2017-10-11 07:38:00

Parokia ya Theresa wa Mtoto Yesu, Jimbo kuu Dodoma: kitovu cha utume!


Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa. Ni mahali ambapo familia ya Mungu inakusanyika kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Ni kiini cha umoja, upendo na mshikamano unaooneshwa na waamini kutoka katika familia na vigango mbali mbali vinavyounda parokia husika. Ni mahali muafaka pa kateksi na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema hapa ni mahali ambapo waamini wanapata nafasi ya kufafanuliwa kwa kina na mapana Neno la Mungu wakitambua kwamba,  wao ni wahudumu wa Neno la wokovu; uzima wa milele, upatanisho na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Wakristo ni wahudumu wa ukweli na nguvu ya Neno la Mungu, wanaopaswa kujenga umoja na kushikamana kidugu katika maisha na sala!

Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, inayoadhimishwa na Mama Kanisa, kila mwaka ifikapo tarehe 1 Oktoba, Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, amezindua Parokia mpya ya Theresa wa Mtoto Yesu ili kusogeza huduma za kichungaji kwa familia ya Mungu katika eneo hili. Waamini wanakumbushwa kwamba, utume wa Kanisa ni kiini cha imani ya Kikristo na kwamba, Wakristo wote, kila mtu kwa nafasi, wito na dhamana yake anatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima.

Utume wa Kanisa unafumbatwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuambata zawadi ya wokovu ambayo kimsingi, Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake. Huu ndio mwelekeo wa jumla katika kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari na kitume katika Parokia husika. Kwa namna ya pekee, Mama Kanisa anawataka vijana kuwa ni wadau wakereketwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa hasa wakati huu wa mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Waamini wawe ni mashuhuda na chachu ya upendo na mshikamano unaovuta kama sumaku, ili wale waliokuwa wamelegea katika imani, waweze kusimama tena na kuanza kupata huduma za kiroho!

Askofu Mkuu Kinyaiya anawataka waamini wa Parokia mpya ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu kuonesha moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kutumia fursa hii hadimu katika maisha yao ya kiroho, ili kuweza kurekebisha kasoro katika maisha yao, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Ibada ya kutabaruku Kanisa la Parokia ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wahakikishe kwamba, wanalitegemeza Kanisa kwa hali na mali, lakini hasa kwa njia ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko! Kanisa ni nyumba ya Mungu, inapaswa kutumika kwa ajili ya sala, sadaka na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Kinyaiya amewapongeza waamini ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanakamilisha ujenzi wa miundo mbinu ya Kanisa na nyumba ya mapadre, ili kukamilisha mchakato wa uundwaji na uzinduzi wa Parokia mpya ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu.

Kama sehemu ya kumbu kumbu hai na endelevu ya Parokia hii, Askofu Mkuu Kinyaiya amefungisha ndoa takatifu kwa familia nne, ambazo zinatakiwa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia inayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya Mafundisho ya Kanisa, ili kweli familia hizi ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya utakatifu, upendo, huruma, haki, amani na maridhiano. Ni mahali pa kuwafunda watoto malezi bora kwa kutambua kwamba, wazazi ni Makatekista wa kwanza wa maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu!

Tukio hili limehudhuriwa na waamini kutoka Parokia mbali mbali za Jimbo Katoliki Dodoma, wawakilishi wa dini, madhehebu na viongozi wa vyama vya kisiasa na Serikali katika ujumla wake. Waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda na familia yake ni kati ya waasisi wa Parokia hii, ambao wanakumbukwa kwa  namna ya pekee katika kutoa hamasa katika ujenzi wa Kanisa hadi kufikia hatua hii! Jimbo kuu la Dodoma kwa sasa linaendelea kukua kwa kasi sana, baada ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Jemedari mkuu Dr. John Pombe Magufuli kuanza kutekeleza kwa vitendo uamuzi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa kuhamia Dodoma kama Makao makuu ya Tanzania. Takwimu zinaonesha kwamba, “vigogo” wengi wa wizara tayari wamehamia Dodoma. Makamu wa Rais yuko mbioni kuhamia na Rais Magufuli atakunja “jamvi la kuhamia Dodoma, hapo mwakani”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa Radio Mwangaza Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.