2017-10-06 15:48:00

Papa Francisko: Mbinu mkakati wa kulinda utu wa watoto mitandaoni!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 6 Oktoba 2017 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Kongamano la Kimataifa kuhusu ulinzi wa watoto wadogo kwenye ulimwengu wa digitali” lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Utu wa watoto wadogo katika ulimwengu wa digitali”. Baba Mtakatifu amewataka wajumbe hawa ambao wamempatia Tamko la Roma kuhusu ulinzi wa watoto wadogo kwenye ulimwengu wa digitali” kuwa makini ili watu wasitumbukie katika mawazo potofu yafuatayo: kudharau madhara ya nyanyaso za kijinsia wanayofanyiwa  watoto wadogo na kuona kuwa ni jambo la kawaida.

Pili, suluhu ya matatizo na changamoto hii si ya kiufundi na inayokuja tu kama maji kwa glasi kwani hili ni tatizo changamani. Tatu, ni tatizo linaloweza kuwatumbukiza watu katika mtazamo wa kisiasa zaidi kwa kujikita katika uhuru usiokuwa na mipaka unao athiri ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kusikiliza shuhuda mbali mbali zilizotolewa na waathirika wa ulimwengu wa digitali na kwamba, hili ni tatizo ambalo halijapembuliwa kwa kina na mapana kwa ushirikiano wa taasisi mbali mbali ili kulinda na kudumisha utu wa watoto wadogo katika ulimwengu wa digitali.

Ikumbukwe kwamba, ulinzi wa utu na heshima ya binadamu ni dhamana na wajibu wa kisiasa na kijamii na Kanisa linatambua haki hizi msingi katika maisha na utume wake; kama ilivyo kwa “Tamko la Haki ya Mtoto la Mwaka 1959” na kama haki hizi zinavyofafanuliwa kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwawezesha watoto kukua na kukomaa katika mazingira salama katika maisha na utu wao. Hawa ni watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Yesu. Unyenyekevu wa watoto ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wanaotaka kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini, Yesu anaonya kwamba, Ole wake atakayemkwaza mtoto mdogo, itabidi afungiwe jiwe la kusagia shingoni na kuzamishwa baharini!

Baba Mtakatifu anasema, leo hii binadamu anaishi katika ulimwengu wa digitali “Digital World”, matunda ya sayansi na maendeleo ya teknolojia ambayo yameleta mageuzi makubwa katika mchakato wa maisha na mawasiliano ya jamii; namna ya kufikiri na kutenda; kwa kujikita katika matarajio na utambulisho wa mtu! Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anakabiliwa na changamoto katika medani mbali mbali za maisha: kimazingira, kiuchumi, kisiasa, kimaadili na hata katika maisha ya kiroho. Changamoto pevu kwa wakati huu ni ulinzi wa utu na heshima ya watoto na vijana; ukuaji wao makini na salama; furaha na matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kuna mamilioni ya watoto wanaotumia mitandao ya kijamii kuwasiliana na huko wanakumbana mambo mbali mbali katika maisha yao kiasi hata cha picha chafu na biashara ya ngono pamoja na  ukatili wa kijinsia mambo yanayoleta athari kubwa kimaadili na katika akili ya watoto hawa! Huko watoto wanakutana na magenge ya kihalifu kimataifa, ukahaba na biashara ya ngono kwenye mitandao inayochukua nafasi kubwa katika mchakato wa usambazaji, ikilinganishwa na njia za zamani za mawasiliano ya jamii, yaani magazeti na majarida ya picha za ngono! Haya ni mambo ambayo yamepembuliwa kwa kina na mapana katika kongamano hili kwa kukazia ukweli na uwazi.

Tabia ya mitandao ya kijamii anasema Baba Mtakatifu ni kujipenyeza zaidi katika ulimwengu wa utandawazi ili kuwafikia watu wengi zaidi. Changamoto hii, kamwe haiwezi kushughulikiwa na kikundi cha watu wachache peke yao bali ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa. Hapa kuna makundi ya kihalifu kimataifa, kuna wafanyabishara haramu na ugaidi wa kimataifa unaotafuta fedha kwa udi na uvumba. Matokeo yake ni malezi na majiundo ya vijana wa kizazi kipya kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha; hali ambayo inakwamisha pia majadiliano kati ya wazazi, walezi na watu pamoja na ulimwengu wa vijana, kiasi hata cha kushindwa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu!

Lakini, jambo la msingi hapa anasema Baba Mtakatifu ni kuondokana na woga na wasi wasi usiokuwa na mshiko wala mvuto! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuunganisha nguvu na rasilimali zake ili kuibua majibu muafaka, kwa kuwa na imani ya kutumia vyema uhuru wa binadamu ili kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa kukaelekeza teknolojia hii, ili kusaidia maendeleo endelevu ya binadamu; kwa kuwa salama, ili kukazia utu na mshikamano wa kijamii.  

Baba Mtakatifu anawataka watu kuwa makini na ulimwengu wa digitali ili wasitumbukie katika mawazo potofu kwanza kabisa kwa: kudharau madhara ya nyanyaso za kijinsia wanayofanyiwa  watoto wadogo na kuona kuwa ni jambo la kawaida.  La hasha watoto wanaathirika vibaya sana katika maisha yao kiasi cha kuwafanya watoto hata na watu wazima kuwa wategemezi kiasi cha kutoweza kuwa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii; watu hawa wanajenga upendo usio wa dhati na matokeo yake ni mahusiano tenge. Kumbe, hapa kuna haja ya kushirikiana katika kupambana na nyanyaso hizi katika mitandao ya kijamii.

Pili, suluhu ya matatizo na changamoto hii si ya kiufundi na wala si rahisi hivi kama wanavyofikiria watu wengi kwa: kutambua, kuzuia na kudhibiti usambazaji wake. Lakini ikumbukwe kwamba, kuna wawekezaji wanaotumia rasilimali watu na fedha; rasilimali vitu na teknolojia ili kuwekeza katika mitandao ya kijamii na wanabahatika kupata faida kubwa kwa muda mfupi! Kumbe, hata katika mchakato wa maendeleo na teknolojia kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kanuni maadili na utu wema vinatawala kwenye mitandao ya kijamii.

Tatu, ni tatizo linaloweza kuwatumbukiza watu katika mtazamo wa kisiasa zaidi kwa kujikita katika uhuru usiokuwa na mipaka unao athiri ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mitandao ya kijamii ni mahali pa watu kujieleza kwa uhhuru pasi na mipaka, lakini pia ustawi, mafao na maendeleo ya wengi hayana budi kulindwa kisheria, ili kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Hapa kinachotiliwa mkazo si uhuru wa mtu kujieleza, bali hapa kuna uvunjifu wa sheria na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Wahusika wanapaswa kushughulikiwa kwa weledi na akili kubwa; kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi mbali mbali kushirikiana kwa dhati, ili kukabiliana na changamoto ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu anawataka watu kutambua ukubwa wa madhara ya nyanyaso za utu na heshima ya watoto kwenye ulimwengu wa digitali, ili hatimaye, kuibua sheria, kanuni na mbinu muafaka za kupambana na uhalifu huu kwa wahusika kufikishwa mbele ya sheria; watoto kupatia huduma makini ya kuweza kurekebisha hali yao; walimu na walezi kujengewa uwezo mkubwa katika kupambana na nyanyaso za utu na heshima ya watoto kwenye mitandao, lakini wao wenyewe wawe pia ni watumizi wema wa mitandao ya kijamii. Kuna haja ya kuendelea kuragibisha kanuni maadili na utu wema pamoja na tafiti za kisayansi zinazoendana na changamoto hii.

Ni Matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kutakuwepo na ushirikiano mkubwa na viongozi wa kidini na waamini katika ujumla wao, ili kuweka kwa pamoja uzoefu, ujuzi na maarifa yao ya malezi ya kimaadili na maisha ya kiroho ili kupambana na vitendo hivi viovu. Kanisa Katoliki, litaendelea kutoa ushirikiano wa dhati ili kupambana na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Kanisa litaendeleza mchakato wa kujisafisha na hatimaye, kujizatiti katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya watoto wadogo.

Kanisa linataka pia kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kukomesha nyanyaso, biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake; vita na ghasia; mambo yanayofafanuliwa kwa kina na mapana na Umoja wa Mataifa katika Mikakati ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameshuhudia mateso na mahangaiko ya watoto hawa sehemu mbali mbali za dunia, changomoto na mwaliko kwa kuwawezesha tena watoto kuwa na furaha, amani na utulivu wa ndani kwa kuwajengea mazingira bora ya malezi na makuzi. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuunganisha nguvu kwa kujikita katika: haki, ujasiri na furaha ya kuwaangalia watoto machoni pao pasi ya kuona aibu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.