2017-10-19 16:17:00

TANZIA: Kardinali Ricardo Vidal kutoka Ufilippini amefariki dunia


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa za kifo cha Kardinali Ricardo Vidal, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Cebu nchini Ufilippini kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 2010, aliyefariki dunia, tarehe 18 Oktoba 2017, akiwa na umri wa miaka 86. Kwa miaka kadhaa alikuwa pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini. Katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Jose S. Palma, wa Jimbo kuu la Cebu, Baba Mtakatifu anapenda kutuma salam zake za rambi rambi kwa familia yote ya Mungu Jimboni humo.

Baba Mtakatifu anaungana na wale wote walioguswa na kutikishwa na msiba huu mzito wa Kardinali Vidal, kiongozi aliyejisadaka bila kuchoka kwa ajili ya kukuza na kudumisha majadiliano na Injili ya amani nchini Ufilippini. Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu Kardinali Vidal, raha ya milele na mwanga wa milele uweze kumwangaza na hatimaye, apumzike kwa amani!

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali Vidal alizaliwa kunako tarehe 6 Februari 1931, Jimbo Katoliki la Lucena kwa wakati huo. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa  Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 17 Machi 1956. Baada ya Upadrisho wake, alipewa dhamana ya kuwa mlezi seminarini hadi mwaka 1971. Kunako mwaka 1971 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo Katoliki Malolos, Bulacan. Mwaka 1973 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu Lipa huko Batangas.

Tarehe 13 Aprili 1981 aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Cebu na kusimikwa tarehe 24 Agosti 1982. Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali kunako mwaka 1985. Ni kiongozi ambaye ameacha urithi mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini Ufilippini kwanza kabisa kama Padre aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya malezi na majiundo ya makasisi ndani ya Kanisa. Katika maisha na utume wake kama Askofu na Kardinali, alionesha ari na moyo wa unyenyekevu, hekima na busara; ni kiongozi aliyekuwa na Ibada kwa Bikira Maria. Kumbe, Marehemu Kardinali Ricardo Vidal, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Cebu nchini Ufilippini ataendelea kukumbukwa na familia ya Mungu nchini Ufilippini.

Na Padre Richard A. Mjiga, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.