2017-12-13 15:43:00

Jumuiya ya Mt.Egidio:Ongeza kiti mezani siku ya Kuzaliwa kwa Bwana!


Kusheherekea Krismasi na maskini, wasiokuwa na makazi, familia zenye shida na wazee, ni dhamira ya  Jumuiya ya Mt. Egidio kuandaa chakula cha mchana tarehe 25 Desemba 2017. Hili ni lengo la kampeni ya kukusanya fedha  yenye kauli mbiu " Ongeza kiti mezani siku ya Krismasi " iliyozinduliwa na Jumuiya ya Mt. Egidio na ambayo kila mtu anaweza kuchangia kwa ujumbe mfupi au simu kwenda namba 45568 kuanzia tarehe 10 hadi 25 Disemba.

Naye Bwana Marco Impagliazzo mwenyekiti wa Jumuiya ya Mt. Egidio akiwasilisha Mjini Roma Kampeni ya pamoja na mwongozo wa "wapi pa akula, kulala na wapi pa kunawa" amesema,  zote hizo ni nyuso zinazojulikana. Kwa maana wote hao ni marafiki na wanawasaidia mwaka mzima. Na chakula cha mchana cha Krismasi sio maonesho bali ni sherehe ya familia,shughuli iliyoanza tangu mwaka 1982 katika madhabahu ya Mt. Maria Trastevere mjini Roma. Leo hii bado inaendelea katika sehemu nyingi za mji wa Roma,kama vile katika taasisi nyingi za wazee na magereza,kama ilivyo  hata Gereza kuu la  Regina Coeli na katika miji mingine ya Italia na ulimwenguni.

Historia hii sasa imepita miaka 35 tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu wa chakula cha mchana cha Noeli ambapo tangu wakati huo, meza ya Krismasi imeongezeka zaidi. Mwaka 2016, Jumuiya ya Mt. Egidio iliweza kuwaalika watu zaidi ya elfu 50 wenye shida nchini Italia ili kuweza kushiriki chakula cha mchana cha Noeli na karibu watu 200,000 duniani.

Aidha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio amefafanua kuwa Mwaka huu 2017 matarajio yao kwa  chini ya Italia ni kuwahudumia watu 60,000. Na thamani ya mchango itakuwa ni Euro 2 kwa kila SMS itakayotumwa kwenye makampuni ya simu za mkononi kama vile: Wind, Tre, Tim, Vodafone, PosteMobile, Coop Voce na Tiscali. Euro 5 kwa kila simu itakayopigwa kutoka kwa mtandao wa landline, Vodafone,Twt, Convergenze; euro 2 kwa PosteMobile, na euro 2 na euro 5 kwa kila simu itakayopigwa  kwenda namba 45568 kutoka kwenye mitandao ya Tim, Wind, Tre, Fastweb na Tiscali.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.