2017-10-07 16:59:00

Tamko la Roma: Ulinzi wa utu na heshima ya watoto wadogo!


Wajumbe wa Kongamano la Kimataifa kuhusu ulinzi wa watoto wadogo kwenye “ulimwengu wa digitali”, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Utu wa watoto wadogo katika ulimwengu wa digitali”, Ijumaa, tarehe 6 Oktoba 2017 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kumpatia “Tamko la Roma” kuhusu ulinzi wa watoto wadogo kwenye “ulimwengu wa digitali”. Baba Mtakatifu amewataka wajumbe hawa kuwa makini ili watu wasitumbukie katika mawazo potofu ya kudharau madhara ya nyanyaso za kijinsia wanayofanyiwa  watoto wadogo na kuona kuwa ni jambo la kawaida. Pili, suluhu ya matatizo na changamoto hii si ya kiufundi na inayokuja tu kama “maji kwa glasi” kwani hili ni tatizo changamani. Tatu, ni tatizo linaloweza kuwatumbukiza watu katika mtazamo wa kisiasa zaidi kwa kujikita katika uhuru usiokuwa na mipaka unao athiri ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Tamko la Roma linasema maisha ya kila mtoto ni ya pekee, ni muhimu na yana thamani kubwa na kwamba, kila mtoto anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake pamoja na kupewa ulinzi na usalama. Lakini, leo hii kuna mamilioni ya watoto ambao hawana ulinzi na usalama. Maendeleo makubwa ya teknolojia na matumizi yake katika maisha ya kila siku yanaendelea kuleta mabadiliko makubwa si tu kwa kile ambacho watu wanatenda, bali hata katika utambulisho wao na kwamba, hii ni baraka kubwa. Lakini, kwa upande mwingine, maendeleo haya yameibua giza linalofumbatwa katika bahari ya mitandao ya kijamii ambayo inaacha madhara makubwa kwa ustawi na makuzi ya watoto wadogo.

Mintandao ya kijamii ina manufaa makubwa kwa jamii na ni fursa inayowashirikisha watu ndani ya jamii na kwamba, inatoa nafasi pia kwa watu kujipatia ufahamu wa mambo mbali mbali. Mitandao hii imesababisha kumong’onyoka kwa utu wa binadamu kutokana na madhara yake kwa watoto. Kumekuwepo na ukatili dhidi ya watoto wadogo; nyanyaso za kijinsia na mielekeo tenge ya tendo la ndoa; mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kuwa ni ya kawaida hata kwa watoto. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo katika mitandao ni tatizo linalotisha sana! Kuna idadi kubwa za picha za ngono walizopigwa watoto na vijana na zimesambazwa kwenye mitandao ya kijami na zinaendelea kuongezeka maradufu. Picha za ngono zina athari kubwa katika akili na makuzi ya watoto wadogo.

Wajumbe wanasema kwamba, wanaunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa ya kutaka kuhakikisha kwamba, matumizi ya mitandao ya kijamii yanawafikia watu wengi zaidi lakini kwa kuzingatia umuhimu wa kuwalinda watoto wote, changamoto kubwa inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali, ili kweli mitandao ya kijamii iweze kutoa huduma inayowawajibisha wote. Watoto wawe na fursa ya kutembelea mitandao ya kijamii wakiwa na uhakika wa usalama wao, unaofumbatwa katika elimu na malezi makini; mawasiliano pamoja na mahusiano yao. Wadau mbali mbali katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano wanayo dhamana na wajibu  mkuu wa kuongoza vita ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ulinzi na usalama wa watoto kwenye mitandao.

Wajumbe wanazihimiza familia, majirani na jumuiya kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na watoto wenyewe kutambua madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. Wanawapongeza viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa ambao wanaendelea kujizatiti kila kukicha, ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo na ulinzi na usalama wa watoto wanaotumia mitandao ya kijamii. Kuna vituo ambavyo vimeanzishwa kwa ajili ya ulinzi na usalama wa utu na heshima ya watoto mitandaoni, kwa namna ya pekee: Kituo cha Ulinzi kwa Watoto Wadogo cha Chuo Kikuu cha Kipapa la Gregorian, kinachoendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya kutoa ulinzi kwa watoto wadogo katika nchi 30 duniani.

Kituo cha “WePROTECT Global Alliance”, kilichoanzishwa huko nchini Uingereza kwa ushirikiano kati ya Jumuiya ya Ulaya na Serikali ya Marekani; kinaunganisha nchi 70 na Makampuni 23 ya teknolojia ya mawasiliano kimataifa. Tamko linatambua juhudi za Umoja wa Mataifa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ifikapo mwaka 2030 ili kuhakikisha kwamba ukatili dhidi ya watoto wadogo zinafutwa , kwa kushirikiana na Taasisi Inayopania Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto. Utu na heshima ya watoto wadogo ni changamoto ya kimataifa inayopaswa kushughulikiwa kimataifa; kwa kuwajumuisha wadau mbali mbali.

Tamko linawataka viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha kampeni ya kuragibisha na kuelimisha walimwengu umuhimu wa kulinda utu wa watoto na madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi yao na kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kuchukua hatua makini. Viongozi wakuu wa dini mbali mbali wajitahidi kuunganisha nguvu ili kulinda ulimwengu wa watoto. Wabunge na watunga sera na sheria watambue madhara yanayofanywa na wahalifu dhidi ya utu na heshima ya watoto kupitia mitandao ya kijamii.

Viongozi wa makampuni ya teknolojia ya mawasiliano wajitahidi kutengeneza vyombo na teknolojia itakayopambana na nyanyaso za kijinsi dhidi ya watoto wadogo kwa kuwatambua kuwa wao ni wahanga! Wadau katika sekta ya afya ya jamii, wajitahidi kuibua mbinu mkakati na programu za tiba kwa wahanga wa nyanyaso za kijinsia. Vyombo vya ulinzi na usalama, viwatambue waathirika na kuwasaidia katika maisha yao. Vishirikiane katika kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha wahalifu wa mitandao ya kijamii mbele ya vyombo vya sheria. Kuna haja ya kuimbua mbinu mkakati wa majiundo ya kitaaluma yatakayowawezesha wataalam wa afya kutambua dalili za nyanyaso za kijinsi; ili kuweza kutoa tiba na uponyaji wa ndani kwa watoto hawa.

Wajumbe wanazitaka taasisi binafsi na zile za kiserikali katika sekta ya elimu, kuwekeza zaidi rasilimali katika tafiti za kisaikolojia na fani nyingine za malezi na makuzi ya watoto wadogo, ili kusaidia kupata tiba kwa watoto ambao wameathirika kutokana na nyanyaso za kijinsia. Viongozi na taasisi za kimataifa zishirikiane na kushikamana ili kutengeneza teknolojia itakayowazuia watoto na vijana kupata mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii! Ruhusa hii itolewe kwa watu wazima peke yao. Wadau mbali mbali washirikiane kuanzisha kampeni za kimataifa zinazowalenga watoto na vijana katika malezi na makuzi yao; kwa kuwapatia vyombo ambayo watavitumia kwa kuwajibika wakati wanapoogelea kwenye mitandao ya kijamii, ili wasiwadhuru hata jirani zao pia. Jumuiya ya Kimataifa ijitaabishe kuwahamasisha watu kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia, ili kuyazuia, kabla hayajawafikia wahusika na kuyatibu kwa wale walioathirika.

Mwishoni, wajumbe wanamalizia kwa kusema, katika ulimwengu wa maendeleo ya  mitandao ya kijamii, dunia inakabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kutokea, ili kujizatiti kikamilifu katika kulinda na kudumisha haki, utu na heshima ya watoto wadogo; kuna haja ya kushikamana kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Hapa kuna haja ya kuwa na mielekeo mipya ya kupambana na changamoto hizi, kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa kiulimwengu pamoja na viongozi wanaotaka kupambana kikamilifu dhidi ya nyanyaso hizi. Tamko la Roma linatolewa kwa ajili ya watu wote wa Mataifa, ili wote waweze kushikamana kulinda utu wa watoto wadogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.