2017-09-18 13:36:00

Papa Francisko: Waamini mnayo dhamana ya kuwaombea viongozi wenu!


Wakristo wanayo dhamana na wajibu wa kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wao wa serikali hata kama wanakabiliwa na udhaifu wao wa kibinadamu. Kushindwa kutekeleza wajibu huu muhimu ni dhambi. Viongozi wa Serikali kwa moyo wa unyenyekevu wanapaswa pia kuomba sala na dua kutoka kwa wananchi wao ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya sheria na katiba ya nchi zao, ili waweze kutenda yote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mtume Paulo anamtaka Timotheo kuwahamasisha Wakristo kusali kwa ajili ya viongozi wao, ili amani na utulivu; ibada na uchaji viweze kutawala katika nyoyo za watu, kwani Mwenyezi Mungu anataka watu wote waokoke na kupata kujua yaliyo ya kweli.

Katika Injili, Kristo Yesu anashangazwa  sana na: imani, unyenyekevu, upendo kwa Mungu na jirani pamoja na mshikamano wa akida na watu aliokuwa anawaongoza na kuwasimamia. Akida aliishi vyema na watu hata kama alikuwa ni mgeni kati yao na kwamba, alimpenda sana mtumwa wake, kiasi cha kutuma wazee kwenda kumwombea huruma kwa Kristo Yesu. Akida alitambua kwamba, licha ya mamlaka makubwa aliyokuwa nayo, lakini bado alihitaji neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu. Alitambua pia nguvu na mamlaka yaliyokuwa juu yake, kiasi cha kujinyenyekesha ili kusali na kuomba msaada. Huu ni mwelekeo chanya kwa viongozi wanaotambua uwezo wa Mungu katika dhamana na utume wao, tayari kumwomba, ili awasaidie kuongoza watu wao!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 18 Septemba 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Kiongozi asiye Sali atajikuta anajifungia katika ubinafsi na chama chake, kiasi cha kushindwa kutoka katika hali na mazingira kama haya. Lakini, kiongozi anayeona matatizo na changamoto za maisha ya watu wake, yuko tayari kujinyenyesha, ili kuomba msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hivi ndivyo alivyofanya Mfalme Sulemani katika maisha yake, alipomwomba Mwenyezi Mungu hekima ya kuongoza watu wake vyema! Hakumwomba Mungu dhahabu, mali na utajiri bali hekima! Hii ni changamoto kwa viongozi wa Serikali kuwa ni watu wa sala na wachamungu, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao vyema.

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga utamaduni wa kusali kwa ajili ya kuwaombea viongozi wao, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya mapenzi ya Mungu. Wasali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani, kwa wale viongozi ambao wanakwenda kinyume cha taratibu, kanuni na katiba za nchi zao. Lengo ni kuwawezesha viongozi hawa kama anavyosema Mtakatifu Paulo, kuwa ni vyombo vya haki, amani na utulivu. Kusali kwa ajili ya kuwaombea viongozi wa serikali ni dhamana na wajibu wa Wakristo, kwa wale wasiosali ni dhambi wanayopaswa kwenda kuiungama mbele ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.