2017-10-03 15:05:00

Papa Francisko atuma salam za rambi rambi kwa wananchi wa Las Vegas


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mauaji ya watu 59 yaliyotokea tarehe 1 Oktoba 2017 huko Las Vegas, Marekani na kuwaacha maelfu ya watu wakiwa wamejeruhiwa baada ya Stephen Craig Paddock kuwafyatulia risasi watu waliokuwa wanashiriki katika tamasha ya muziki. Katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Joseph Anthony Pepe anasema, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote walioguswa na kutikishwa na mashambulizi haya. Anawapongeza wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kwa jinsi ambavyo vimejitahidi kuokoa maisha ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaweka  marehemu wote chini ya huruma ya Baba wa milele pamoja na kuwaombea wale waliopata majeraha kupona haraka ili waweze kuendelea na kushughuli zao.

Wakati huo huo, Askofu Joseph Anthony Pepe katika tamko lake kwa familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Las Vegas, nchini Marekani, anasema, anapenda kuungana na watu wote wenye mapenzi mema kuomboleza vifo vya watu waliouwawa kwa shambulizi la risasi; anapenda kuwatia shime wafanyakazi katika sekta ya afya wanaoendelea kutoa tiba kwa majeruhi na kwamba, kila mtu anahamasishwa kuwa ni Msamaria mwema kwa jirani yake. Anapenda kuchukua nafasi hii kuwaombea wananchi wote wa Las Vegas na sehemu mbali mbali za dunia, ambao wanaathirika kutokana na mashambulizi, vurgu na kinzani za kijamii. Jioni, tarehe 2 Oktoba 2017, kumefanyika Ibada ya kiekumene kwa ajili ya kuwambuka na kuwaombea waliopoteza maisha pamoja na wale waliojeruhiwa wakati wa shambulizi hilo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.