2017-09-29 09:59:00

Jumuiya ya Kimataifa na mapambano dhidi ya biashara ya binadamu


Sera ya tamko la utekelezaji wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu iliyoridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa inakazia pamoja na mambo mengine: mshikamano na huruma kwa wahanga wa biashara haramu ya binadamu; umuhimu wa kudumisha haki zao msingi pamoja na kuwasaidia ili kuanza tena maisha mapya, dhamana inayotekelezwa kwa ushirikiano wa wadau mbali mbali. Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake, limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu,ambayo kimsingi ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa, katika mkutano wa 72 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, huko New York, Marekani, kama sehemu ya majadiliano ya viongozi wakuu wa kimataifa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo!

Viongozi mbali mbali wa kidini kwa kuongozwa na tunu msingi za maisha ya dini zao, huku wakisukumwa na uhuru wa ndani, wameamua kwa dhati kabisa, kupambana na biashara haramu ya binadamu duniani kwa matumaini kwamba, vita hii, itaungwa mkono pia na wadau wengine wa maendeleo endelevu ya binadamu, ili hatimaye, utumwa mamboleo na mifumo yake yote, iweze kung’olewa kutoka katika uso wa duni. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kama sehemu ya vipaumbele vyake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Katika mwelekeo huu, TALITHA KUM,  ambao ni mtandao wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume yapatayo 22, kutoka katika nchi 70 duniani, umekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo na mifumo yake yote. Umewasaidia wanawake na wasichana kupata heshima na utu wao kama binadamu; umewajengea fursa ya kurejea tena katika maisha yao ya kawaida.

Barani Ulaya, kuna mtandao wa mashirika ya kitawa dhidi ya biashara haramu ya binadamu unaojulikana kama RENATE unaounganisha mashirika 63 ya kitawa yanayotekeleza dhamana na utume wake katika nchi 27 Barani Ulaya. Wahanga wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo, wana imani zaidi na mashirika ya kitawa na kazi za kitume katika huduma kwa ajili yao ikilinganishwa na wadau wengine. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa dhati katika umoja na udugu ili kuendeleza mapambano dhidi ya biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, akichangia hoja kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kwa mwaka 2030 anasema ni alama ya matumaini inayoiwajibisha Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika mapambano dhidi ya: umaskini wa hali na kipato, biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake yote inayonyanyasa utu na heshima ya binadamu. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kufanya tathmini ya kina ili kuangalia mafanikio na na mapungufu yake.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika: kuzuia biashara haramu ya binadamu na kuwalinda waathirika; kuwafikisha wahusika kwenye mkondo wa sheria; kushirikiana na wadau mbali mbali katika mapambano na huduma kwa waathirika wa biashara na utumwa mamboleo. Ili kufanikisha malengo haya kuna haja ya kuendeleza elimu ya umma na uragibishaji wa madhara ya biashara na utumwa mamboleo, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote! Kudhibiti: vita, ghasia na mipasuko ya kijamii kwa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, ustawi na mafao ya wengi.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwafikisha kwenye mkondo wa sheria wafanyabiashara na wafadhili wao; kuimarisha mfumo na utekelezaji wa sheria kimataifa; kukuza ushirikiano wa kiintelijensia ili hatimaye, biashara hii iweze kushughulikiwa kuanzia kwenye mizizi yake. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa kimsingi na Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha kinachowajumuisha Makamanda wa Polisi na Maaskofu wanaoshirikiana kwa karibu sana katika mapambano haya! Umoja, mshikamano na udugu ni mambo msingi katika kufanikisha sera na mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.