2017-10-17 10:10:00

Chuchumilieni utakatifu kama kielelezo cha maisha na utume wenu!


Waamini wanaposhiri kikikamilifu adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, nyoyo zao zinashibishwa kwa Neno la Mungu na chakula cha uzima wa milele na hivyo kushiriki maisha ya Kimungu. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumatatu, tarehe 16 Oktoba 2017 imetoa utambulisho wa Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa anayetumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu bila kigugumizi, kwani amehesabiwa kuwa ni kati ya watumishi wa Mungu, kama anavyofafanua Nabii Isaya. Mtume Paulo, anatumwa kuwatangazia watu wote Habari Njema ya Wokovu.

Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ndiye kiini cha Injili inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa ari na moyo mkuu. Mtume Paulo anasema amekirimiwa nguvu ya Roho Mtakatifu, chemchemi ya utakatifu uliomo ndani mwake! Hii ndiyo nguvu ya Roho Mtakatifu inayowezesha hata waamini kuwa watakatifu kama Paulo Mtume anavyowaandikia Warumi kwamba, wanaitwa kuwa watakatifu, huku wakikirimiwa neema na amani itokayo kwa Mungu Mwenyezi. Wakristo wanakumbushwa kwamba, wao wameitwa na kuteuliwa na Mwenyezi Mungu ili kuunda taifa jipya la Israeli, lililopendwa sana na Mwenyezi Mungu hata akalipatia nafasi ya pekee katika historia nzima ya ukombozi!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa, Jumatatu, tarehe 16 Oktoba 2017 na Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican wakati ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafanyakazi katika Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican waliokuwa wanahudhuria semina maalum kama sehemu ya majiundo yao endelevu, katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa katika tasnia ya vyombo vya habari vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Vatican. Anasema, kiini cha Neno la Mungu ni mwaliko na changamoto ya kuambata utakatifu wa maisha kila mwamini kadiri ya wito na dhamana yake katika maisha na utume wa Kanisa.

Kama Wakristo, anasema Monsinyo Dario Edoardo Viganò, wao wameteuliwa kwa namna ya pekee, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kuwa sehemu ya watu wa Kristo ni dhamana nyeti sana, inayofumbata masha ya mtu mzima, changamoto ni kutubu na kumwongokea Mungu, ili kufurahia uwepo wake katika maisha yao. Malkia wa Sheba na watu wa Ninawi, walitubu na kumwongokea Mungu kwa mahubiri yaliyotolewa na Yona. Leo hii, pengine kuna baadhi ya waamini wanadhani kwamba, hawana sababu ya kutubu na kumwongokea Mungu, kwani Ukristo kwao ni maisha ya raha mustarehe.

Baba Mtakatifu Francisko katika mwelekeo kama huu, ni mkali na anapenda kuwakemea Wakristo ambao ni wavivu, wanaobweteka bila ya kujihangaisha katika maisha na wito wao; Wakristo wanaodhani kwamba, tayari wao “wameokoka”, hawaoni tena sababu ya Kanisa, kwani Kanisa kwao linageuka kuwa ni mahali pa “maegesho”. Monsinyo Dario Eouardo Viganò, anakaza kusema, Wakristo wavivu ni kundi kubwa linalowameza waamini walei na hata wakleri! Kumbe, Wakristo wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanachakarika katika kutafuta utakatifu wa maisha; kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Watoe nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwapatia neema ya maisha mapya, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kati ya watu wa Mataifa.

Kwa njia ya Ubatizo, Wakristo ni Manabii na Wamisionari wanaoitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Watambue kwamba, maisha yao ni safari inayopaswa kuwaelekeza katika ukamilifu wa maisha ya Kikristo na utakatifu wa maisha. Mwishoni, Monsinyo Dario Edoardo Viganò amewaalika wafanyakazi katika Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka ya matumaini ya maisha yao; mateso na mahangaiko yao ya ndani; furaha na upendo; ili yote haya yaweze kuunganishwa na sadaka ya Kristo Yesu inayotolewa Altareni, ili iweze kumpendeza Mungu, asili ya zawadi zote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.