2017-09-25 12:21:00

Uchaguzi mkuu nchini Kenya kwa Mwaka 2017 wachukua sura mpya tena!


Sakata la uchaguzi mkuu nchini Kenya linaendelea kuchukua sura mpya baada ya Mwendesha mashtaka mkuu wa Serikali ya Kenya Bwana Keriako Tobiko kuamuru Tume ya kupambana na rushwa pamoja na Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa madai ya kuvuruga zoezi la uchaguzi mkuu nchini Kenya uliofanyika tarehe 8 Agosti 2017, hali iliyopelekea matokeo ya uchaguzi mkuu kufutwa na Mahakama kuu ya Kenya. Kenya inatarajia kufanya tena uchaguzi mkuu hapo tarehe 26 Oktoba 2017.

Uchunguzi huu unapaswa kuwasilisha taarifa zake katika kipindi cha siku 21 kuanzia sasa. Vyombo hivi vya ulinzi na usalama vitakuwa na dhamana ya kuchunguza madai kwamba, maafida wawili wakuu wa Muungano wa Upinzani nchini Kenya, walifaulu kudukua Computer za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka. Na habari zaidi kutoka kwenye vyama vya upinzani nchini Kenya zinasema, vinajipanga ili kwa maandamano makubwa ili kuwashinikisha viongozi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kuachia ngazi ya uongozi kwani wanannchi hawana imani nao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.