2017-10-14 09:26:00

Itikieni wito wa Kimungu kwa kuwa na vazi la harusi!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XXVIII ya Mwaka A wa Kanisa inaonesha matumaini ya watu wa Mungu watakavyoshirikishwa katika karamu ya maisha ya uzima wa milele kwenye Ufalme wa Mungu. Karamu hii ni kielelezo cha Fumbo la Ekaristi Takatifu ambamo mwamini analishwa kwa Neno la uzima na kupewa chakula cha maisha ya uzima wa milele. Jambo la msingi hapa ni kuhakikisha kwamba, waamini wanaadhimisha Fumbo hili kwa ibada na uchaji; katika roho na haki, kama kielelezo cha vazi la harusi na wala si kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa mazoea. Katika Juma hili, tumwombe Mwenyezi Mungu atukurimie vazi la harusi linalopambwa kwa: ukarimu, msamaha, kiasi, unyenyekevu na huruma. Uwe ni muda wa kutulia na kutafakari ukuu na huruma ya Mungu katika maisha ya kila mmoja wetu!

Harusi ni kielelezo cha furaha na wokovu ulioletwa na Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Ni ushuhuda wa umoja, upendo, mshikamano na uaminifu wa Kristo Yesu kwa Kanisa lake. Harusi ni mwaliko wa kutambua ukuu na utakatifu wa Injili ya ndoa na familia, inayowashirikisha wanandoa katika mpango mzima wa kazi ya uumbaji. Tuungane na Baba Mtakatifu Francisko anapowatangaza wenyeheri kuwa watakatifu kati yao kuna kundi kubwa la waamini walei, mapadre na vijana waliomimina maisha yao kwa ajili ya uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake

Mwenyezi Mungu huwahangaikia watu wake, anajisikia kuwajibika, kwa maaana ya kwamba anatamani kuwaona watu watu wake wakiwa na afya njema, wakiwa wamejaha furaha na amani tele. Mwenyezi Mungu hushughulikia mahitaji yao na huwaandalia mema daima katika ulimwengu huu na ule ujao. Maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanatupatia nafasi ya kutafakari sifa hii ya Mungu na kuona nini tunachopaswa kufanya ili kunufaika na yale ambayo Mungu anayashugulikia na kuyaandaa kwa ajili yetu.

Katika Injili, Kristo anatoa mfano - simulizi kuhusu ufalme wa Mungu. Ufalme anaouelekezea kama sherehe ya harusi ambayo mfalme mmoja alimfanyia mwanawe na akaalika watu kuja kushiriki. Katika mfano huu, Kristo anatumia vitu vinavyoonekana, vya kimwili na vilivyozoeleka katika maisha ya kawaida ya mwanadamu - sherehe, harusi, vinono, mwaliko na kadhalika ili kutupa picha ya mambo makubwa zaidi ambayo Mungu humwandalia kila mmoja wetu. Tena kwa jinsi ile ile ya huyo mfalme, Mungu hutuma mwaliko kwa kila mmoja mmoja wetu kuwa ‘vyote vimekuwa tayari, njooni arusini’.

Ni nini Mungu amekuandalia na ni vitu gani vilivyo tayari? Ni yote yanayohitajika kwa ajili ya usalama na ustawi wa nafsi yako nzima kama mwana mpendwa wa Mungu. Tena ni yote na katika ukamilifu wake unayohitaji kwa ajili ya wokovu wako. Kama ilivyokuwa kwa harusi aliyoisimulia Kristo, ile taswira ya wageni waalikwa kutoa udhuru katika arusi ya mwana mfalme huwa pia taswira ya maisha yetu kutoa udhuru kwa mema anayotuandalia Mwenyezi Mungu. Namna ile ile waliyoitumia wageni wale ndiyo namna inayotutawala hadi leo: kwenda shambani na kwenye biashara - yaani kusongwa na wajibu mbalimbali tulizonazo na shughuli za kutafuta mahitaji ya maisha kwa kiasi kinachofunika nafasi ya Mungu na kipaumbele chake katika maisha yetu na kutusahaulisha kabisa kwamba uzima, usalama na wokovu wetu uko kwa Mungu pekee. Kwa bahati mbaya zaidi wakati mwingine mizunguko hiyo ya kimaisha huondoa kabisa akilini mwetu fikra kwamba uzima, usalama na wokovu ni vitu tunavyohitaji na bila hivyo maisha yetu huwa kama kasha lililo tupu.

Nyakati tulizomo sasa, nyakati za mabadiliko ya mfumo ya maisha na harakati zake unaosababishwa hasa na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi, ni nyakati za kutopoteza kabisa kipaumbele chetu kwa mwaliko wa kimungu. Je, tunawezaje kutopoteza kipaumbele kwa mwaliko wa kimungu katika harakati za maisha katika nyakati zetu hizi? Somo la Pili linatualika tujifunze kutoka kwa Mtakatifu Paulo. Yeye alipitia kila hali katika maisha: kukosa, kufanikiwa, kushiba, kuona njaa, kuwa na vingi na kuishiwa bila kupoteza kipaumbele kwa mwaliko wa kimungu. Sababu ya kutopoteza kipaumbele hicho anaeleza mwenyewe kuwa alijifunza kuridhika katika maisha na hivyo anathubutu kusema “nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. Pasipo kujifunza kuridhika maisha yetu yatageuka kuwa ni mahangaiko yasiyotulia ya kutafuta tunachodhani kitatupa ukamilifu na kumbe baada ya kukipata tunagundua kinapungua kwa mbali sana kutoka ukamilifu unapatikana katika mwaliko wa kimungu.

Ni dhahiri kuwa kuridhika hakumaanishi katu kujinasua katika kutimiza wajibu tulionao na kukaa tu. Hakumaanishi pia kutokufanya jitihada za ziada kuboresha hali zetu, mazingira na maisha kwa ujumla. Pamoja na hayo yote na zaidi ya hayo yote, kuridhika ni karama inayotusaidia kutambua kuwa sisi sote na maisha tuliyonayo tupo mikononi mwa Mungu na katika maongozi yake. Harakati za maisha zinapaswa kutusaidia kuwa karibu zaidi naye kuliko kututenga naye. Tumwombe Mungu atujalie karama ya kuridhika, ili tunapokipata kila kitu katika maisha yetu nafasi yake tutoe daima kipaumbele kwa mwaliko wa kimungu.

Padre William Bahitwa.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.