2017-09-29 10:32:00

Maaskofu Katoliki DRC: Utekaji nyara na mauaji ya viongozi wa Kanisa


Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO linasema, matukio ya utekaji nyara na mauaji ya viongozi wa Kanisa ambao wamekuwa ni sauti ya kinabii katika mchakato wa kutetea haki, amani na upatanisho wa kitaifa ni dalili kwamba, Kanisa kwa sasa linashambuliwa na “watu wasiojulikana”, kwani hadi sasa Serikali imeshindwa kuwatia mbaroni na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa vitendo hivi vya kinyama! Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Marcel Utembi Tapa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC anayewataka wale wote waliowateka Mapadre kuwaachia huru ili waweze kuendelea na utume na maisha yao ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Mapadre ambao wametekwa nyara na hadi sasa hawajulikani mahali waliko ni pamoja na:  Padre Pierre Akilimali na Padre Charles Kipasa; Padre Jean Pierre Ndulani, Anselme Wasikundi na Edmond Bamutate; waliotekwa nyara kunako mwezi Oktoba 2012. Matukio ya utekaji nyara na mauaji ya viongozi wa Kanisa yanaendelea kuongeza hofu na mashaka ya ulinzi na usalama wa viongozi wa Kanisa nchini DRC. Hawa ni viongozi ambao wengi wao wamesimama kidete kupigania haki, amani na upatanisho wa kitaifa kwa kulaani uporaji wa rasilimali za DRC kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache ndani ya jamii, wanaoshirikiana na Makampuni ya kigeni!

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaendelea kufafanua kwamba, machafuko ya hali ya kisiasa nchini humo, kukwama kwa mchakato wa uchaguzi mkuu uliotarajiwa kufanyika mwaka 2017 pamoja na kuvunjwa kwa makusudi makubaliano ya mwaka 2016 yaliyopitisha kwamba, uchaguzi mkuu nchini DRC ufanyike mwaka 2017. Baraza la Maaskofu Katoliki likaombwa kusaidia mchakato wa majadiliano ya kisiasa nchini humo, hali ambayo ilitafsiriwa na baadhi ya wakereketwa wa masuala ya kisiasa kwamba Kanisa lilikuwa linaingilia masuala ya kisiasa na kusahau kwamba, Kanisa pia linamhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika waraka wao wa “Gaudium et spes” yaani “Furaha na matumaini” wanasema uchungu na fadhaa ya mwanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo la hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao! Mchango wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC katika mchakato wa amani na upatanisho nchini DRC, ulipelekea baadhi ya Makanisa kuchomwa moto, kama njia ya kulitisha Kanisa Katoliki nchini DRC, ili lisijiingize kwenye masuala ya kisiasa. Lakini, Askofu mkuu Marcel Utembi Tapa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC anasema, Kanisa litaendelea kutangaza na kushuhudia haki, amani, utawala wa sheria; utawala bora mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.