2017-10-07 16:27:00

Walezi wakuu wa miito: Mungu, Mapadre, Maaskofu na Familia ya Mungu


Malezi na majiundo ya kipadre kwanza kabisa ni kazi ya Mwenyezi Mungu ambayo inamtaka jandokasisi kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumfunda kadiri anavyotaka! Pili, Kasisi mwenyewe anapaswa kutambua kwamba, ni mhusika mkuu wa majiundo katika wito, maisha na utume wake wa kipadre. Tatu, wadau wakuu wa malezi ni walezi waliopewa dhamana kwa kusaidiana na Maaskofu, kwa kutambua kwamba, wito unazaliwa, unakua na kukomaa ndani ya Kanisa.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 7 Oktoba 2017 alipokutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la Kimataifa juu ya Mwongozo wa Malezi ya Kipadre “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre”, wakati wa kuhitimisha Kongamano hili, lililofunguliwa, Alhamisi, tarehe 5 Oktoba 2017 huko Castel Gandolfo. Baba Mtakatifu anasema, malezi ya kipadre kwanza kabisa ni jukumu la Mwenyezi Mungu na kwamba, tema ya majiundo awali na endelevu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika upyaisho wa imani sanjari na maboresho ya miito kwa siku za usoni, jambo linalowezekana ikiwa kama Kanisa litakuwa na Mapadre waliofundwa wakafundika barabara.

Hii ni changamoto kwa majandokasisi kumwachia nafasi Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaunda na kuwafunda kama chombo cha udongo mikononi mwake, kadiri ya upendo wenye huruma. Mwenyezi Mungu anajitahidi kulinda na kutunza kazi ya mikono yake. Majiundo makini si mchakato wa maboresho ya kitamaduni, bali ni sanaa inayofanywa na Mwenyezi Mungu katika hali ya utulivu na huruma na kwamba, hii ni dhamana inayodumu katika maisha yote. Mapadre wanakumbushwa kwamba wito wao ni hazina kubwa inayotunzwa katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu na wala si kutoka kwa mapadre wenyewe!

Mapadre wajenge tabia ya kujinyenyekesha mbele ya Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaunda na kuwafunda, vinginevyo, wakuwa mapadre waliozimika kama “Kibatari”, hali ambayo itawapelekea kutekeleza utume wao kwa mazoea pasi na ari wala mwamko; pasi na upendo kwa Injili na watu wa Mungu. Kwa mapadre wanaojiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu ili aweze kuwafunda kila siku ya maisha yao wanakuwa ni chachu mpya ya Injili na kila wanapohubiri, Neno la Mungu linazama na kukita mizizi yake kwenye sakafu ya roho za waamini. Hawa ni mapadre ambao mikono yao imepakwa mafuta matakatifu kwa ajili ya kuganga na kuponya madonda ya waamini wao na hatimaye, kuzima kiu ya matumaini ya watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mapadre ni wahusika wakuu katika malezi na majiundo yao ya awali na endelevu, kumbe, wanapaswa kushirikiana kikamilifu na neema ya Mungu katika maisha yao daima wakiwa na nia ambayo ilikuwamo ndani ya Kristo Yesu, kwa kuwa wazi na kujiendelea kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu kama Mitume waaminifu. Ili jandokasisi au padre aweze kuwa mhusika mkuu katika malezi na majiundo yake, hana budi kuwa na utashi thabiti wa kusema “Ndiyo” au “Hapana” badala ya kutafuta “ujiko” usiokuwa na mvuto wa mashiko! Sala na ukimya ni mambo msingi katika malezi na majiundo ya kipadre sanjari na kujikita katika kipaji cha ubunifu kinachompatia Kasisi wa Mungu nafasi ya kujiachilia katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kutumia karama na mapaji kwa ajili kuwashirikisha watu wa Mungu furaha ya kukutana na Mwenyezi Mungu na ndugu zake katika Kristo!

Mapadre wajenge na kudumisha umoja, udugu na urafiki katika maisha na utume wao na watu wanaowahudumia, kwani wito wao ni matunda ya wao kukutana na Mwenyezi Mungu, Kristo Yesu na watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kwamba, wahusika wengine katika malezi na majiundo ya kipadre ni walezi na Maaskofu, kwani wito unazaliwa, unakuwa na kukomaa ndani ya Kanisa. Hawa ni ndio magombera, mapadre wa maisha ya kiroho, walezi na waalimu pamoja na wale wote waliopewa dhamana ya malezi endelevu ya mapadre. Wote hawa wanapaswa kushirikiana na neema ya Mungu ili kuliwezesha Kanisa kupata Mapadre waliofundwa na kufundika barabara!

Dhamana hii inahitaji uwepo wa karibu wa walezi na Maaskofu; kwa kuwajibika kikamilifu katika maisha na wito wa kipadre! Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kushirikiana kwa karibu sana na Maaskofu wenzao katika kukuza na kudumisha miito mitakatifu; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano na mapadre wao; sera na mikakati makini ya malezi na majiundo ya kipadre kijimbo bila kusahau kuwaandaa walezi katika maisha na utume wa kipadre. Kanisa linahitaji mapadre ambao wana uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa ari na moyo mkuu; kwa hekima na busara, ili kuwasha moto wa matumaini, pale mahali ambapo waamini wamekata tamaa, ili kupyaisha imani katika majangwa na nyoyo za watu!

Baba Mtakatifu mwishoni anasema, hata watu wa Mungu wanayo dhamana nyeti katika malezi na makuzi ya wito na maisha ya mapadre! Ni wajibu wa makasisi kuhakikisha kwamba, wanazima kiu na matamanio halali ya watu wa Mungu, wanaosaidia pia kuleta mabadiliko katika maisha. Licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza, lakini makasisi wanapotembea kati ya watu wa Mungu wanaweza kuonja wema na upendo wao! Hii ndiyo shule makini ya kiutu, maisha ya kiroho, kiakili na kichungaji. Padre anapaswa kuwa kati ya Kristo Yesu na watu wa Mungu, kwa njia ya sala na tafakari ya kina; kwa unyofu na upole wa moyo; kwa kujitoa na kujisadaka; kwa kubariki na kuwafariji wale wote anaokutana nao katika hija ya maisha yake.

Padre anafundwa kwa kuyakimbia malimwengu; kwa kutokubali kuzamishwa kwenye tasaufi tupu isiyokuwa na Mungu ndani mwake. Katika majiundo na malezi ya kipadre, kila mtu ajiulize swali na msingi! Je, anatakuwa Padre wa aina gani? Padre anayeketi masaa 24 sebuleni akiwa “anaangalia TV na kutafuna karanga” au Padre ambaye ni mtume mmisionari anayechakarika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake na kwa ajili ya  ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu; Au Padre anayeamsha dhamiri za waamini ili waweze kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao? Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amemwomba Bikira Maria wa Rozari Takatifu anayekumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 7 Oktoba, awasaidie mapadre kutembea kwa furaha katika huduma ya kitume, huku wakionesha moyo wa unyenyekevu na upole kama udongo wa mfinyanzi kwenye mikono ya muunzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.