2017-10-17 10:33:00

Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Manyoni, Jimbo Katoliki Singida


Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida, kuanzia tarehe 19 Oktoba hadi tarehe 21 Oktoba 2017, Kumbu kumbu ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo mwanzilishi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, atakuwa na ziara ya kichungaji Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni, Manyoni ili kuzindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni ilipoanzishwa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kunako mwaka 1967. Askofu Mapunda anatembelea ili kukagua maendeleo ya Parokia: kiroho na kimwili; ataweka jiwe la msingi wa ujenzi wa Kigango cha Msemembo pamoja na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini wa Parokia ya Manyoni, kielelezo makini cha ukomavu wa imani unaowadai kuilinda na kuishuhudia katika matendo.

Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Jubilei Manyoni, Imani na Matendo” (Rej. Yak. 2: 16-18). Imani bila matendo hiyo imekufa ndani mwake! Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ilikuwa ni changamoto kwa familia ya Mungu kuhakikisha kwamba, inamwilisha huruma na upendo wa Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Ndiyo maana familia ya Mungu Parokiani Manyoni inapenda kumwimbia Mungu utenzi wa sifa, shukrani, toba na wongofu wa ndani kwa kuhakikisha kwamba, imani hii inakuwa ni sehemu ya ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Kilele cha Jubilei hii ni hapo tarehe 13 Mei 2018, Mama Kanisa atakapokuwa anaadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni. Tukio hili ni sehemu pia ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, familia ya Mungu nchini Tanzania inapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa sadaka na majitoleo ya Wamisionari waliosaidia kupandikiza imani na sasa matunda ya kazi hii yanaanza kuonekana Kanisa la Tanzania kuendelea kushamiri katika sekta mbali mbali za maisha ya kiroho na kimwili!

Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Manyoni, Singida ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uinjilishaji wa kina uliowawezesha watu wa Mungu Parokiani Manyoni kupata huduma makini: kiroho na kimwili na kwamba, uwepo wa wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Manyoni, Singida na Tanzania katika ujumla wake, umesaidia sana katika kukoleza huduma makini katika mchakato wa ukombozi wa mtu mzima: kiroho na kimwili. Manyoni kimekuwa ni kitovu cha huduma ya maji safi na salama kwa watu waliokuwa wanaishi katika maeneo yenye ukame wa kutisha!

Manyoni ni chimbuko la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida na leo hii imekuwa chemchemi ya huruma ya huruma ya Mungu na kitovu cha huduma bora ya afya kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na magonjwa yao. Manyoni, imekuwa ni chimbuko ya ukombozi kwa wasichana na wanawake, waliokuwa wanaelemewa kwa kiasi kikubwa na mfumo dume, leo hii kwa njia ya elimu makini na endelevu kutoka katika Chuo cha ufundi hadi kufikia sekondari, wasichana wanaohitimu katika taasisi za Kanisa wamejengewa uwezo mkubwa katika kupambana na changamoto za maisha yao ndani na nje ya Manyoni!

Elimu imewajengea vijana wengi fursa za ajira binafsi na wengi wao wamepata mafanikio makubwa kutokana na nidhamu, bidii, juhudi na maarifa waliyojengewa wakati wakiwa chuoni hapo! Huduma kwa wazee na watoto yatima imepewa msukumo wa pekee kabisa katika maisha na utume wa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu! Kijiji cha Matumaini, Jimbo kuu la Dodoma kwa ajili ya watoto waliothirika kwa ugonjwa wa Ukimwi, ni ndoto iliyoanzia Manyoni, leo hii kuna watoto waliozaliwa, wakatunzwa na kulelewa na Kijiji cha Matumaini, leo ni watu wazima wanaojitegemea na kuwategemeza ndugu zao! Kwa hakika ndoto ya Mtakatifu Gaspar, bado inaendelea!

Padre Thomas Wambura, Paroko wa Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni, Manyoni, Jimbo Katoliki la Singida anasema, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Parokia hii ni muda pia wa kuomba toba, huruma na upendo wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa wakati huu, mkazo zaidi ni kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa kuhuisha na kupyaisha imani, ili iweze kumwilishwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Ni kipindi cha kuimarisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo: Shule ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Jubilei hii inapania kuimarisha makuzi ya kiroho, kiutu na kimaadili, ili kuwajengea watu wa Mungu uwezo wa kupambana na changamoto za maisha mintarafu Neno la Mungu, Mafundisho Jamii ya Kanisa, kanuni maadili na utu wema. Ili kufanikisha matamanio yote haya, Parokia inapania kuimarisha mfumo wa uongozi na utekelezaji wa sera na mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Pia inataka kukuza moyo na ari ya waamini kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali ili kuondokana na tabia ya kutegemea wafadhili ambayo kwa sasa imepitwa na wakati! Miaka 50 ni muda muafaka wa kujijengea utamaduni wa kujitegemea! Ni wakati muafaka wa kujenga Makanisa bora zaidi vigangoni pamoja na kukarabati yale yaliyopo, ili kweli waamini waweze kuwa na mahali pazuri zaidi pa sala na ibada kwa kusoma alama za nyakati!

Kama sehemu ya kumbu kumbu hai ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Manyoni, Singida, familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki Singida inapania kuchangia ujenzi wa shule ya awali na msingi itakayoendeshwa na kusimamiwa na Parokia, kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika malezi na makuzi ya watoto na vijana wa kizazi kipya. Hii ni kumbukumbu inayoanzishwa katika Mwaka wa Bwana kama ushuhuda wa imani katika matendo kwa kizazi cha sasa na kile kijacho! Makisio ya awali ya gharama za ujenzi wa miundo mbinu ni shilingi milioni 206, 700, 000. Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imetoa ardhi yenye ukubwa wa Ekari 18. Familia ya Mungu inaendelea kuchangia fedha na vifaa vya ujenzi. Ni matarajio ya viongozi wa Parokia kwamba, shule hii itaweza kuzinduliwa wakati wa kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni, Manyoni, mwaka 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.