2017-10-06 07:53:00

Wandugu zalisheni mazao yenye viwango na tija! Vinginevyo...!


Wakati fulani tunasikia Rais wa nchi anakutana Ikulu na wasanii, au wanamichezo, wazee wa kaya, viongozi wa dini, ili kuongea na kuwapa ujumbe fulani muhimu kwa manufaa yao na ya taifa kijumla. Katika fasuli ya Injili ya leo Yesu anakutana na wakuu wa makuhani yaani viongozi wa dini kama vile mafarisayo, wataalamu wa Maandiko matakatifu; pamoja na wazee wa watu yaani viongozi wa serikali kwa ujumla wao.  Kwa vyovyote kuna ujumbe mahususi anataka kuwapa kama anavyoanza: “Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa makuhani: Sikilizeni mfano mwingine.” Hapa ni dhahiri kabisa mfano huu unao ujumbe mzito unaowalenga. Hebu tumfuatilie Yesu ili kuuelewa ujumbe ulio katika mfano wake.

Mfano unaanza hivi: “Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, alipanda shamba la mizabibu.” Yesu anatuingiza katika mazingira ya kiuchumi na kijamii ya wakati wake. Mazingira aliyokulia Yesu huko Nazareti kulikuwa na nyanda za kilimo cha ngano na mizabibu. Leo anatuletea mfano wa mwekezaji wa kilimo cha zabibu. Yasemekana kwamba wawekezaji hao walikuwa na mashamba makubwa ya zabibu na waliweka wafanyakazi kuliendesha shamba hilo. Kuhusu zabibu, Waisraeli wanaposikia tu unatamkwa mradi huo, mara moja waliuhusisha na wao wenyewe. Kwa sababu manabii waliwafundisha kuwa wao ni mzabibu wa Bwana. Yaani Mungu ndiye mwenye nyumba au mwekezaji mkuu, aliyelima na kuutunza mzabibu wake  – Taifa la Waisraeli – kwa uangalifu mkubwa na alisubiri lizae zabibu nzuri ili akamue divai. Kama asemavyo Isaya katika wimbo wa shamba la mizabibu: “Mpendwa wangu alikuwa na mizabibu aliyopanda kwenye shamba alilolitayarisha vizuri.” (Isaya 5). Kadhalika mzaburi anasema: “Bwana alienda kuchukua mche wa mzabibu huko Misri. Halafu akatayarisha ardhi (shamba) ili kupanda, akafukia vizuri mizizi yake. Halafu mzabibu huko ukaona na kuchanua vizuri na kueneza matawi yake hadi kwenye maziwa makubwa, na vimelea vingine vikaenea hadi mto Eufrates.” (Zab. 80) Kumbe sasa taifa jipya la Waisraeli ni jumuia ya Kikristu aliyoanzisha Yesu.

Kisha mwekezaji “akalizungusha ugo shamba la mizabibu.” Ugo ni kinga ya shamba dhidi ya wanyama mwitu na wevi. Mungu pia alililinda taifa lake kwa ngao ya neno lake, ambayo ni Tora ili lisiathirike na upagani wa mataifa.Halafu mwekezaji: “akachimba shimo la shinikizo ndani yake.” Mahali pakukamulia zabibu ili kutengeneza divai. Mungu anawatakia watu wake furaha na shangwe kama ya mtu aliyekunywa divai. Tena mwekezaji: “alijenga mnara.” Mnara huo tungeulinganisha na ngokwe (ghala) au lindo. Waisraeli walitengeneza ngokwe ndani ya shamba la zabibu na juu yake kulikuwa na kijichumba cha kulinda zabibu. Mnara huo ni alama ya ulinzi anaoufanya Mungu kama mama anavyomlinda mtoto wake. Hatimaye mwekezaji: “akapangisha shamba hili kwa wakulima na akaenda zake.” Baada ya kupangisha, wawekezaji walirudi kukaa kwenye miji mikubwa ya utawala wa kirumi kama vile Roma, Aleksandria, Antiokia, Efeso na kusubiri mavuno anayokidhi kiwango cha kukamua divai bora. Hadi hapa sasa wasikilizaji walitegemea kusikia Yesu anasema kuwa zabibu zimezaa vya kutosha na Mungu anayafurahia matunda ambayo taifa lake linamtolea kama tunavyosoma kwamba: “Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, mwenye nyumba akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake.”

Kumbe Yesu anaendelea kivyake kabisa kusimulia mfano anaposema: “Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe….” Ili kuupata vizuri ujumbe wa maneno haya budi kujiuliza: “Kulikoni wakulima wanawakamata watumwa wale wanawapiga na kuwaua?” Je, hawakuwa wamepata mavuno ya kutosha? La hasha, wale wakulima walikuwa wamefanya kazi nzuri kabisa na walipata mavuno mengi tu. Kisha wakayakabidhi mavuno hayo yote kwa watumwa.  Sasa yaonekana mavuno yale hayakukidhi kiwango kilichotakiwa. Hivi watumwa hawakuwa tayari kuchukua mavuno yale na kumpelekea mwekezaji kwani naye asingeyapokea kwa sababu yalikosa kiwango.

Hapa Yesu alitaka kusema kwamba Mungu mwekezaji mkuu alishawatuma watumwa wake yaani manabii, kwa Waisraeli yaani wakulima. Walipofika wakakabidhiwa zabibu (taifa lake), lakini wakaona matunda hayakidhi kiwango anachokipenda Mungu. Mathalani, pale Mungu kwa kinywa cha nabii Isaya anakemea kazi ya wakulima (wakuu wa makuhani na wazee wa watu) anasema: “Mnapofukiza ubani wa sadaka zetu mimi ninageukia upande mwingine, kwani moshi wake unanuka. Mnapopiga zumari wakati wa ibada mimi ninaziba masikio yangu.” Kumbe matunda anayoyategemea Mungu ni “kutenda mema, kuwa watu wa haki, kuwatunza yatima, na wanaoonewa, kuwatendea haki wajane.” Aidha nabii anasema: “Bwana alikuwa anategemea haki kumbe anaona umwagaji damu. Alitegemea huruma na upendo, kumbe anasikia malalamiko na vilio vya ugandamizaji.” (Isaya 5). Kadhalika nabii Yeremia anakemea vikali sana namna makuhani walivyoendesha madhehebu hekaluni: “Ninyi mnadhani mnatolea sadaka nzuri na mnadhani mpo hakika na mnachofanya, kumbe mnaharibu kila kitu.” Mapato yake manabii hao walichukiwa sana: mathalani, nabii Uria aliuawa kwa upanga. Yeremia alitumbukizwa kwenye handaki la matope. Zakaria mwana wa Barakia alitekwa akiwa madhabahuni.

Hapa unakuta alama za nabii wa kweli: Mosi, hatafuti masilahi binafsi bali daima yeye anatangaza fikra za Mungu. Hata katika mfumo wa maisha ya kanisa tunaweza kufikiri kwamba tuko sawa katika kutenda mambo, katika kuabudu. Kisha anafika nabii anayesema kwamba mambo siyo hivyo, na anaongea si kwa ajili ya masilahi binafsi bali anataka kanisa lililo katika mstari mzuri unaoakisi thamani na vigezo vya kiinjili. Pili nabii wa kweli anatenda kama mtumwa au mtumishi wa Injili, yaani, anatangaza huruma na upendo alioleta Kristu.

Tatu, nabii wa kweli ni yule anayelipa nafsi yake, yaani  haogopi kuhatarisha maisha yake kwa vile anatambua kuwa  anatangaza Neno la Bwana. Mfano unaendelea kumwonesha Mwekezaji akitupa kete ya mwisho: “Mwishoni akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu…. Huyo wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu wakamwua.” Ama kweli hapa mwekezaji huyu anatofautiana kabisa na wawekezaji wengine wote. Tungekuwa sisi, tusingemtuma mwana kirahisi hivi tena mikono mitupu bila ulinzi. Kumbe huyu anamtuma mwanae bila kinga yeyote tena kwa wakulima walewale waliowapiga na kuwaua watumwa wake. Mwekezaji huyu ambaye ni Bwana wa nyumba siyo mwingine bali ni Mungu Mwenyezi. Anamtuma Mwanae kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Lengo kubwa lilikuwa kuwaonesha wale wakulima, zabibu zinazokidhi kiwango anachokitegemea kutoka kwao. Mungu anataka matunda ya upendo kutoka kwa wakulima wake. Kwa vyovyote pendo halidaiwi kwa mabavu, bali kwa mfano wa maisha. Hili ndilo fundisho na shule ya Mungu tunayopata leo.

Leo tunapozungumzia mzabibu wa Bwana tunawamaanisha Wakristu na wasikilizaji wake wote hususani viongozi wa kanisa na wa serikali. Hao wanaweza kumfukuza Mwana (Kristu) nje ya shamba la zabibu (wakristu) na kudai kuongoza na kufanya kazi kadiri ya vigezo vyao. Kadhalika Mwana anaweza kufukuzwa katika jumuia ya kikristu kutokana na aina ya mazungumzo na maamuzi ya wakristu wanaoishi kama wapagani. Mathalani Wakristu wanaobana wake wawili wawili wanaweza kupata kigagasi kuzungumzia maisha ya ndoa. Huko ni kumfukuza Mwana kutoka kwenye shamba la mzabibu. Hata katika jamii zetu tunaweza kufukuza chachu ya kiinjili na kumtupilia mbali Mungu na hata kusema kuwa “Mungu amekufa” na mapato ya kumwua Mungu katika jamii zetu tunayaona yaani vita, vitisho, balaa, upweke, kukosa maana ya maisha.

Mfano unatamatika kwa swali ambalo Yesu anawauliza wasikilizaji wake: “Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima?” Swali hili linawahusu wale wote walio katika jumuia ya kikristu wanaoifukuza Injili. Nadhani ukiulizwa  wewe ungejibu kama wanavyojibu wakuu hawa wa makuhani na wazee wa watu kwamba: “Bwana wa nyumba atawaadhibu vikali sana wale wadhalimu. Yaani, watalaaniwa hao na kwa vyovyote watatupwa motoni.” Mawazo haya ni ya laana. Kumbe mawazo na fikra za Yesu ni tofauti. Yesu anatangaza habari njema siyo laana. Hebu angalia anachosema: “Yesu akawaambia, hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni.”  Hapa ndipo palipolala uhondo. Badala ya kulaani na kuwakufuzia mbali wakulima wale kama vile tofali lisilofaa linavyotupwa na mjenzi, sasa jiwe hilo linatumika kikamilifu tena linakuwa ni msingi wa jengo jipya na linaanzisha ulimwengu mpya wa kutenda mambo. Hapa Yesu anatangaza maajabu machoni petu, kwamba uovu mkubwa alioufanya binadamu, Mungu ameugeuza, ameubadilisha na kuwa kazi bora ya upendo na ukombozi. Yaani yule Mwanakondoo aliyetupwa kati ya kundi la mbwa mwitu, sasa ameanzisha utawala mpya na ulimwengu mpya ambao siyo tena ule wa wanyama bali wa upendo kati ya watu. Ama kweli “Neno hili limetoka kwa Bwana nalo ni ajabu machoni yetu?” Hitimisho hili linabeba maneno ya matumaini makubwa.

Aidha kuhusu Jiwe hili, kama mtu atajikwaa nalo huyo ataumia mwenyewe. Aidha kama linakuangukia litakuponda. Picha hii ina maana kwamba pale fikra za ulimwengu na filosofia yake itakapopambana na fikra za kiinjili hizo filosofia zitaonekana kuwa si za utu. Injili peke yake itaendelea kumwangaza binadamu juu ya ukweli halisi wa utu wa binadamu katika maisha. Aidha popote inapoingia Injili (litakapoangukia jiwe) kila aina ya kukosa utu itanyauka. Kwa hiyo hilo si tangazo la vitisho bali ni la matumaini na la furaha kuu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.