2017-09-27 13:08:00

Utii unamwilishwa katika ukweli na matendo!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, tuanze tafakari yetu tukisoma sehemu ya Injili ya Mt. 7:21 – si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana’, atakayeingia katika ufalme wa mbingu, bali yeye afanyaye atakayo Baba yangu aliye mbinguni. Leo tunasoma sehemu ya Injili ya Mt. 21:28-32 ambapo Yesu anaongea kuhusu utii na ukweli katika hekalu la Yerusalemu siku chake kabla ya hukumu na kifo chake. Katika Iinjili ya leo tunasikia habari ya wana wawili wanaotumwa kazi na baba yao.  Wa kwanza anasema hapana halafu anaenda. Hili kundi halina maneno mema lakini linatenda.Yule anayesema hapana halafu anatenda, anawakilisha kundi la wale ambao waliishi nje ya sheria na mapenzi ya Mungu, lakini pamoja na Kristo, walitafakari na kulipokea neno. Kundi hili linafananishwa na makahaba na watoza ushuru ambao kwanza wanasema hapana halafu wanafuata mapenzi ya baba. 

Wa pili anasema ndiyo lakini haendi. Yule anayesema ndiyo halafu hatendi anawakilisha kundi la wale waliofuata sheria kwa namna yao lakini hawakumpokea Kristo ambaye ni ukamilifu wa sheria. Kundi hili linasema ndiyo linawakilisha mafarisayo na waandishi. Hili kundi lina maneno mazuri lakini halina matendo mema. Kwa hakika watoto wote wawili si wema kwani si watiifu kwa baba yao. Hapa tunaona makundi mawili tofauti ya watu na namna mbili tofauti za kuhusiana na Mungu. Hata hivyo namna hizi mbili sio njia au namna sahihi ya kumfuata Yesu. Ndiyo maana Yesu anahitimisha fundisho lake akisema hata makahaba na wapagani wataingia ufalme wa Mungu kabla ya Mafarisayo na walimu wa sheria. Sisi tunatakiwa kuwa wazi na watii, tukishuhudia imani yetu kwa maneno na matendo.  Ili hili liwezekane ni lazima upendo wa Mungu kwetu upate nafasi ya kwanza katika maisha yetu.

Tutafakarishwe na mfano huu thabiti wa maisha ya utii, ukweli na uwazi ya mashahidi wa Uganda jinsi ya kuwa waaminifu katika ndiyo yetu kwa Bwana. Katika kitabu ‘Hadithi za Kiafrika’, uk. 55 ikitoka katika kitabu cha ‘Our Ancestors in Faith’ tunapata habari ya maisha ya ujasiri, ya uwazi, ya utii na ukweli ya kina Karoli Lwanga na wenzake wafia dini mashahidi wa Uganda. Yosefu Mukasa alikuwa wa kwanza kuuawa na baadaye usukani wa kundi ukachukuliwa na Karoli Lwanga. Karoli Lwanga alihakikisha na kuhamasisha kundi libaki aminifu katika pendo lao kwa Bwana wao. Hawakubadilika katika ile ndiyo yao kwa Bwana, katika imani yao kwa Kristo. Walikaidi amri ya ufalme na wakaweka matumaini yao yote kwa Mungu. Walipoamrishwa kumkana Kristo, Bruno mmoja wa mashujaa chipukizi alisema kwa utulivu, ‘unaweza kuichoma moto miili yetu, lakini hutaweza kuziunguza roho zetu. Roho zetu zitakwenda Paradiso’. Huu ndio ufuasi wa kweli na maisha mapya na aminifu katika Kristo. Katika msalaba wa Kristo wanapata utukufu. Wafiadini hawa watusaidie leo kutafakari uaminifu wetu katika ufuasi. Wao walibaki aminifu katika ndiyo yao kwa sauti na wito wa Bwana.

Tukumbuke kuwa upendo kwa Kristo huimarisha mapendo mengine, maana katika yeye upendo wa kweli hupata maana na msingi wa kudumu na neema ya Mungu katika utendaji wetu huonekana wazi. Mtume Paulo katika Efeso 5:2 anasema – mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi, tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.

Ndugu wapendwa, maisha halisi ya ufuasi na utii wa kweli huonekana katika kumpenda Bwana kama alivyotupenda sisi na kwamba kuishi kadiri ya amri na agizo lake tunapata wokovu. Upendo huu ukiwepo basi ile hatari ya hapana halafu ndiyo na ndiyo halafu hapana itatoweka. Mwinjili Luka katika 5:1-11 – anatukumbusha juu ya faida ipatikanayo katika kuitii sauti ya Mungu. Katika sehemu hii ya maandiko matakatifu tunasikia Mtume Petro akiambiwa na Bwana atupe nyavu baharini baada ya wao kukosa samaki usiku na anamwagiza kuvua katika muda ambao si muda wa kuvua samaki. Petro anasema, Bwana, tumejitahidi sana usiku mzima tusipate kitu, lakini kwa neno lako nitashusha nyavu. Walipofanya hivyo, walinasa samaki wengi mno, hata nyavu zao zikaanza kukatika. Utii kwa sauti ya Bwana unakuwa wokovu kwake na toka hapo anapewa wajibu mkubwa zaidi. Nasi leo baada ya kusikia neno hili hatuna budi kujiuliza juu ya usikivu wetu, utii wetu na uaminifu wetu kwa sauti ya Bwana anayetuita kushirika uzima wake wa milele. Sisi tunasikia nini na tunafaya nini katika ujenzi wa ufalme wa Mungu? Je kuna uwiano sahihi kati ya kile tunachofahamu kuhusu ufalme wa Mungu na kile tunachotenda katika kuujenga ufalme huo?

Tumsifu Yesu Kristo

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.