2017-10-12 13:05:00

Jubilei ya Miaka 25 ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki: Adhabu ya kifo!


Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki ambao ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti, Maisha adili na Maisha ya Sala, iliyopitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kama sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hii ni Amana ya imani ya Kanisa inayoshuhudia uzuri wa imani kwa Kristo Yesu; urithi wa ukweli kutoka kwa Mababa wa Kanisa pamoja na matarajio ya watu wa Mungu kwa nyakati hizi, mwendelezo wa hija ya Mama Kanisa katika kipindi cha karne ishirini zilizopita. Kanisa lina dhamana ya kulinda na kudumisha ukweli unaofumbatwa katika Injili, ili kuweza kufikia utimilifu wake.

Hii ni neema ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia watu wake kama dhamana na utume unaowawajibisha kwani unabubujika kutoka katika matumaini ya Kikristo yanayopambwa kwa dawa ya huruma ya Mungu. Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana ya mafundisho tanzu ya Kanisa, msaada wa Roho Mtakatifu unaoliwezesha Kanisa kuangaza imani, changamoto na fursa zilizopo kwa sasa. Hiki ni chombo na jibu makini la imani linalotoa maana ya maisha ya mwanadamu katika kipindi hiki maalum ili kukabiliana na changamoto zinazomkabili mwanadamu na Kanisa ili kuweza kutangaza na kushuhudia upya wa Injili ya Kristo inayofumbatwa katika Neno la Mungu. Hii ni hazina ya mambo ya kale na mambo mapya!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano,  jioni tarehe 11 Oktoba, 2017, wakati alipokutana na kuzungumza na washiriki wa kongamano lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa uinjilishaji mpya kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuchapishwa kwa Katekisimu ya Kanisa Katoliki. Kipaumbele cha kwanza ni utii kwa mitume wa Yesu unaowataka kulinda na kudumisha umoja wa Kanisa kama utimilifu wa utume wa Kristo Yesu hapa duniani. Hii ni changamoto ya kutaka kumfahamu Mwenyezi Mungu kama kielelezo cha upendo kwa Baba wa mbinguni. Kristo Yesu anaendelea kufanya hija na waja wake kwa maneno na ishara mbali mbali, mwaliko kwa waamini kujibidisha zaidi kulifahamu pendo hili.

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni matunda ya Katekisimu ya Kirumi ambayo inakazia kwamba, hatima na kiini chote cha mafundisho ya imani vinaelekezwa katika upendo ambao hauna kikomo. Iwe inaelekezwa kwa ajili ya ukweli wa imani au, matumaini au wajibu wa utendaji wa maadili, upendo wa Mungu utadumu daima.  Kwa kusoma alama za nyakati, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na uhai wa binadamu dhidi ya adhabu ya kifo inayokumbatia utamaduni wa kifo.

Mwenyezi Mungu anawapatia waja wake nafasi ya kutubu na kumwongokea, ili aweze kuwakirimia msamaha na kuwaonjesha tena huruma na upendo wake usiokuwa na kifani! Adhabu ya kifo ilitolewa kama alama ya utekelezaji na upatikanaji wa haki, hali ambayo hata Vatican katika sheria zake, imeitumia adhabu hii kiasi hata kushindwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huruma katika haki. Hii ni hali iliyofumbatwa katika madaraka na uchu wa mali ya dunia, kiasi cha kuwafanya watu kushindwa kuzama katika undani wa Injili. Kanisa leo hii linataka kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, hapa hakuna kinzani na Mafundisho ya Kanisa yaliyopita, kwani jambo la msingi hapa ni kusimama kidete kulinda uhai wa binadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwendelezo wa uelewa wa kina wa Mafundisho tanzu ya Kanisa kwani adhabu ya kifo ina athari kwa utu na heshima ya binadamu. Hivyo Kanisa katika mafundisho, maisha na ibada zake, linaendeleza daima na kuvirithisha vizazi vyote ukweli juu yake, na juu ya yale anayoyaamini. Huu ni muhtasari wa asili na utume wa Kanisa unaofafanuliwa katika mafundisho na maisha yake kama chachu muhimu inayowaunganisha na kuwawezesha waamini kuwa ni watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Amana ya imani” ni endelevu kama lilivyo pia Neno la Mungu linalokuwa na kuendelea kukomaa katika maisha ya waamini na kamwe haliwezi kudumazwa na binadamu kama anavyobainisha Mtakatifu Vincent wa Lèrins kwani hii ni sehemu ya ukweli mfunuliwa unaotangazwa na kurtithishwa na Mama Kanisa na wala si mabadiliko ya Mafundisho tanzu ya Kanisa, kwani hii pia ni kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa. Kama ilivyokuwa wakati wa Agano la Kale Mwenyezi Mungu ambaye alinena zamani na mababa katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi na sasa anazungumza kwa njia ya Mwanaye Kristo Yesu, mwaliko kwa waamini kuisikiliza sauti hii kwa umakini, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kama ilivyokuwa wakati wa Kanisa la mwanzo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.