2017-10-06 06:57:00

Papa Francisko: Wakristo ni wahudumu wa Neno!


Wakristo wanapaswa kutambua kwamba wao ni wahudumu wa Neno la wokovu; uzima wa milele, upatanisho na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Wakristo ni wahudumu wa ukweli na nguvu ya Neno la Mungu, wanaopaswa kujenga umoja na kushikamana kidugu katika maisha na sala! Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 5 Oktoba 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Shirikisho la Vyama vya Biblia KImataifa, kinachoendelea kujizatiti kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, Injili inafahamika kwa wengi, kwa kuchapisha Biblia katika lugha mbali mbali pamoja na kuzisambaza katika mifumo mbali mbali ya mawasiliano ya kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko akifafanua kuhusu  dhana ya Wakristo kuwa ni wahudumu wa Neno la Wokovu, anawataka waamini kujitahidi kuguswa na Neno la Mungu katika undani wa mioyo yao kwa kutambua kwamba, Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote, ukatao kuwili; tena lachoma na kuzigawanya nafsi na roho. (Rej. Heb. 4:21.).  Wakristo ni wahudumu wa Neno la uzima kwani mtu haishi kwa mkate peke yake, bali kwa kila Neno litokalo katika kinywa cha Bwana. Kumbe, ni wajibu wa Wakristo kuhakikisha kwamba, kwa njia ya msaada wa Roho Mtakatifu wanarutubisha maisha yao: kwa kusoma, kulitafakari na kulishuhudia Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha; kwa kujikita katika upendo wa Mungu anayetamani kuzungumza na waja wake na kuwakirimia Neno la uzima wa milele!

Baba Mtakatifu anawakumbusha Wakristo kwamba, wao ni wahudumu wa Neno la Upatanisho, kwa kuheshimu na kuthamini Neno hili katika maisha, kwani kimsingi wao ni wahudumu pia wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, changamoto kwa Mama Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya wokovu pasi na woga, bila kuchelewa, kwa kutekeleza amri ya Kristo inayowatuma kama wamisionari kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Wakristo wanafahamishwa kuwa wao ni wahudumu wa Neno la Ukweli, chemchemi ya umoja na ufunuo wa Imani na kwamba, wanahamasishwa kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima, aliyewapatanisha wote kwa kusimamia ukweli!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, Wakristo ni wahudumu wa nguvu ya Neno la Mungu linaloangaza; linalolinda, linaloganga na kuponya pamoja na kumweka mtu huru! Neno la Mungu linapaswa kupewa uzito wake kwani kuna Wakristo ambao wametupwa gerezani kutokana na ushuhuda wao kwa Neno la Mungu na kwamba, kuna Wakristo wengi ambao wameyamimina maisha yao kama ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa njia hii, Wakristo wanapaswa kutembea kwa pamoja, huku wakiwa wameshikamana katika udugu na sala, ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kutimiza mapenzi yake! Wakristo wanao wajibu wa kuombeana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.