2017-10-05 07:34:00

Utu na heshima ya binadamu ni kiini cha sera na mikakati ya maendeleo


Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka inajitahidi kupiga hatua mbele katika mapambano dhidi ya umaskini duniani, lakini hali ya umaskini bado inahitaji kuvaliwa njuga! Kumekuwepo na dalili za kucharuka kwa hali ya uchumi kimataifa, ustawi na maendeleo ya teknolojia, lakini bado kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu ili kuhakikisha kwamba Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu kwa Mwaka 2030 yanatekelezwa kwa dhati.

Hoja hii inapaswa kwenda sanjari na maboresho ya maisha ya wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia: usalama, hifadhi na haki zao msingi. Baa la njaa linaendelea pia kutishia usalama na maisha ya mamilioni ya watu duniani na kwamba, kuna pengo kubwa kati ya matajiri na maskini, ndio hao “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi”. Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kuwekeza katika utengenezaji wa fursa za ajira, lakini bado kuna mamilioni ya watu wanaoendelea kuteseka kutokana na mifumo ya uchumi isiyojikita katika maendeleo endelevu ya binadamu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake! Matokeo yake, maskini wanaendelea kutengwa kutoka katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani! Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika sera za maendeleo endelevu ya binadamu, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza kama mhimili mkuu wa maendeleo duniani, ili kukuza na kudumisha haki, usawa, amani na utulivu kati ya watu wa Mataifa!

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati akichangia hoja ya maendeleo ya kijamii, kwenye mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huko New York, Marekani. Anakaza kusema, uchumi wa kimataifa hauna budi kuwaletea watu wengi zaidi, ustawi na maendeleo: kiroho na kimwili, kwa kuzingatia kanuni ya auni; utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana ili kukidhi mahitaji msingi hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Uwajibikaji na mafao ya wengi ni mambo msingi katika utekelezaji wa sera makini za kiuchumi.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwajengea maskini uwezo wa kupambana na hali zao za maisha kwa kuwashirikisha katika kupanga sera na utekelezaji wake. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwaangalia wazee na maskini kwa kuwapatia huduma makini, ili kuwawezesha pia kuendelea kuchangia katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya jamii, kama sehemu ya utu wao. Harakati zinazopania kuboresha huduma za kijamii, kwa kukazia umuhimu wa kuanzishwa kwa Mifuko ya Kijamii itakayowasaidia walengwa kupata huduma mbali mbali za kijamii kama vile Bima ya Afya na uhakika wa maisha yao ni mambo muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya watu, hasa wazee na maskini.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anakazia umuhimu  wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hasa kwa kuwekeza miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili kutambua na kuthamini zawadi ya uhai na kwamba, maendeleo ni mchakato wa utimilifu wa utu na heshima ya binadamu! Vijana wajengewe uwezo wa kupambana na changamoto zao za maisha.

Askofu mkuu Bernardito Auza anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi katika utekelezaji wa sera na mikakati inayopania kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna sababu mbali mbali ambazo zinawafanya watu kukimbia na kuzihama nchi zao. Hawa ni watu walioathirika kwa vita, majanga asilia, dhuluma na nyanyaso. Kumbe, wanapaswa kupewa huduma msingi katika maisha yao, kwa kulinda na kuheshimu utu wao kama binadamu. Sera na maendeleo endelevu hazina budi kujikita katika utu wa binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.