2017-09-28 14:44:00

Padre Ryszard Szmydki, ateuliwa kuwa Katibu mkuu msaidizi!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Ryszard Szmydki, O.M.I kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Katibu mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari. Alizaliwa tarehe 26 Aprili 1951 huko Tarebiski, nchini Poland. Kunako mwaka 1970 akajiunga na Shirika la Wamisionari wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na kuweka nadhiri zake za daima kunako tarehe 21 Januari 1977.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe 2 Julai 1978. Baadaye akajiendeleza kwa masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana na kufaulu kujipatia Shahada ya Uzamivu katika masomo ya Mafundisho Sadikifu ya Kanisa kutoka katika Chuo Kikuu cha Lubin, nchini Poland ambako pia alibahatika kufundisha kwa muda wa miaka kadhaa. Alitumwa na wakuu wake wa Shirika kwenda kufanya utume nchini Cameroon kwa muda wa miaka miwili.

Kunako mwaka 2005 alirejea tena nchini Poland na kuteuliwa kuwa ni Vikarieti wa Kanda kwa ajili ya nchi za kimisionari kwa upande wa Shirika. Mwaka 2010 akateuliwa kuwa Padre mkuu wa kanda ya Shirika la Wamisionari wa Bikira maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na kuchaguliwa tena kunako mwaka 2013. Tarehe 3 Aprili 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamteuliwa kuwa Katibu mkuu Katibu mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari chini ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.