2017-09-21 16:26:00

Mchakato wa haki na amani ni sehemu ya uinjilishaji mpya!


Familia ya Mungu nchini Japan inapaswa kuwa ni chombo cha ujenzi wa amani; kukuza na kudumisha wito wake katika masuala ya kimaadili na maisha ya kiroho mjini Hiroshima na Japan katika ujumla wake mintarafu mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Japan bado ina kiu ya kutaka kuinjilishwa, dhamana inayotekelezwa na Mama Kanisa kwa njia ya majadiliano  ya kidini na huduma makini kwa watu wa Mungu.

Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Watakatifu Andrea Kim Taegon na wenzake, hapo tarehe 20 Septemba, 2017 wameombwa wasaidie kulipyaisha Kanisa la Kristo nchini Japan kwa kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya! Haya ndiyo mawazo makuu yaliyojiri wakati Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu alipokutana na kuzungumza na wakleri, watawa na waamini walei, Jimbo Katoliki la Hiroshima, nchini Japan, Jimbo linaloongozwa na Askofu Alexis Mitsuru Shirahama.

Kardinali Filoni amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtalatifu Francisko kwa ajili ya waamini wa Jimbo la Hiroshima, akiwakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika ujana wake, alitamani sana kuwa kati ya wamisionari nchini Japan. Yuko kati yao ili kuwatia shime, imani na matumaini ya kusonga mbele katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika msingi wa mashuhuda wa imani wa Hiroshima, ambao bado wanalikumbuka shambulio la kinyuklia lililofanywa kunako mwaka 1945 na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Huo ukawa ni mwanzo wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kutafuta haki na amani ndani na nje ya Japan. Mambo makuu matatu ni muhimu sana katika ujenzi wa amani duniani: msamaha, ukweli na haki. Msamaha wa Kikristo ni kitendo cha ujasiri mkubwa kinachomfungulia mwamini vifungo vya kutaka kulipiza kisasi na kuanza mchakato wa ujenzi wa msingi wa amani jamii na mwanzo mpya wa maisha ya kiroho; dawa inayotolewa na Mwenyezi Mungu peke yake anayefariji, anayeganga, kuponya na kusamehe dhambi.

Kardinali Filoni anaendelea kufafanua kwamba, Hiroshima maana yake ni “Mji wa amani”, changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hiroshima ni mahali pa upyaisho ambao Kristo anataka kuufanya kwa watu wake kwa kuamsha ari na mwamko wa maisha na utume wa kimisionari unaojikita katika ukarimu na moyo wa kitume, chemchemi ya furaha ya uinjilishaji yanayosaidia upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa.

Familia ya Mungu nchini Japan haina budi kusimama kidete kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ufalme wa Mungu, unaofunua utukufu, huruma, upendo na uaminifu wa Mungu kwa waja wake. Utukufu, neema na ukweli vinapaswa pia kuwafikie na kuwaambata wananchi wa Japan, ili kujenga na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu; umoja, upendo na mshikamano. Uwepo wa Kristo kati pamoja na watu wake, uwapatia matumaini mapya: maskini wanaoteseka, vijana wanaoathirika kwa matumizi haramu ya dawa za kulevya, kiasi hata cha kujikatia tamaa ya maisha. Wote hawa wanapaswa kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu inayowafunulia: huruma, neema na msamaha. Uinjilishaji unawawezesha waamini kuwathamini ndugu zao katika Kristo Yesu; unawawezesha kusimama kidete dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na kutoa huduma makini na endelevu kwa watu wote.

Katika mahubiri, Kardinali Filoni amewakumbuka mashuhuda wa imani na wafiadini nchini Korea waliojisadaka kwa ajili ya kumtangaza Kristo na Kanisa lake na kwamba, hata Japan ni nchi ambayo imelowanishwa kwa damu ya mashuhuda na waungama imani. Uinjilishaji mpya unajikita katika ushuhuda wa huduma makini kwa watu wa Mungu dhidi ya anasa, uchu wa mali na fedha. Jimbo Katoliki la Hiroshima halina budi kuwa ni chombo cha ujenzi wa haki na amani. Bado kuna madhara ya vita yanayojionesha nchini Iraq, Siria, Libya na katika sehemu mbali mbali za dunia. Mashuhuda wa imani wawawezeshe waamini kuwa kweli ni vyombo vya: haki, ukweli na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.