2017-10-18 09:49:00

Siku ya Kupambana na Umaskini:"Njia ya kuelekea jamii zenye amani na umoja"


Kila ifikapo tarehe 17 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini duniani ambapo takwimu za mwaka jana 2016 inakadiriwa watu bilioni moja wanaishi katika umaskini uliokithiri huku wengine zaidi ya milioni 800 wakikabiliwa na njaa. Mataifa 10 kutoka barani Afrika yanashika nafasi za juu katika orodha ya nchi maskini duniani. Katika kilele cha Siku ya Kupambana na Umaskini duniani yenye kuwa na kaulimbiu ya mwaka 2017 ''Njia ya kuelekea jamii zenye amani na umoja'' ni kuzingatia wito uliotolewa miaka 25 iliyopita ya kutambua ujuzi na ujasiri wa familia zinazoishi katika umaskini duniani kote, umuhimu wa kuwafikia zaidi maskini na kuanzisha ushirikiano na wananchi wanaotoka katika mazingira yaliyokuwa na umaskini na wenye nia ya kuutokomeza umaskini. Aidha  kaulimbiu ya mwaka huu inakumbushia umuhimu wa maadili ya heshima, mshikamano na kuwa na sauti moja katika kuitikia wito wa kuutokomeza umaskini kila mahali.

Jumapili baada ya Misa Takatifu ya kuwatangaza watakatifu wapya hata  Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbushaumati wa waamnini juu ya  Siku ya Kupambana  na Umaskini duniani.  Baba Mtakatifu amesema, Umaskini siyo maafa: una sababu  zake ambazo ni lazima kutambuliwa na kuondolewa, ili kuheshimu hadhi ya ndugu  kaka na dada wangi duniani. Pamoja na ujumbe huo hata mwaka Jana alikuwa amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuunganisha nguvu zao za kimaadili na kiuchumi katika mapambano dhidi ya umaskini unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa kujikita katika sera makini zinazosimamia tunu msingi za kifamilia pamoja na kazi bila kusahau sala kwa ajili ya kuombea amani.

http://sw.radiovaticana.va/news/2017/10/15/papa_ametangaza_sinodi_ya_maaskofu_oktoba_2019_kwa_ajili_ya_amazon_/1343169 

Aidha katika mikutano ya hivi karibu huko Ujermani wa mataifa makubwa G20 mapema mwaka, pamoja na masuala nyeti waliyozungumzia  walijikita katika masuala ya kitaifa na kimataifa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu ili kupambana na baa la umaskini na njaa duniani. Umoja wa Mataifa ndio uliotangaza siku hiyo kwa lengo la kukutanisha pamoja nguvu za mataifa yote ya dunia katika jambo moja, ambalo ni kupambana na umaskini. Kila mwaka siku hiyo hutumiwa kutangaza mshikamano wa mataifa yote ya dunia kwa ajili ya kuwapa moyo na faraja hasa walea wahanga wa ukata na majanga ya njaa na vilevile kutafuta njia za kuweza kung'oa kikamilifu mizizi ya umaskini na ubaguzi ili kudhamini heshima na utukufu wa mwanadamu.

Mwaka huu pia ni kumbukumbu ya miaka 30 ya Siku ya Kuushinda Umaskini Uliokithiri Duniani. Siku hii ilitambuliwa na Umoja wa Mataifa baada ya wito uliotolewa na Padre Joseph Wresinski. Tarehe 17 Oktoba 1987, watetezi wa haki za binadamu na haki za kiraia kutoka duniani kote walikutana mjini Paris, Ufaransa kwa lengo la kuahidi kuonyesha mshikamano na watu wote ulimwenguni na kujitahidi kuondoa umaskini uliokithiri.
Pamoja na hayo wito huo ulichukuliwa na kufanyiwa kazi katika nchi nyingi duniani na umewawezesha watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri kuvunja ukimya na kuzungumza kuhusu umaskini pamoja na kuchukua hatua katika kushirikiana na wale wanaotamani kuwa washirika wao. Tangu wakati huo watu, taasisi na jumuiya mbalimbali duniani huadhimisha siku ya tarehe 17 Oktoba kama siku ya kuonesha kwa mara nyingine tena mshikamano na ushirikiano wa kung'oa mizizi ya umaskini duniani.

Tarehe 17 Oktoba 1992  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza rasmi siku hiyo kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini. Suala la kupambana na umaskini lilipata nguvu zaidi kuanzia mwaka 2000 mara baada ya kupitisha Hati ya Milenia ambayo moja ya malengo yake makuu ilikuwa ni kuhakikisha umaskini umepungua kwa kiwango kikubwa duniani kufikia mwaka 2015.
Licha ya kuweka jitihada mbalimbali za kufanikisha malengo ya Milenia ya kung'oa mizizi ya umaskini duniani, lakini maeneo mengi ya dunia yanaishi kwenye umaskini wa kukithiri zaidi. Umoja wa Mataifa unaendesha miradi mbalimbali ya kufanikisha malengo ya milenia ili kupungaza umaskini kwa kiwango kikubwa duniani. Hata hivyo bado kuna mamilioni ya watu hususan watoto wadogo ambao wanaishi katika ukata wa kupindukia. Takwimu za mwaka jana lilikuwa linaonesha kuwa watu milioni 780 wanaofanya kazi hawawezi kupata pato linaloweza kuwaondoa wao wenyewe na familia zao chini ya mstari wa umaskini yaani pato la zaidi ya dola mbili kwa siku.

Kiwango hicho kinaunda thuluthi moja ya watu wanaofanya kazi katika nchi zinaondlea. Robo ya wafanyakazi katika nchi zinazoendela pia wanapata dola kati ya 2 na 4 kwa siku. Kundi hili ambalo haliko mbali na mstari wa umaskini daima limekuwa katika hatari ya kutumbukia kwenye ukata na ufukara kutokana na sababu mbalimbali kama vile maradhi na kadhalika. Umaskini na ufukara pia vina mfungamano na masuala ya kiroho na kisiasa. Umaskini huwaathiri wanadamu kwa sura mbalimbali na kwa makali tofauti kulingana na vipindi mbalimbali, nafasi zao na hali za watu binasfi. Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) linatoa taarifa kuwa umaskini ni kutokuwa na pato la kiasi fulani, kutokuwa na hadhi na fursa za kupata elimu na au kutokufanya harakati za kijamii pia kutoshirikishwa katika kuchukua maamuzi.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anasema aina nyingi za umaskini zinasababishwa na kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira, kukosekana kwa usalama na usawa, mizozo na mabadiliko ya tabia nchi. Anaongeza kusema, leo tunaungana na watu milioni 800 duniani wanaoishi katika umaskini uliokithiri. Lakini tumepiga hatua katika kuondoa umaskini tangu 1990 na nchi zote zimejizatiti katika kuutokomeza umaskini. Ajenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu inaahidi kuhakikisha dunia yenye afya, salama na kujenga jamii iliyo na amani na umoja unaoheshimikwa kwa wote.

Umuhimu wa uelewa wa umma, sauti ya pamoja na kuwashirikisha ipasavyo watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri, unatambuliwa katika ajenda yenyewe na kwenye mchakato wa mashauriano yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba uwajibikaji na vipaumbele vya mamilioni ya watu, hasa wale wanaoishi katika umaskini uliokithiri, wanajumuishwa na kusikilizwa. Kushirikishwa ipasavyo kwa watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri, kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu. Kampeni ya kimataifa pia inawakaribisha watu binafsi, jumuiya, mashirika na nchi mbalimbali kuifanya siku hii katika njia tofauti, ikiwemo kugundua au kuelezana jinsi umaskini unavyoweza ukatokomezwa, wakati watu wanapoungana pamoja katika juhudi za kuimarisha haki kwa wote.

Sr Angela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.