2017-10-19 15:53:00

Papa Francisko: Fedha fedhea, jihadharini msiwe watumwa wa fedha!


Wanafunzi wa “Taasisi Chartreux” kutoka Ufaransa wanapaswa kufundwa vyema ili wanapohitimu masomo yao, waweze kushiriki kikalimifu katika utekelezaji wa majukumu yao katika taasisi za biashara na fedha kimataifa. Haya ni malezi na mjiundo yanayokazia kwa namna ya pekee utu, falsafa na maisha ya kiroho, jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto kuanzia sasa, kuhakikisha kwamba, wanakuwa makini, ili kamwe wasimezwe na uchu wa fedha na mali na hatimaye, kugeuzwa kuwa ni watumwa wa fedha, kwa wale wote wanao abudu na kuthamini fedha kupindukia! Wanafunzi wawe na ari na ujasiri wa kuhoji mkono wa nguvu unaofichika katika soko. Fursa ya masomo wanayoipata wakiwa mjini Roma iwasaidie kukuwa na kukomaa ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na wajenzi wa usawa, haki mintarafu nyumba ya pamoja, yaani ulimwengu!

Ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 19 Oktoba 2017 alipokutana na kuzungumza na wanafunzi wa “Taasisi Chartreux” kutoka Ufaransa walipomtembelea mjini Vatican. Majiundo yao yanawezesha kutambua historia ya mambo mazito yaliyopelekea kuanzishwa kwa Jumuiya ya Ulaya; kwa kushangaa; akili, utashi na matumaini yaliyowawezesha kuibua na hatimaye, kutekeleza mambo mazito, changamoto hata kwa wanafunzi hawa kuhakikisha kwamba, wanaacha alama ya kudumu katika historia, kwani matumaini ya mbeleni yako miokoni mwao!

Baba Mtakatifu anasema ili kuweza kufikia azma hii, hawana budi kuhakikisha kwamba, wana wajibika hapa duniani na kwa maisha ya kila mtu, kwani ukosefu wa haki dhidi ya maskini ni sawa na donda ambalo liko wazi, kwani linadhalilisha utu na heshima yake kama binadamu. Mwelekeo wa ulimwengu mamboleo ni mafanikio ya chapuchapu!

Lakini wao, wajiwekee muda na kutafuta njia halali ili kujenga madaraja ya udugu yanayowaunganisha watu kuliko kuta zinazowatenganisha watu, ili hatimaye, kuweza kujenga jamii inayosimikwa katika haki na utu! Wakristo wanaweza kufikia lengo hili kwa kuungana na Kristo Yesu kwa njia ya sala na kujidhaminisha mbele yake, kamwe wasitumbukie katika kishawishi cha kujikataia au kukatishwa tamaa. Wajitahidi kufanya kazi kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kwa njia ya unyenyekevu waweze kuwa ni mbegu ya ulimwengu mpya. Baba Mtakatifu Francisko akiwa na matumaini haya, anahitimisha hotuba yake huku akiwaaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu na kushirikiana kwa pamoja kama familia moja ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.