2017-10-06 06:44:00

Jengeni utamaduni wa uvuvi endelevu na unaowawajibikia binadamu!


Kongamano la XXIV la Utume wa Bahari limefunguliwa tarehe 1 Oktoba, 2017 huko Kaohsiung, Taiwan, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Nimenaswa katika mtego”. Wajumbe wanajielekeza zaidi katika maboresho ya maisha ya wafanyakazi katika sekta ya uvuvi duniani kwa kupambana na biashara haramu ya binadamu; changamoto ya wahamiaji na wakimbizi; kazi za suluba pamoja na uvuvi haramu mambo yanayotishia usalama, maisha, utu na heshima ya binadamu miongoni mwa wavuvi.

Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu katika hotuba yake elekezi, amekazia utu, heshima pamoja na haki msingi za binadamu na kwa namna ya pekee, wavuvi, ili pamoja na familia zao, waweze kuishi maisha bora zaidi kuliko kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na umaskini na kiwango chao cha elimu! Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuzivalia njuga changamoto za maisha ya wavuvi na utume wao katika sekta ya uvuvi.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, biashara baharini inachukua nafasi kubwa sana katika kuchangia kwa biashara na ukuaji wa uchumi duniani. Lakini, inasikitisha kuona kwamba, haki msingi za binadamu, utu na heshima ya wavuvi vinatelekezwa na matokeo yake, wavuvi mara nyingi wamekuwa ni wahanga wa biashara haramu ya binadamu na nyanyaso za kila aina. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana na biashara haramu ya binadamu; kazi za suluba; pamoja na kuhakikisha kwamba, wahalifu wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria, ili kweli sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Mama Kanisa kwa upande wake, ataendelea kuwa karibu sana wavuvi pamoja na familia zao, kwa njia ya Utume wa Bahari, ili kuwasaidia kiroho na kimwili. Kanisa linataka kuwa ni sauti ya kinabii kwa wavuvi wanaonyanyasika katika maisha, hata kama wanachangia kikamilifu katika mchakato wa ukuaji wa uchumi kimataifa! Jumuiya ya kimataifa haina budi pia kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendelea rasimali na urithi wa Jumuiya ya Kimataifa. Binadamu anapaswakutambua kwamba, amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho!

Askofu mkuu Marcelo Sanchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi pamoja na Sayansi Jamii amepembua kwa kina na mapana jitihada za Baba Mtakatifu Francisko katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo na mifumo yake yote, inayodhalilisha ut una heshima ya binadamu. Huu ni ushirikiano kati ya viongozi wa kidini, makamanda wa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Haya ni mapambano yanayozingatia utawala wa sheria, hakimsingi za binadamu na itifaki za Jumuiya ya Kimataifa. Askofu mkuu Marcelo Sanchez Sorondo anasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuragibisha jitihada za kijamii dhidi ya biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake yote. Jamii inapaswa kuwajibika kikamilifu dhidi ya vitendo hivi ambavyo ni uhalifu dhidi ya binadamu na haki zake msingi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.