2017-12-14 16:41:00

Papa:Mungu anatumia sauti kama ya mtoto kubembeleza mwanae!


Huruma ya Mungu ndiyo imekuwa kitovu cha mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko, siku ya Alhamis 14 Desemba 2017 katika Kikanisa cha Mtakatifu Marta mjini Vatican. Mada ya siku imetolewa  katika kitabu cha Nabii Isaya  na  zaburi  isemayo  Bwana ni mwema kwa watu wote na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.  Baba Mtakatifu akifafanua zaidi amesema, sura na sauti  ya nabii Isaya inavyojieleza , ni kama ile ya Mungu akimwelekea mtoto, ambapo anabadili  sauti yake ya ukubwa  iweze kufafana kama ya mtoto. Na kwa maana hiyo,  sauti inamtuliza na kumwakikishia asiogope, kwa maana anakuja kumsaidia.

Hiyo pia ni kuonesha kama vile sauti ya Mungu inataka kuimba wimbo mzuri  wakati mtoto anapokuwa anataka kulala usingizi usiku.  Mungu wetu anao uwezo wa kufanya hivyo Baba Mtakatifu anathibitisha! Ukarimu wake ni wa namna hiyo yaani kama wa  Baba na mama. Mara nyingi yeye amesema, hata kama ni mama anasahau mtoto wake, yeye hatasahau kamwe! Yeye anatuchukua katika umbu lake. Mungu anazungumza kwa namna hiyo ya udogo ili tuweze kutambua, kuwa na imani naye na tunaweza kuwa na ujasiri kama wa Mtakatifu Paulo anaye badili maneno  na kumwita Abba…badala ya Baba,  maana hiyo ndiyo huruma ya Mungu.

Ni mkubwa anayejifanya mdogo na mdogo ambaye ni mkubwa, kwani hakika, Baba Mtakatifu anasema, mara nyingi  ni kama Mungu anatupiga kiboko. Yeye ni mkubwa lakini huruma yake inatukaribia na kutukomboa. Hilo ni fumbo na moja ya mambo mazuri!  Ni Mungu mkubwa anayejifanya mdogo na udogo wake auishi kuendeleza ukubwa wake. Na ndiyo lugha ya ukubwa katika udogo: kwa maana ya uwepo wa huruma ya Mungu. Mkubwa anajifanya mdogo na mdogo ndiye mkubwa.

 Tunasaidiwa kulitambua hili wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwa Bwana. Kwa maana ya  kutazama  holini ndipo unamwona Mungu katika udogo.  Baba Mtakatifu amekumbusha maneno ya Mtakatifu Tomas  katika maandishi yake akitafakari na kuelezea suala hili kwamba: “Mungu ni nini, ni kitu gani cha kimungu? Jibu lake  anasema, (Non coerceri a maximo  contineri tamen a minimo divinum est) Usiogope mambo makuu, lakini uzingatie mambo madogo. Hayo ndiyo Mungu na wote wawili  pamoja.

Je ni mahali gani Mungu anaonesha huruma yake? Katika kujibu Baba Mtakatifu anafafanua kuwa: Ni Mungu peke yake anatusaidia likini pia anatoa ahadi za furaha wakati wa kumtafakari na kutusaidia kwenda mbele ,kwa sababu ni baba.  Mungu anajionesha katika madonda na majeraha yangu na hata majera ya jirani, kwa maana yeye mwenye anasema, ”katika majeraha yangu wote mmeponywa”.

Kwa kusisiztia juu ya hilo, anakumbusha Injili ya Msamaria, kwa maana amethibitisha kuwa yupo mtu aliyenama kumsaidia  huyo aliye vamiwa na kujeruhiwa na majambazi.  Alimsaidia na kulipa kile kilichotakiwa . Na kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anaonesha kuwa, ndiyo eneo la taalimungu  ya huruma ya Mungu : majeraha yetu. Na hivyo amemaliza kwa ushauri wa kujikita kwa ndani zaidi  tafakari ili  kuona majeraha yetu ya ndani kwa kufanya hivyo ndipo  Bwana aweze kuyaponyesha.

Sr Angela Rwezaula 
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.