2017-12-09 10:57:00

Itengenezeni njia ya Bwana,yanyosheni mapito yake,Bwana anakuja!


Habari ya Yohane Mbatizaji ni simulizi mahususi wakati wa kipindi cha Majilio. Dominika ya Pili ya Majilio hujikita katika kuuelezea Unabii wake. Yeye anajitambulisha kama “Sauti ya mtu aliaye nyikani”. Anaelezewa kama mtangulizi wa Bwana na ambaye anamtambulisha Kristo katika jamii ya watu. Katika masimulizi ya Injili Yohane anaelezewa kuwa na unasaba na Kristo kwani mama yake Yohane Elizabeti alikuwa ni shangazi ya Bikira Maria, Mama yake Kristo (Lk 1:36). Pamoja na undugu huu, masimulizi ya Injili hayaoneshi unasaba uliokuwa juu yao wakati wa utume wao. Yohane Mbatizaji anatambulishwa kama mtangulizi na anayemwandalia Kristo njia. Aliutambua ukuu wake ndiyo maana hata wakati wa ubatizo wake alisita kumbatiza Kristo. Huyu ndiye Yohane Mbatizani ambaye ni sauti iliayo nyikani akisema: “itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake”. Hii ndiyo dhamira ya Dominika ya pili ya Majilio, yaani kufanya toba na kumwandalia Mungu mahali ili akae nafsini mwetu.

Taifa la Israeli liliteuliwa na Mungu na kutendewa fadhili mbalimbali. Kinyume chake na kwa mtindo wa shukrani ya Punda walimuasi Mungu. Matokeo yake walipelekwa utumwani Babeli kwa kipindi cha miaka 40. Hali ya utumwa katika ujumla inaondoa uhuru wa mtu. Aliyepo utumwani huwa katika hali ya wasiwasi na hajui kesho yake itakuwa vipi. Matarajio yake yote yapo chini ya Bwana wake. Ndivyo walivyokuwa wana wa Israeli kule Babeli. Walikosa hata ladha ya kumtukuza Mungu kama Mzaburi anavyowaelezea wakilalamika huku wakisema: “Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni? (Zab 137:4). Ndiyo katika muktadha huu inawafikia sauti ya faraja tunayoisikia katika Somo la kwanza ikisema: “Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu, kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa”.

Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inatufunulia ukuu na upana wa huruma ya Mungu. Yeye hatusahau milele hata kama tunamkosea na kuasi. Hii ni kwa sababu upendo wake mkuu wadumu milele. Kama ilivyokuwa kwa Waisraeli sisi nasi tunaingia utumwani kwa dhambi zetu. Dhambi inatufanya tushindwe kuuona upendo wa Mungu na kukumbatia mambo ya ulimwengu. Katika mazingira ya kuasi tunafurahia na kuona mkono wa mwanadamu una nguvu na wenye kuleta matumaini lakini mwisho wake hutuingiza katika maisha ya hofu na kuchanganyikiwa. Tunajaa vihoro na kukosa furaha nafsini mwetu. Lakini Mungu wetu ni mwema sana kwetu na huruma yake ni ya milele. Kila wakati anatupatia nafasi ya kuanza tena na kujishikamanisha naye.

Furaha ya majira haya ya Majilio ipo katika kujiandaa kwa ujio huu wa pili wa Bwana. Ni furaha kwa sababu tunakifahamu tulichopoteza kwa kumuasi Mungu na hivyo tunapoahidiwa kurudishiwa tena hiyo tunu yake bila shaka furaha inakuwa kubwa sana. Kelele na furaha za kidunia zinaonekana mbele yetu kama takataka kwani zilipotuondoa katika reli tuliingia katika mahangaiko na mateso mengi. Ndiyo maana Nabii Isaya anaendelea kuwaeleza wana wa Israeli akisema: “Itengenezeni nyikani njia ya Bwana, nyosheni jangwani njia kuu ya Mungu wetu”. Hapa inatumika taswira ya nyika na jangwa ili kuonesha ni jinsi gani katika  hali ya dhambi roho zetu zinapoteza hadhi yake. Nyika na jangwa ni ishara ya kukosekana kwa rutuba na mvua. Ndivyo alivyo yeye aliye katika hali ya uasi. Hivyo wito unaotujia katika Dominika hii ya pili ya Majilio ni kutengeneza njia yaani kufanya maandalizi katika nyika hizo na majwangwa hayo ili Bwana aweze kupita.

Katika dhambi zetu tumekuwa na mabonde mengi, yaani upunguvu wa neema na misaada ya kimungu. Tunashindwa kujitajirisha kwa matendo ya sala, sakramenti na tafakari ya Neno la Mungu. Tunamuondoa Mungu nafsini mwetu na matokeo yake ni kusikia utupu na shimo kubwa ndani ya nafsi. Mabonde haya yanapaswa kuinuliwa. Tulijitengenezea vilima kwa kiburi chetu na kujiinua basi tunaambiwa leo tukisawazishe kilima hicho. Kuondoa kiburi cha pesa, mali na madaraka ambavyo vinaathiri urafiki wetu na Mungu na urafiki wetu na wenzetu. Wakati mwingine tumepindishapindisha mambo kwa kuukwepa ukweli na hapa tunaalikwa kunyoosha mambo na kutenda kadiri ya makusudi ya Mungu kwetu. Tunajaribu kuufanya ukweli urandane na matamanio yetu ya kidunia. Na mwisho tumekwangua kwangua haiba njema tuliyopewa na Mungu na kujiivika hadhi zisizoendana nasi, napo pia tunaalikwa kulainisha na na kuutunza uzuri wetu wa asili. Hayo ndiyo maandalizi ambayo tunaambiwa kuyafanya ili Bwana ajapo tena kwa mara ya pili aweze kupita katika njia nzuri.

Sauti hii ya mtu aliaye nyikani inaonekana katika nafsi ya Yohane Mbatizaji kama inavyosimuliwa katika Injili ya Dominika hii. Yeye ambaye alikuwa mtangulizi wa Masiha aliwaalika watu wa wakati wake kufanya toba ili kumtayarishia Bwana njia stahiki. “Yohane alitokea, akabatiza nyikani, na kuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo ya dhambi.” Hapa tunaona muunganiko wa jukumu hilo la kumwandalia njia Bwana na toba kwani “walimwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto Yordani, wakiziungama dhambi zao. Njia tunayoalikwa ni kunyoosha matendo yetu na kurudia katika mstari ulionyooka. Wana wa Israeli walipokuwa wanapewa ujumbe wa furaha waliambatanishiwa na kufanya tendo hilo la kufanya toba yaani kuyaacha matendo yao yaliyowasababishia utumwa.

Yohane alijitambulisha kama sauti iliayo nyikani. Alipohubiri alisema “yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake”. Katika hili tunapata tafakari nyingine muhimu katika maandalizi wetu ya kipindi hiki. Maandalizi yetu si kujitengenezea njia sisi bali kuifanya nafsi yetu njia ya kupita huyo ajaye, ambaye ni mkuu kuliko sisi. Tunapomwandalia njia hiyo kunakuwa na mambo mawili. Kwanza anakaa ndani mwetu na kutupatia faraja na pili kupitia sisi anawafikia watu wengine. Kumbe maandalizi yetu haya yanabeba pia taswira ya kimisionari, yaani tunamfanyia njia Kristo ili atutumie kama nyenzo ya kuwafikia wengine. Yote hata yanawezeshwa na unyenyekevu na kuitambua nafasi na ukuu wa Maisha. Yohane Mbatizaji alilionesha hili kwa vitendo aliposema: “Basi hii ni furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua” (Yoh 3:30).

Mtume Petro anatuhakikishia kwamba Bwana atakuja tena: “Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi… lakini kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya ambayo haki yakaa ndani yake. Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake”. Himizo hili la kitume ni kwetu tulio na imani katika Kristo kuikumbuka ahadi ya Bwana kwamba atarudi tena na hivyo kujiandaa vema, yaani kuifanya njia yake iwe nzuri na yenye kupitika. Maandilizi yetu yanapaswa kuwa ya wakati wote kwani Yeye anakuja kama mwivi; hatujui siku wala saa ambayo atakuja. Maandalizi yetu ya ujio wake wa pili yanakuwa kwetu ni maandalizi ya maisha yetu yote kwa kuzipamba roho zetu na matendo mema na yenye kumpendeza Mungu.

Na Padre Joseph Peter Mosha.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.