2017-09-22 16:26:00

Bado Japan inahitaji kuinjilishwa!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika safari yake ya kikazi nchini Japan, Alhamisi, tarehe 21 Septemba 2017 ametembelea Jimbo kuu la Osaka na kukutana na maaskofu, mapadre na waamini walei na hatimaye, akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Amekazia umuhimu wa ushuhuda wa Kanisa katika huduma makini ya binadamu kwenye sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji! Amewashukuru Maaskofu kwa upendo na ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaohitaji: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi huko Japan.

Kardinali Filoni anasema, hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo bado kuna haja ya kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya nchini Japan, unaojikita katika ushuhuda amini na makini! Katika mahubiri yake, anakaza kusema, Mwenyezi Mungu ndiye anayepiga hatua ya kwanza katika mchakato wa wito kama alivyofanya kwa Mathayo, mtoza ushuru, aliyebahatika kuangaliwa na Kristo Yesu kwa jicho la huruma na mapendo, kiasi cha kuacha yote na kuanza kumfuasa!

Kardinali Filoni ametumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza Maaskofu Katoliki wanaounda Jimbo kuu la Osaka, Japan pamoja na kuwafikishia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewakumbuka na kuwasindikiza katika maisbha na utume wao kwa njia ya sala na sadaka yake. Imekuwa ni nafasi ya kusikiliza, mafanikio, matatizo, changamoto na fursa zilizopo Jimbo kuu la Osaka katika maisha na utume wa Kanisa. Huduma makini katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii ni kati ya mchango mkubwa ambao umetolewa na Mama Kanisa nchini Japan tangu baada ya Vita kuu ya Pili ya dunia.

Kanisa limeendelea kuwafunda watu wa Mungu nchini Japan kwa katekesi makini na huduma mbali mbali za maisha ya kiroho kama sehemu ya maadhimisho ya Mafumbo ya kanisa. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuwekeza katika miito, ari na mwamko wa kimisionari ili kuwapata watenda kazi katika shamba la Bwana watakaokuwa tayari kutangaza, kushuhudia na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, daima wakivutwa na upendo wa Mungu na jirani katika maisha yao! Kanisa linawapongeza Maaskofu Katoliki nchini Japan kwa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji; kwa kuwapokea na kuwakirimia kwa moyo wa upendo na ukarimu pamoja na kuendelea kupangusa machozi na majonzi ya maisha yao! Kardinali Filoni anawaalika Maaskofu kushirikiana na Makanisa mahalia wanamotoka wakimbizi na wahamiaji hawa ili kuweza kuwapatia huduma makini zaidi

Akizungumza na mapadre, watawa na waamini walei, Kardinali Filoni, ameipongeza familia ya Mungu nchini Japan kwa juhudi na bidii ya kazi. Amewataka wawe makini katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, ili kamwe wasimezwe na malimwengu na kujikuta wakikengeuka katika maadili, utu wema au ukanimungu kiasi cha kutoona tena umuhimu wa maisha ya sala na utakatifu wa maisha. Waendelee kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama kielelezo cha imani tendaji. Maaskofu wawe ni mashuhuda na vyombo vya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; mambo msingi katika mchakato wa uinjilishaji mpya!

Hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, Japan bado inahitaji kuinjilishwa, kwa kujikita katika Injili ya upendo, huruma na mshikamano; kwa kupambana na umaskini wa hali na kipato, ili kuwarejeshea watu utu na heshima yao kama binadamu! Maaskofu wakumbuke kwamba, maskini ni walengwa wakubwa wa Habari Njema ya Wokovu na amana ya Kanisa. Maaskofu katika mchakato wa uinjilishaji mpya wasimame kidete kulinda, kutetea na kudumisha  utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Changamoto za maisha na utume wa Kanisa nchini Japan zivaliwe njuga na kupewa ufumbuzi kwa mwanga wa Injili.

Katika mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Osaka, nchini Japan, Kardinali Filoni, amekazia umuhimu wa kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu anayechukua hatua ya kwanza kwa kuita waja wake, ili waweze kushiriki katika kazi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama alivyofanya kwa Mathayo, mtoza ushuru, ambaye sasa ni mtangazaji na shuhuda wa Injili ya Kristo! Katika kuitikia wito, waamini wajenge tabi ana utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kutenda mintarafu mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Katika mchakato wa uinjilishaji mpya, Kanisa nchini Japan linakumbana na ugumu wa mioyo ya watu ambao wamesongwa sana na: kazi, masomo, shughuli za kijamii na kiuchumi kiasi hata cha kusahau kuboresha maisha yao ya kiroho, kiutu na kimaadili. Matokeo yake ni watu kusongwa sana na matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia, michezo ya Computer kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu hana tena nafasi katika maisha ya watu! Waamini wanapaswa kuboresha wito wao wa kwanza ambao ni maisha ya Kikristo yanayopaswa kufumbatwa katika mchakato wa utakatifu wa maisha. Wito wa pili ni ndoa na familia; au maisha ya kipadre na kitawa. Waamini wawe daima na ujasiri wa kubeba vyema misalaba yao na kuanza kumfuasa Kristo ili waweze kujifunza kutoka kwake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.