2017-10-19 14:52:00

Washirikisheni wengine wokovu wa Mungu kwa njia ya matendo ya huruma


Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake kumbu kumbu ya kutambua kwamba, wokovu ni zawadi inayotolewa bure kabisa kwa watu wote, lakini binadamu anapaswa kuishughulikia. Mwenyezi Mungu anapenda kuwa karibu zaidi na watu wake na kwamba, uwepo huu unapaswa kushuhuda unaomwilishwa katika matendo ya huruma ya kiroho na kimwili! Kwa njia hii, waamini wataweza kujifungulia lango la uzima wa milele na kuwawezesha wengine pia kupitia katika lango hili na wala si kuwa kizingiti kama ambavyo inafafanuliwa kwenye Liturujia ya Neno la Mungu, Lk. 11:47- 54 na Rom. 3: 21- 30, Alhamisi, tarehe 19 Oktoba 2017.

Yesu anawashutumu Mafarisayo na Walimu wa sheria kwa mauaji ya Manabii na kwa kuuondoa ufunguo wa maarifa, kiasi cha kushindwa kufahamu Ufunuo wa Mungu katika historia ya maisha ya watu wake na badala yake wanajidai kuwa ni wenye haki mbele ya Mungu na kusahau kwamba, Mungu peke yake ndiye mwenye haki. Wamesahau yale yanayofumbatwa katika moyo wa Mungu na mpango wake katika historia nzima ya wokovu ambao ni zawadi ya bure kwa watu wote, inayoshuhudia ukaribu na huruma ya Mungu kwa waja wake! Wao wametokomea na ufunguo wa maarifa.  Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 19 Oktoba 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Wao wamejikita katika Sheria ambayo wameiongezeka na kuinyambulisha kiasi hata cha kushindikana kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mafarisayo na Walimu wa sheria wanamtambua Mungu ambaye ametunga Sheria na wala si Mwenyezi Mungu ambaye amejifunua katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, tangu wakati wa Abrahamu hadi utimilifu wake kwa Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele. Historia nzima ya wokovu inayonesha ukaribu na uwepo wa Mwenyezi Mungu katika safari ya ukombozi wa watu wake.

Pale watu wanaposhindwa kutambua uwepo wa Mungu kati ya watu wake na kuweka kando maisha ya sala, hapo hata ufafanuzi wa Mafundisho msingi yanakosa mashiko! Taalimungu maadili inafumbatwa katika sala, ili kuwa karibu na Mwenyezi Mungu ambaye amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa Mungu. Haki ya Mungu anasema Baba Mtakatifu imedhihirika pasi na sheria, inashuhudiwa na Torati na Manabii; hii ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Kristo Yesu kwa wale wote wanao mwamini. Yesu ni chombo cha upatanisho kwa njia ya imani katka Damu yake Azizi, ili aoneshe haki yake.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni kielelezo cha imani tendaji na utimilifu wa Sheria. Kwa njia hii, waamini wanamhudumia Kristo mteswa: kiroho na kimwili kwa njia ya matendo ya huruma kwa jirani zao. Kuna baadhi ya viongozi wa Kanisa wamepewa ufunguo wa maarifa, lakini bado wanaendelea kuwa ni kizingiti kwa waamini wanaotaka kumwendea Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kuwasindikiza viongozi wao wa dini kwa sala na majitoleo, ili kamwe wasipoteze ufunguo wa maarifa, kwa kujifungia mlango na kutowaruhusu wengine kuingia kwa kupitia lango hili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.