2017-10-19 16:00:00

Maji safi na salama na huduma bora za afya ni haki msingi za binadamu


Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu kwani ni muhimu sana katika maisha ya viumbe hai, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu katika Nyanja mbali mbali za maisha. Maji ni kito cha thamani ambacho Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii ya binadamu. Maji ni hitaji muhimu sana la binadamu linalopaswa kulindwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, “Sifa iwe kwako “Juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, bila maji, maisha ya binadamu yako mshakani na hatarini sana!

Kanisa katika Mafundisho Jamii linakazia umuhimu wa matumizi ya maji safi na salama kama njia makini ya kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Kumbe, maji yanapaswa kupatikana kwa wote katika umbali unaokubalika na kwamba, huduma hii iwe ni endelevu! Uchafuzi wa vyanzo vya maji ni hatari sana kwa maisha ya binadamu na ekolojia nzima. Haya ni kati ya mambo msingi yaliyopewa uzito wa juu hivi karibuni na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu wakati alipokuwa anashiriki katika kongamano la maji safi na salama pamoja na huduma bora ya afya kama sehemu ya haki msingi za binadamu.

Kongamano hili liliandaliwa na Mwakilishi wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao yake makuu mjini Geneva, nchini Uswiss kwa kushirikiana na wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa huko Geneva pamoja na “Mfuko wa Caritas in Veritate”. Kardinali Turkson anasema, maji safi na salama ni kikolezo makini cha afya, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu! Maji ni kito cha thamani ambacho binadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya matumizi ya wote na kwamba, hiki ni kiini cha ustawi na maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii ya binadamu. Kanisa limekuwa daima mstari wa mbele kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kutambua kwamba, maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu, ustawi na mafao ya wengi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Jumuiya ya Kimataifa imeendelea kutoa uzito wa hali ya juu kwa maji safi na salama. Kwa kuibua sera na mbinu mkakati wa maboresho ya huduma ya maji safi na salama; kwa kugaribisha na kutunga sheria za utunzaji bora wa vyanzo vya maji kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya hali na afya ya jamii na maendeleo endelevu ya binadamu. Ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha kwamba, linalinda na kutunza vyanzo vya maji dhidi ya uchafuzi unaoweza kusababisha maafa makubwa kwa afya ya watu. Ikumbukwe kwamba, maji safi na salama ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hili ni hitaji msingi la binadamu wote.

Kardinali Turkson anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Laudato si” juu ya utunzaji bora wa mazingira anakaza kusema maji ni kito cha tamani katika maisha ya binadamu, ni sehemu ya haki msingi za binadamu, bila maji, maisha ya binadamu yako hatarini na mashakani na kwamba, haki hii inakwenda sanjari na huduma bora ya afya. Uchafuzi wa vyanzo vya maji ni hatari kwa ustawi, maendeleo na ekolojia ya viumbe hai. Magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasio safi na salama yamekuwa pia ni chanzo cha vifo vya watoto wengi wenye umri chini ya miaka 5 hasa katika Nchi zinazoendelea duniani.

Matumizi ya maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu yatasaidia kukuza na kudumisha haki jamii na amani, kanuni maadili na mshikamano kati ya watu. Maji ni muhimu sana katika kudumisha ekolojia endelevu. Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali haina budi kudhibiti  matumizi sahihi ya maji pamoja na hifadhi yake. Kwa miaka ya hivi karibuni maji pia kwa njia ya mafuriko na ukame yamekuwa ni sababu ya majanga makubwa katika maisha ya binadamu. Maji yasipopewa msukumo wa pekee yanaweza kuwa sababu ya vita na kinzani kwa siku za usoni.

Utu na heshima ya binadamu; umuhimu wa maisha, ustawi na maendeleo ya wengi ni kati ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa badala ya kusukumwa na matumizi ya maji kama bidhaa kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache katika jamii. Jumuiya ya Kimataifa ijenge na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano badala ya kugubikwa na uchoyo na ubinafsi katika matumizi ya rasilimali za dunia. Matumizi bora ya maji safi na salama, uwe ni mwelekeo unaopania kudumisha haki hii msingi katika maisha ya binadamu anasema Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.