2017-09-20 15:23:00

Kanisa linataka kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwawezesha vijana


Kanisa linaendelea kujijengea utamaduni wa: kuwasindikiza na kuandamana na vijana; kuwasikiliza kwa makini ili kujibu matamanio yao halali katika maisha na hatimaye, kuwajengea uwezo ili kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa kuzingatia vipaumbele. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu, hivi karibuni imehitimisha mkutano wa kimataifa wa vijana kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayotimua vumbi mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”.

Mkutano wa vijana kimataifa, umewashirikisha vijana 82 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wataalam wa masuala ya vijana kutoka katika vyuo vikuu vya kipapa na vya kiserikali; walezi na mabingwa wa utume wa vijana. Semina hii imekuwa na uwakilishi mpana zaidi uliowashirikisha hata vijana kutoka katika dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, ambao kwa pamoja, wamejadili kuhusu utambulisho wao kama vijana, changamoto na matatizo wanayokumbana nayo katika maisha yao ya ujana.

Changamoto kubwa kwa wakati huu ni maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii; utandawazi: faida na hasara zake: Vijana na teknolojia; vijana na masuala ya maisha ya kiroho. Vijana wamepata fursa ya kutafakari mada zote hizi kwa kuongozwa na Neno la Mungu na hatimaye, vijana wakajimwaga uwanjani ili kuchangia hisia, vionjo, uzoefu na mang’amuzi yao katika ulimwengu wa vijana. Imekuwa ni fursa pia kwa vijana wa kizazi kipya kutoa ushuhuda wa mambo msingi katika maisha yao. Baadhi yao wamesimulia mateso na mahangaiko ya vijana katika maeneo ya vita, ghasia na mipasuko ya kijamii.

Vijana wamesisitiziwa kuhusu umuhimu wa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, kama mashuhuda wa matumaini kwa vijana wanaoteseka kutokana na changamoto za maisha: matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia pamoja na athari za utumwa mamboleo unaonyanyasa utu na heshima ya binadamu. Vijana wametakiwa kuwa makini na kamwe wasikubali kutumbukizwa kwenye utamaduni wa kifo na badala yake, wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai. Vijana wa kizazi kipya ni kundi linalotafuta utambulisho wake unaoweza kupatikana kwanza kabisa kwa njia ya elimu makini na endelevu; kwa kujikita katika toba, wongofu wa ndani na msamaha.

Changamoto kubwa inayoendelea kuwafanya vijana kukuna vichwa kiasi hata cha kukosa matumaini kwa siku za usoni ni ukosefu wa fursa za ajira. Kuna idadi kubwa ya vijana wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii, kisiasa na kidini. Lakini, vijana wamekumbushwa kwamba, wao ni matumaini na jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Wanapaswa kuwa ni vyombo na wajenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu badala ya kutumiwa na wajanja wachache kuchochea vita, vurugu na kinzani za kijamii kwa mafao ya wanasiasa uchwara! Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajihusisha kikamilifu katika maisha ya kisiasa na kijamii; kwa kuchangia mawazo na kushiriki katika vikao vinavyotoa maamuzi. Vijana wawe mstari wa mbele katika kushiriki kazi za kujitolea kama kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano.

Kama kuna jambo linalowatia vijana kiwewe ni maendeleo makubwa ya sayansi na kwamba, wangependa wawe ni wadau wakuu katika mchakato huu. Lakini, wamekumbushwa kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia yanabeba ndani mwake faida, hasara na changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga kwa njia ya elimu makini, kanuni maadili na utu wema. Sayansi na teknolojia iwawezeshe vijana pia kuwa ni wainjilishaji miongoni mwa vijana wenzao. Vijana wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa, kwa kujitahidi kukubai kuelimishwa na kufundwa na Mama Kanisa katika hija ya maisha yao ya ujana. Kanisa litaendelea kujenga utamaduni wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuandamana na vijana katika safari ya maisha yao: kiroho na kimwili. Kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, wamekumbushwa kwamba, wao ni sehemu ya familia ya Mungu, wanapaswa kusikilizana na hatimaye, kukua na kukomaa katika umoja wao kama vijana. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Kanisa ni nyumbani kwao; ambamo wanasikilizwa na kuhudumiwa kikamilifu.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu amehitimisha mkutano huu wa kimataifa kwa kuwakumbusha vijana kwamba, Kanisa linataka kuwasikiliza vijana kwa makini, lakini hata wao wanapaswa kuhamasishwa na ari, mwamko na upyaisho wa shughuli za kimisionari unayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa vijana. Wakati wa maadhimisho ya Sinodi vijana wataendele kutumia mitandao ya kijamii iliyotengwa na Sekretarieti kuu ya Maaskofu ili kuweza kufikisha ujumbe wao kwa Mababa wa Sinodi kwa anuani ifuatayo: “Synod2018”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.