2017-10-06 06:17:00

Papa Francisko: Imarisheni upatanisho wa kitaifa ili kujenga Iraq


Mababa wa Sinodi ya Kanisa la Caldea wanao wajibu na dhamana ya kukabiliana na changamoto ya uhamiaji wa nguvu dhidi ya Wakristo, ujenzi wa vijiji vilivyobomolewa wakati wa ghasia na vita; huduma kwa watu wasiokuwa na makazi wanaotamani kurejea makwao ili kuendelea na maisha; haki za Kanisa mahalia, Liturujia Takatifu na huduma ya kichungaji kwa miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Ni wakati wa kujenga na kuimarisha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa Wakristo huko Iraq ambao wanakabiliwa na changamoto kubwa katika maisha na utume wao kama Wakristo.

Ni matumaini ya Kanisa kwamba, huruma ya Mungu itaweza kuganga na kuponya madonda ya vita na ghasia na hatimaye, kutoa faraja kwa watu wanaowaombolezea ndugu zao waliopoteza maisha wakati wa vita! Familia ya Mungu nchini Iraq inaanza kujenga ukurasa mpya wa maisha na utume wake, changamoto kwa viongozi wa Kanisa ni kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa umoja na mshikamano kati ya viongozi wa Makanisa pamoja na waamini wao, ili kuondokana na kishawishi cha utengano na mipasuko na kuwa na uhakika wa mshikamano hata kwa siku za usoni nchini Iraq, sanjari na ujenzi wa matumaini kati ya watu bila ya kukata wala kukatishwa tamaa.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 5 Oktoba 2017, wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Sinodi ya Kanisa la Caldea wanaojiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi yao. Iraq ni nchi ambayo kadiri ya Mapokeo ya Kanisa iliinjilishwa na Mtakatifu Toma na sasa inapaswa kuwa ni eneo la majadiliano ya kidini na kiekumene, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema.

Baba Mtakatifu anawataka Mababa wa Sinodi kuwa makini na vijana wanaotamani kuingia katika maisha na wito wa Kipadre na Kitawa; kwa viongozi wa Kanisa kuwa karibu nao sanjari na kuhakikisha kwamba, wanapata majiundo makini ya awali na endelevu katika maisha na utume wao kama Mapadre na Watawa. Baba Mtakatifu anawashauri Mababa wa Sinodi ya Kanisa la Caldea kutoa kipaumbele cha pekee kwa waamini wao walioko nje ya Iraq: kwa kuangalia idadi yao na uhuru wa kidini, ili wote hawa waweze kupata huduma za kichungaji hata wakiwa nje ya nchi yao kama walivyokazia Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, daima kwa kujenga umoja, udugu na mshikamano na Wakristo wengine wote, kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Majadiliano ya kidini na kiekumene, hayana budi kupata chimbuko lake katika umoja na mshikamano kama Wakatoliki.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahakikishia Mababa wa Sinodi ya Kanisa la Caldea kuwa, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, litaendelea kuwa pamoja nao katika maisha na utume wao. Ni matumaini yake kwamba, Sinodi hii, inayofanyika hapa mjini Roma, kwa jicho la Kristo Mchungaji mwema, ni muda muafaka wa tafakari ya kina kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Caldea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.