2017-10-02 14:31:00

Papa Francisko awataka watu wenye mapenzi mema kuwa walinzi wa maisha


Maisha ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika katika utunzaji bora wa kazi ya uumbaji, kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Changamoto za uharibifu wa ekolojia kwa nyakati hizi ni chachu ya kuanza kujikita katika mchakato wa matumaini ya utunzaji bora wa kazi ya uumbaji, kama kielelezo cha upendo wa Mungu kwa binadamu! Binadamu wanahamasishwa na Kristo Yesu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo kwa jirani zao, kwa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha Amri ya upendo kwa Mungu na jirani kama kielelezo na ushuhuda wa Fumbo la Pasaka.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 2 Oktoba 2017 wakati alipokutana na kuzungumza na washiriki wa mkutano wa Taasisi ya Kujitolea Kitaifa nchini Italia. Upya wa amri ya upendo unafumbatwa katika tafsiri yenyewe ambayo Kristo Yesu anajitambulishwa kuwa ni kielelezo cha upendo unaomwilishwa katika huduma makini, kama alivyofanya mwenyewe kwa kuwaosha Mitume miguu yao. Huu ni upendo unaosimikwa katika unyenyekevu; kwa kukataa aina zote za ghasia na fujo; ni upendo unaoheshimu na kuthamini: uhuru na utu wa binadamu; kwa kuwaambata wote pasi na ubaguzi.

Baba Mtakatifu anasema, huu ni upendo wenye nguvu kuliko chuki, hasira na uhasama. Amri ya upendo ni urithi kwa wafuasi wote wa Kristo Yesu wanaopaswa kuratibu maisha na matendo yao mintarafu ukarimu wa Kristo mwenyewe! Siku ya majitoleo kitaifa, inaadhimishwa nchini Italia, kila mwaka ifikapo tarehe 4 Oktoba na kwamba, sadaka na majitoleo binafsi ni kiini cha Injili ya Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujichotea uzoefu na mang’amuzi ya maisha haya kama sehemu ya malezi na majiundo yao ya kiutu. Kutoa kwa ukarimu ni tendo linalomwongezea mtoaji furaha na yule anayepoke zawadi hii; ni tendo linalojenga na kukuza umoja na mshikamano.

Papa Francisko anawataka vijana wawe mstari wa mbele katika kulinda zawadi ya maisha na kazi ya uumbaji; mashuhuda wa upendo unaozaa mafao ya wengi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia wajumbe hawa uwepo wake wa daima kwa njia ya sala, ili kuwasindikiza katika sadaka na majitoleo yao! Amewasihi hata wao, kumkumbuka katika sala na sadaka zao, anapotekeleza dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.