2017-10-11 07:18:00

Maaskofu Katoliki Ulaya: Dumisheni utu wa binadamu na jengeni umoja!


Bara la Ulaya linapaswa kutambua kuwa utu na heshima ya binadamu ni ukweli unaofumbatwa hata katika maisha ya kiroho licha ya tofauti zake za kiuchumi, kisiasa na kijiografia. Mama Kanisa kwa upande wake anapenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi, maendeleo na haki msingi za binadamu dhidi ya utamaduni wa ubinafsi na mifumo ya ubaguzi! Bara la Ulaya linapaswa kutambua kwamba, lina hazina kubwa ambayo imefichika katika sakafu ya maisha yake, ambayo linapaswa kuwashirikisha watu wengine na kuwa tayari kupokea utajiri unaoshuhudiwa na watu wa Mataifa!

Dhamana na wajibu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE ni kuhakikisha kwamba, kunajengeka umoja na mshikamano kati ya waamini pamoja na wachungaji wao kutoka katika nchi mbali mbali, ili hatimaye, kuweza kupata njia na wananchi wa Bara la Ulaya kuthubutu kusema tena, kuwa wao ni ”watu wa Bara la Ulaya”! Huu ni ushuhuda unaopaswa kujionesha katika tamaduni na jamii katika ujumla wake; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeonjeshwa upendo na mshikamano kwa njia ya Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake.

Kwa miaka mingi utambulisho wa Bara la Ulaya umejikita katika: upendo, sanaa na utamaduni; shuhuda hai kabisa! Hii ndiyo changamoto mpya kwa Bara la Ulaya inayopaswa kutekelezwa kwa ujasiri na umakini mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Bara la Ulaya. Kanisa linatambua kwamba, ni shuhuda na chombo cha Habari Njema ya Wokovu; mshikamano wa upendo na maskini na kwamba, Injili ni chemchemi ya utamaduni wake wa kiutu, demokrasia pamoja na haki msingi za binadamu!

Haya ni kati ya mambo msingi yanayotiliwa mkazo na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Barani Ulaya katika Tamko lao mwisho baada ya kuhitimisha mkutano wao mkuu wa mwaka uliokuwa unafanyika huko Minsk, Bielorussia kuanzia tarehe 27 Septemba hadi tarehe 1 Oktoba, 2017. Licha ya changamoto za kutaka Jumuiya ya Ulaya kutengana, Kanisa bado lina amini kwamba hatima ya maisha ya Bara la Ulaya inajikita katika umoja wa tunu msingi za maisha ya kiroho; sanjari na kuendeleza mchakato wa upatanisho na maridhiano kati ya watu; utu na heshima ya binadamu pamoja na kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene.

Tunu msingi za maisha ya kiroho, mahusiano ya mshikamano, umoja na upendo, ni mambo ambayo yamepata chimbuko lake kutoka katika Injili; kiasi kwamba, hata utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu inaweza kuonekana na kuvaliwa njuga. Bara la Ulaya limeonesha mafanikio makubwa, lakini pia mapungufu yake, hasa katika kushughulikia changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kuliko walikotoka. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika utamaduni wa ukarimu, ushirikishwaji na utawala wa sheria, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake!

Bara la Ulaya halina budi kusimama kidete kupambana na athari za ukanimungu, zinazotaka kumweka Mwenyezi Mungu nje kabisa ya vipaumbele vya mwanadamu na matokeo yake ni kushamiri kwa uchoyo na ubinafsi; uchu wa mali na madaraka; upweke hasi na hali ya kukata na kujikatia tamaa, hali ambayo inakumbatia pia kwa kiasi kikubwa utamaduni wa kifo. Maaskofu wanasema, Injili ya uhai katika hatua zake zote ni dalili ya matumaini ya jamii yenye afya bora. Ndiyo maana, Kanisa limeamua kujikita katika utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwajengea vijana uwezo katika maamuzi yao msingi, mada itakayovaliwa njuga na Mababa wa Sinodi wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayoanza kutimua vumbi mwezi, Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”.

Mababa wa Kanisa wanataka kuwaonjesha vijana upendo wa dhati unaotafsiriwa katika uwepo wao wa karibu katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya; kwa kutaka kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuwasikiliza kwa dhati pamoja na kuwasindikiza kwa unyenyekevu na upendo mkuu katika maisha yao ya ujana, kwani ujana ni mali, fainali uzeeni! Kanisa ni Mama na Mwalimu mwenye imani na matumaini kwa watoto wake, lakini anasikitishwa na yale yanayotendeka hasa kutokana na athari za utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Tabia ya uchoyo na ubinafsi, inazidi kuota mizizi kwa kasi kubwa.

Kanisa kama Mama na Mwalimu anataka kuambatana na vijana wa kizazi kipya ili kuwatangazia na kuwashuhudia Habari Njema ya Wokovu. Hii ni Injili inayofumbatwa katika maisha, upendo, uhuru wa kweli na furaha inayowawezesha vijana kumkubali Kristo Yesu, kuwa ni kiongozi wao wa maisha! Kanisa linataka kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliokata tamaa; alama ya umoja na mshikamano na wote, dira na mwelekeo unaopaswa kufuatwa pia na sera za kisiasa na kiuchumi. Familia ya Mungu Barani Ulaya haina sababu ya msingi ya kuogopa, kwani Kristo Yesu, amekwisha waambia wafuasi wake kwamba, yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahari, changamoto ni kusimama kidete ili kukumbatia Injili ya uhai, utamaduni unaosimikwa katika utu na maendeleo endelevu ya binadamu. Kanisa ni rafiki na mwandani wa watu wa Bara la Ulaya, anayetamani kutembea bega kwa bega na familia ya Mungu Barani Ulaya kama sehemu ya mchakato wa upatanisho, haki na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.