2017-09-20 07:09:00

Kanisa limejengwa katika msingi wa imani ya Mitume wa Yesu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 tangu Kanisa kuu la Casamari lilipotabarukiwa na hivyo kutengwa rasmi kuwa ni nyumba ya ibada na sala. Kardinali Parolin, ameadhimisha Ibada hii kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa kukazia umuhimu wa Neno la Mungu katika ujenzi wa mji wa binadamu. Ujenzi wa Kanisa hili ulichukua muda wa miaka kumi na mitano na kuwekwa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni; Watakatifu Yohane na Paulo pamoja na wafiadini wa Roma.

Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa waamini kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu. Waamini wanapaswa kukita maisha yao katika Injili ya Kristo, ili waweze kukua na kukomaa katika: imani, matumaini na mapendo, ili kwa pamoja waweze kuimarishwa na Neno la Mungu. Waamini wawe ni mashuhuda wa: ukweli, haki na amani ili kuimarisha lile Agano ambalo Mwenyezi Mungu alilifunga na Waisraeli.

Lakini leo hii, Agano hili linapata mwelekeo mpya unaowaambata watu wote, ili waweze kushiriki katika furaha na matumaini ya watu wa Mungu, tayari kujisadaka kama sadaka safi kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. Waamini wasaidie kuzima kiu ya haki na maisha, kwa kujitahidi kuwapeleka watu hawa kwa Kristo Yesu. Ujenzi wa nyumba ya ibada ni kielelezo endelevu cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake, tayari hata kwa waamini kuwa ni mawe hai yanalolijenga Kanisa la Kristo aliyeteswa akafa na kufufuka kwa wafu. Kanisa ni kielelezo hai cha Fumbo la Pasaka. Yeye ndiye lile jiwe lililokataliwa na waashi, lakini sasa limekuwa ni jiwe kuu la pembeni na lenye thamani machoni pa Mungu.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu ndiye msingi thabiti wa Kanisa lake, mwaliko kwa waamini wote kuendelea kumjongea Kristo, ili aweze kuwatumia kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa. Ni dhamana na kazi ya Roho Mtakatifu anayeendelea kulijenga na kuliimarisha Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika! Hawa ndio wale wateule wa Mungu, wanaoitwa kutoka katika giza la dhambi na mauti na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka na hivyo kuunda taifa jipya la watu wa Mungu ambaye anataka kufunga Agano Jipya la milele na watu hawa!

Hii ni Jumuiya ya waamini wanaokiri na kushuhudia katika maisha yao, Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, Kristo Yesu ndiye Mkombozi wa ulimwengu! Kardinali Parolin anahitimisha kwa kusema, hii ndiyo imani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.