2017-09-30 15:11:00

Viongozi wanayo dhamana na wajibu wa kimaadili kuwalinda watu wao!


Viongozi wanayo dhamana na wajibu wa kuwalinda raia na mali zao; kutekeleza utawala wa sheria kadiri ya katiba ya nchi, kanuni maadili na utu wema, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa msukumo wa pekee. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kusimama kidete kuwalinda watu dhidi ya mauaji ya kimbari, vita na ghasia; ukabila na udini usiokuwa na mvuto wala mashiko sanjari na kuhakikisha kwamba: maisha ya watu, mali na usalama wao vinadumishwa katika jamii!

Lakini, ukweli wa mambo unaonesha kwamba, kuna wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wa kuwalinda watu, utu na heshima yao kama binadamu na matokeo yake ni vita, ghasia na mipasuko ya kijamii inayosikika sehemu mbali mbali za dunia! Ikumbukwe kwamba, hata viongozi wa kidini wanayo dhamana na wajibu wanaopaswa kuutekeleza katika jamii zao kwa kujikita zaidi katika kanuni ya dhahabu! Mtendee mwenzako yale unayotaka kutendewa naye! Hii ni kanuni maadili inayolinda na kudumisha maisha ya mwanadamu dhidi ya utamaduni wa kifo!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati akichangia hoja kuhusu wajibu wa viongozi kuwalinda raia wao kwenye mkutano wa 72 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani! Baba Mtakatifu Francisko anasema, viongozi wa kidini wanayo dhamana ya kujenga utamaduni wa amani na madaraja ya watu kukutana katika hali ya unyenyekevu na uvumilivu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kuweza kutoa huduma makini kwa familia ya Mungu duniani.

Dini ya kweli, kamwe haiwezi kuchochea vita na ghasia kwani kufanya hivi ni kwenda kinyume cha haki msingi za binadamu! Umoja na udugu ni mambo yanayofumbatwa katika imani kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa vyote anayewaunganisha binadamu wote, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wake. Pale Mwenyezi Mungu anapoondolewa katika maisha ya watu, matokeo yake ni kudhalilisha utu na heshima ya binadamu sanjari na kuvunja haki zake msingi! Uwepo wa Mungu ni kigezo kikuu cha ujenzi wa udugu, amani na mshikamano wa dhati; mambo yanayokuzwa kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene.

Dini ya kweli ni chemchemi ya amani, upendo na mshikamano na kamwe si sababu ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii. Ubaguzi wowote ule unaofanywa kwa misingi ya kidini ni kinyume kabisa cha uwepo wa Mungu kwani Mungu ni upendo! Dini mbali mbali duniani ziwe ni vyombo vya upendo, umoja, mshikamano na maridhiano kati ya watu! Viongozi wa kidini wasaidie jitihada za Jumuiya ya Kimataifa katika ujenzi wa maridhiano kati ya watu, ili hatimaye, kuondokana na mauaji ya kimbari, vita na ghasia mambo ambayo ni kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu anasema Askofu mkuu Paul Richard Gallagher.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.