2017-10-17 14:57:00

Jubilei ya Miaka 800 ya uwepo na utume wa Wafranciskani Nchi Takatifu


Jubilei ya Miaka 800 ya Utume wa Shirika la Wafranciskani katika ulinzi wa maeneo matakatifu kwenye Nchi Takatifu ni tukio ambalo limepambwa kwa shughuli mbali mbali za kidini, kichungaji na maisha ya kiroho kama kumbu kumbu endelevu ya mchango wa watawa hawa katika, maeneo ambamo Neno wa Mungu alifanyika mwili na kukaa kati ya watu wake, huyu ndiye Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Uwepo wa watawa hawa ni ushuhuda wa imani ya Kikristo pamoja na wale wote wanaotaka “kujichimbia” katika tafakari na masomo ya sayansi ya Biblia bila kusahau kwamba, wao wamekuwa ni chemchemi ya ukarimu kwa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotembelea maeneo haya matakatifu!

Ilikuwa ni mwaka 1217 Mtakatifu Francisko wa Assisi, wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa Shirika alipoamua kulipatia Shirika lake mwelekeo wa kimisionari na kiulimwengu, ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani. Tangu wakati huo, sehemu hii ikawa ni Kanda ya Nchi Takatifu ya Shirika la Wafranciskani. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 yalizunduliwa tarehe 11 Juni 2017, huko Acri, mahali ambapo watawa wa kwanza walianza kupiga kasia kuelekea Nchi Takatifu, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa umoja, udugu, upendo na amani kwa watu kutoka katika makabila na dini mbali mbali. Tangu wakati huo, Wafranciskani wameonesha ukarimu wa ajabu sana kwa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuwaongoza na kuwatembeza katika maeneno matakatifu, kiasi cha kuwasaidia waamini kuchapa Maandiko Matakatifu katika sakafu ya mioyo yao kwa sura na shuhuda kutoka katika maeneo matakatifu bila kusahau huduma ya kichungaji kwa Makanisa mahalia na ulinzi kwa madhabahu mbali mbali.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Padre Francesco Patton, O.F.M, Mlinzi mkuu wa maeneo matakatifu, wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 ya uwepo na huduma makini katika Nchi Takatifu. Papa Francisko anawataka watawa hawa kuendelea kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwapatia watu matumaini na kuwajengea msingi wa amani katika maeneo haya ambamo amani bado ni ndoto.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana na watangulizi wake, na kwa namna ya pekee na Papa Clement VI ambaye katika Waraka wake wa Kitume “Gratias agimus” yaani “Shukuruni daima” aliwadhaminisha Wafranciskani utunzaji wa Maeneo Matakatifu na kuwataka kuendeleza utume huu, kama mashuhuda wa furaha ya Injili ya Kristo Mfufuka katika Nchi Takatifu. Anawataka kuwa ni mabalozi wa watu wa Mungu, ambao wanaendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya Kanisa katika Nchi Takatifu, ili imani kwa Kristo Yesu iendelee kushuhudiwa katika huduma. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa kumuunga mkono kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa namna ya pekee, wakati huu, Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki wakati huu linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake! Anawataka kujenga na kudumisha amani bila kushutumiana kwa jambo lolote lile, bali wawe wanyofu na wenye amani; watulivu, watu wa kiasi na wavumilivu; daima wajifunze kuwa wakweli kwa watu wote na hivi ndivyo inavyotakiwa. Baba Mtakatifu Francisko anawaweka wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na Mtakatifu Anthony wa Padua.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.