2017-09-21 15:34:00

Kashfa ya wema na huruma ya Mungu kwa Mathayo mtoza ushuru


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Septemba, anaadhimisha Siku kuu ya Mtume Mathayo, Mwinjili ambaye jina lake kwa lugha ya Kigiriki lina maanisha “Zawadi ya Mungu”. Alikuwa ni mtoza ushuru, lakini akabahatika kukutana na Lango la huruma ya Mungu, Kristo Yesu, aliyemwita na akaamua kuacha yote na kumfuasa na huo ukawa ni mwanzo wa toba na wongofu wa Mathayo mtoza ushuru. Mkutano huu na Yesu, ufunuo wa huruma ya Baba inakuwa ni nafasi ya kukutana, inageuka kuwa sherehe kubwa ya huruma ya Mungu na hatimaye, Mafarisayo wanaigeuza kuwa ni kashfa ya huruma ya Mungu. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa mahubiri yake, Alhamisi, tarehe 21 Septemba 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican.

Mathayo alikuwa na uso wa aibu na wala hakutaka kukutanisha uso wake na Kristo Yesu, lakini walipobahatika kukutanisha nyuso zao, akagundua jinsi ambavyo Yesu alimwangalia kwa jicho la huruma na mapendo! Mathayo mtoza ushuru aliyekuwa amejishikamanisha na fedha akayeyuka kama “mshumaa” na kuamua kumfuasa Kristo katika maisha yake. Hapa yalikuwa ni mapambano kati ya dhambi na huruma ya Mungu kwa mwanadamu anasema Baba Mtakatifu Francisko!

Lakini, upendo una nguvu, ukashinda na kupenyeza hata katika sakafu ya maisha ya Mathayo mtoza ushuru, aliyetambua kwamba, alikuwa ni mdhambi na wala hakupendwa na watu kwani alionekana kuwa ni kibaraka wa Warumi. Alijisikia mgonjwa na mdhambi lakini akaona mwanga wa huruma na mapendo kutoka kwa Kristo Yesu; mwanga unaoganga, kuponya na kumwokoa mwanadamu! Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa akina Lazaro aliyesikia mwaliko wa Kristo na kumwalika nyumbani kwake ili aweze kumfanyia sherehe kubwa, mdhambi akatubu na kumwongokea Mungu, hii ikawa ni siku kuu ya huruma ya Mungu ambayo Yesu ana amua kuwagawia watu wote pasi na ubaguzi.

Badala ya kuwa ni sherehe ya huruma ya Mungu kwa Mathayo mtoza ushuru na wadhambi wenzake, ikageuka kuwa ni sherehe ya kashfa ya huruma ya Mungu, kwa Yesu kushutumiwa kwamba, alikuwa anakula na kushirikiana na watoza ushuru! Alishutumiwa kwa kutofuata Sheria, lakini Yesu alitambua utume wake katika mchakato mzima wa ujenzi wa ufalme wa Mungu unaojengwa kwa upendo kwa Mungu na jirani. Huruma na upendo wa Kristo kwa wadhambi inakuwa ni fursa kwa watu kutubu na kumwongokea Mungu na kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma, upendo na wokovu wa Mungu kwa binadamu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hata kuna baadhi ya Wakatoliki wanao pigwa butwaa kutokana na kashfa ya huruma ya Mungu kwa wadhambi, lakini hii ni nafasi ya kujifunza kwamba, Mwenyezi Mungu anataka huruma na wala si sadaka. Hii ni nafasi kwa waamini kutambua kwamba, wao ni wadhambi na wanahitaji kufunuliwa Uso wa huruma ya Mungu. Kuna wadhambi wengi wengi ndani ya Kanisa wanaohitaji toba na wongofu wa ndani! Lakini pia, kuna watakatifu wengi ambao wameteseka sana na kudhulumiwa hawa ni kama akina Mtakatifu Yohana D’Arco, Mtakatifu Theresa na Mwenyeheri Rosmini. Lakini wote hawa wamekutana na Ufunuo wa huruma ya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu anayewatambua jinsi walivyo na anataka kukutana nao katika hija ya maisha yao! Inafurahisha sana kukutana na Uso wa huruma ya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, anasema, Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.