2017-09-21 16:01:00

Utumwa mamboleo ni kashfa dhidi ya utu na heshima ya binadamu!


Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo na mifumo yake yote inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Kanisa limeendelea kuwatetea watu wanaofanyishwa kazi za suluba kwa ujira “kiduchu”. Hivi ni vitendo vinavyowadhalilisha watu na kuwageuza kuwa kama biashara sokoni, jambo ambalo ni kashfa kwa Mwenyezi Mungu. Biashara haramu ya binadamu inaweza kudhibitiwa kikamilifu na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwa na muundo imara wa mahakama, ushirikiano makini na wadau mbali mbali; kwa kuibua na kutekeleza mbinu mkakati wa muda mrefu ili kupambana na uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kuwaadhibu wahusika sanjari na kuwahudumia waathirika.

Huu ni mchango uliotolewa na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati alipokuwa anashiriki kwenye mkutano wa viongozi wakuu, ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa, huko New York, Marekani, tarehe 19 Septemba 2017. Anasema, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa mstari wa mbele kulaani biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake yote na kwamba, hivi ni kati ya vipaumbele vyake katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu. Kutokana na mwelekeo huu, Kanisa Katoliki, taasisi pamoja na wadau mbali mbali kutoka katika serikali na sekta ya watu binafsi, wamekuwa wakishirikiana katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anaendelea kufafanua kwamba, Vatican kwa namna ya pekee, imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Uingereza katika ngazi mbali mbali kama sehemu ya mchakato unaopania kung’oa kabisa biashara haramu ya binadamu. Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha, kilianzishwa kwa sababu hii, ili kushirikiana kwa karibu zaidi na viongozi wa ulinzi na usalama pamoja na taasisi za Kanisa ili kuwaokoa waathirika na kuwasaidia ili waweze kurejea tena katika hali yao ya kawaida. Uzoefu unaonesha kwamba, waathirika wengi wanaogopa mchakato wa utekelezaji wa utawala wa sheria, lakini wana matumaini zaidi na taasisi zinazosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa, zinazowapatia msaada na makazi salama.

Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake, limekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wanawake na wasichana kutoka katika minyororo ya utumwa mamboleo, kwa kuwaonesha: huruma, upendo na uvumilivu tayari kuwasindikiza katika uhuru na hatimaye, kufikia ukamilifu wa maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Watawa wamekuwa mstari wa mbele katika huduma hii makini kwa waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Wameunda mtandao wa mshikamano kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanawake wanaookolewa kutoka katika nyanyaso za utumwa mamboleo. Wanaendelea kutumia rasilimali vitu na watu, ili kuwasaidia wanawake hawa.

Azimio la Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Dunia katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu uko mbioni kuanzishwa. Ni mpango mkakati unaokazia umuhimu wa ushirikiano katika utekelezaji wa maamuzi ya pamoja; sera na mikakati ya kung’oa biashara haramu ya binadamu. Kazi za suluba, utumwa mamboleo pamoja na biashara haramu ya binadamu ni mambo ambayo yanapaswa kushughuliwa kikamilifu na Jumuiya ya Kimataifa kwani yanavuka mipaka ya nchi. Ushirikiano, udugu na mshikamano wa dhati ni mambo msingi yanayoweza kuokoa mamilioni ya watu wanaonyanyasika utu na heshima yao, kwa kuwajengea tena uwezo wa kurejea katika uhalia wa maisha; kwa kudumisha utu na heshima yao sanjari na uhuru wao kama binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.