katika usingizi wa amani. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kutoa baraka zake za kitume kwa wale wote walioguswa na kutikiswa sana na msiba huu mzito.

Baba Mtakatifu anapenda kumweka Marehemu Kardinali Bernard Law chini ya maombezi, ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Waroma! Kardinali Angelo Sodano ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akaongoza Ibada ya Mazishi ya Kardinali Bernard Law yaliyofanyika Alhamisi, tarehe 21 Desemba 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.