2017-10-10 07:25:00

Yaliyojiri Askofu Mkuu Giacomo Morandi alipowekwa wakfu, huko Modena


Monsinyo Giacomo Morandi aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, amewekwa wakfu kuwa Askofu mkuu kwenye Ibada iliyoadhimishwa Jimbo kuu la Modena, Kaskazini mwa Italia, tarehe 30 Septemba 2017 na tayari ameanza kutekeleza dhamana na majukumu yake katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo. Ibada hii imeongozwa na Askofu mkuu Angelo De Donatis, Makamu wa Askofu Jimbo kuu la Roma na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wakleri na familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Modena.

Askofu mkuu Nonantolai Erio Castellucci wa Jimbo kuu la Modena, amefafanua uhusiano uliopo kati ya Askofu mkuu Giacomo Morandi na mahali anapozaliwa na kwamba, sasa anatumwa kwenda kuhudumia Kanisa la Kiulimwengu kama Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Askofu mkuu Angelo De Donatis katika wosia wake, amemkumbusha Askofu mkuu Giacomo Morandi kwamba, Sekretarieti kuu ya Vatican si mahali pa uchu wa madaraka, ukiritimba au mahali pa “kupigana vijembe ili kutafuta ujiko na masilahi binafsi!” Si mahali pa wafanyakazi wa mshahara wanaotekeleza wajibu wao hata pengine bila kuguswa kutoka katika undani wa maisha yao.

Askofu mkuu Giacomo Morandi amebahatika kupenda sana Maandiko Matakatifu, kiasi cha kuwa ni chakula chake cha kila siku. Amebahatika pia kuwa ni mcheshi kati ya watu, fadhila ambazo zimemwezesha daima kuwa ni chemchemi ya furaha ya Injili kwa watu waliobahatika kukutana naye katika maisha na utume wake! Hizi ni tunu anazopaswa kuziendeleza kwa ari na moyo mkuu katika utume huu mpya wenye changamoto nyingi!

Askofu mkuu Angelo De Donatis anasema, Sekretarieti kuu ya Vatican ni Jumuiya ya waamini inayomzunguka na kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuliongoza Kanisa la Kristo katika umoja, imani na maadili na utu wema. Wao ni viongozi wa Kanisa waliopewa dhamana na madaraka ya kuwaganga watu wa Mungu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Wao wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya utakatifu wa maisha yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa watu wa Mungu, kwa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu.

Askofu mkuu Morandi daima ajitahidi kufuata nyayo za Kristo mchungaji mwema aliyejisadaka kiasi hata cha kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Awe ni mtu wa sala na mnyenyekevu; anayeshuhudia upendo wa kidugu katika maisha na utume wake, fadhila anazozimwilisha katika mahusiano na viongozi wenzake waliopewa dhamana ya kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kutekeleza wajibu wake kwa Kristo na Kanisa lake.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Giacomo Morandi, amewashukuru watu wote wa Mungu waliohudhuria katika Ibada hii ya kuwekwa wakfu kama Askofu mkuu. Amewashukuru wazazi, ndugu na jamaa pamoja na marafiki waliosaidia kumfunda katika maisha na utume wake wa kipadre na kuwa kama alivyo kwa sasa. Amewashukuru Maaskofu na viongozi mbali mbali wa Kanisa aliobahatika kufanya nao utume; vyama mbali mbali vya kitume, vilivyomjengea ari na mwamko wa kupenda kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, kiasi hata cha kujisikia kuwa na wajibu wa kuwashirikisha wengine ile furaha ya Injili inayopigiwa “debe” na Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa! Amemkumbuka kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Luis Francisco Ladaria Ferreri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, aliyepaswa kumweka wakfu, lakini ikashindikana kutokana na sababu ya ugonjwa! Huyu alikuwa ni Jaalimu wake wa Maandiko Matakatifu, aliyemfundisha kulipenda Neno la Mungu, dira na mwongozo katika maisha na utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.