2017-11-17 16:58:00

Tuipande ardhini tunu ya imani ili ichipue,ikue na kuzaa matunda mema


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican! Leo Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya kwanza ya maskini duniani. Hili ni zao la Jubilei ya Huruma ya Mungu ambalo linabeba ujumbe mahususi wenye kichwa cha habari: “Tupende si kwa maneno bali kwa matendo”. Huu ni Ujumbe ambao unatutaka kutekeleza kwa matendo upendo wetu. Ni Ujumbe ambao unamwalika kila mwanadamu kusikia kweli kilio cha maskini, kunyoosha mkono wake kwa ujasiri na kumuhudumia kwa upendo. Tunapoitafakari siku hii adhimu ambayo kwayo mwanadamu anarejeshewa hadhi yake Neno la Mungu katika Masomo ya Dominika hii yanatualikwa kuistawisha mbegu ya imani iliyopandwa ndani mwetu na matunda hayo yawe ni manufaa kwa watu wote. Tunapotenda kweli kwa matendo kwa hakika tuzaa matunda mema.

Mwanataalimungu Jules Mimmeault kutoka Chuo cha Kipapa kilichojikita katika taalimungu maadili cha Accademia Alfonsiana anauelezea upendo wa mama kama “asymmetrical love”. Hii humaanisha kwamba upendo wa mama ni upendo usio na uwiano au usawa. Mama amejaliwa tabia maalum sana ambayo humfanya kujitoa na kuifikiria familia yake bila kujibakisha wala kutegemea kulipwa na hao anaowapenda. Upendo huu ni upendo unaohitaji sadaka kubwa sana na humithilishwa na upendo wa Mungu. Tunu ya umama hupata maana pale iponakubali kuwekwa ardhini kama mbegu kusudi izae matunda mema. Zawadi ya imani tuliyoipokea wakati wa ubatizo wetu ni mithili ya tunu hii ya umama ambayo inapaswa kukua na kuzaa matunda mema.

Leo tunaalikwa kutafakari juu ya tunu hiyo ya kujitoa bila kujibakiza au kutegemea malipo. Msimulizi wa kitabu cha mithali anamwelezea huyu mama kama “mke mwema”. Anaanza kwa kumtaja kwamba “hutenda mema wala si mabaya, siku zote za maisha yake”. Hii ni sifa muhimu ambayo imefichika ndani ya mama. Mama anasifika kwa kunuia mema kwa ajili ya familia yake. Mwandishi anaendelea kumwonesha mama kama mchapa kazi hodari kwani daima “hutia mikono yake katika kusokota”. Sifa ya ya tatu ni ukarimu. Mama anaelezewa kama yule ambaye “huwakunjulia maskini mikono yake; naam, huwanyooshea wahitaji mikono yake”. Ndani ya familia ya mwanadamu mama ndiye anaonekana zaidi kuwatia nguvu walio dhaifu na kuhakikisha wote wanapata haki zao.

Sifa zote hizi zinawezekana pale mama atakapokuwa tayari kuifanyia kazi karama yake aliyopewa kwa ajili ya familia inayomtegemea. Kinyume chake kinaonekana kwa mwanamke anayeonekana kujijali mwenyewe kwa uzuri wake. Mwandishi anatuambia kwamba “upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili”. Mama anayetumia muda wake wote kujipamba au kuupambanua uzuri wake huyu hakika anajitafuta mwenyewe. Ni aghalabu kwake huyu kuitambua tunu iliyofichika ndani mwake na kuifanyia kazi kwa ajili ya manufaa ya wanafamilia wake. Ataweza vipi kuonesha upendo kwa watoto wake kwa kuwahudumia mfano kuwapikia na kuwaogesha wakati muda wote anahangaikia uzuri wake? Ataweza vipi kuwa furaha kwa mumewe kwa huduma nzuri za kimama ili hali muda wote anahangaikia urembo wake?

Katika Injili ya leo Kristo anaonesha mfano huo wa kuifanyia kazi talanta tuliyopewa mithili ya taswira ya kimama katika namna zote mbili. Kwanza anatuwekea mbele yetu mfano wa watu wawili ambao wanaifanyia kazi talanta waliyopewa na matokeo yake inazaa matunda. “Yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida”. Hapa tunafundishwa upendo huo wa kimama ambao hauna uwiano lakini daima unazaa matunda. Ni mithili ya mshumaa ambao unakubali kuteketea lakini faida yake inaonekana kwa kutoa nuru na kuwaangazia wengine.

Mfano wa pili ni wa yule aliyepewa talanta moja. Yeye aliifukia chini na asiifanyie kazi na alipohojiwa na Bwana wake alimjibu hivi: “nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya”. Huu ni mfano dhahiri wa upendo wa “nipe nikupe” na unakinzana na upendo wa kimama. Aina hii ya upendo haitoi fursa kwa mmoja kujitoa bali unaangalia faida binafsi. Wengi wanaogubikwa na upendo huu uipokea talanta wapewayo na mwenyezi Mungu na kuifukia na hivyo kutozaa matunda. Hawa ni wale Wakristo wa jina tu ambao hujitangaza kuwa ni Wakristo lakini hawapo tayari kutumikia mithili ya upendo wa Kristo ambao unafunuliwa na upendo wa kimama. Ni wale ambao wanaangalia kile watakachopata ndipo wanajitoa kutumikia.

Haya tunaweza kuyashuhudia katika jamii inayopoteza hamu ya kujisadaka kwa ajili jamii nzima. Unapoomba watu kutoa huduma fulani swali litakalokuja katika nafasi ya kwanza ni kwamba “mimi nitapata nini?” Watu wanakuwa wazito kuonesha vipaji vyao kwani hawaoni faida ya vitu vinavyoshikika. Wengi wanasahau kwamba kila mmoja anapoitendea haki talanta yake wote katika umoja wanapokea zaidi ya walicho nacho. Katika jamii ya Wapare nchini Tanzania zipo kazi za kujitolea zinazoitwa “msaragambo”. Kazi hizi huweza kuwa ni kutengeneza barabara kwa ajili ya kijiji au kushirikiana katika shughuli ya mazishi au shughuli nyingine. Ushiriki wa mmoja katika “msaragambo” hakumpatii ujira lakini kunatoa fursa ya kusafiri vizuri au kufanya matanga ya ndugu yako upatapwo na msiba bila kuwa na mzigo mzito.

Kipaji chako ambacho ni talanta yako uliyopewa si chako binafsi. Umepewa kusudi uende ukawatumikie wengine. Mwalimu anaudhihirisha ualimu wake kwa ufundishaji na malezi yake bora shuleni. Hali kadhalika Daktari anatambulika kwa huduma zake kwa wagonjwa. Hakuna hata mmoja hapo juu ambaye amepokea kipaji alichonacho kwa ajili ya kujinufaisha yeye mwenyewe. Tunapoanza kuweka mbele maslahi yetu badala ya huduma tarajiwa kadiri ya talanta tuliyokirimiwa tunapoteza hadhi yetu na tunauharibu ubinadamu. Tunaweza kuona ubinadamu unateseka kwa sababu mimi na wewe tumeacha kujipambanua kwa kuzifanyia kazi talanta zetu kwa faida ya wote bali tumetumia nafasi zetu kama mtaji wa kujinufaisha na kujineemesha sisi binafsi.

Ndiyo maana changamoto nyingi katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinaonekana katika juhudi ya wahusika kujilimbikizia na kujineemesha wao binafsi. Mfano wa Injili unatukumbusha wajibu wetu kama Wakristo. Anayetupatia talanta hizo ni Mungu. Hivi ni vipaji mbalimbali anavyotoa kwa watu tofauti ili kila mmoja katika haiba ya kimama azae matunda kwa faida ya wote. Mwisho wa maisha yetu tutaulizwa juu ya talanta hizi na nini tulichonacho kama faida. Hii ina maana kwamba tunu ya imani tuliyoipokea inapaswa kukua na kuzaa matunda. Mtume Paulo anatuonya katika somo la pili kwamba ujio huo wa Bwana haujulikani “maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku…basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe na kuwa na kiasi”.

Zawadi ya ukristo inatupatia fursa ya kujitajirisha daima na kuiweka hai imani yetu. Tujishughulishe kwa kutenda mema kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ni wito kwetu kutosombwa na upepo wa kidunia. Tumepewa mfano mwema wa mama katika familia hivyo tujifunze fadhila za kimama na hatimaye tuweze kujitoa bila kujibakiza kwa kuzipanda talanta zetu ili zikue na kuzaa matunda mema. Tukumbuke kwamba imani yetu si imani mfu bali ni imani iliyo hai. Ahadi yetu ya upendo kwa Mungu na jirani ionekane katika matendo na si kwa maneno. Leo tunapoadhimisha siku ya maskini duniani tunaalikwa kwa kuambiwa: “Tupende kwa matendo wala si kwa maneno”.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.